Polisi Moro |
Mtibwa Sugar |
Mechi hiyo itafanyika katika uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Morogoro kuanzia saa 10 kwa kiingilio cha sh 1,000.
kwa mujibu wa taarifa iliotolewa na Afisa habari wa Shirikisho la soka nchini TFF Boniface Wambura alisema tiketi za mechi hiyo zitaanza kuuzwa leo kupitia mtandao wa M-Pesa, CRDB Simbanking na maduka 30 ya Fahari Huduma yaliyopo katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro.
Alisema mashabiki 100 wa kwanza watakaoanza kuingia uwanjani wapata jezi za timu ya Mtibwa Sugar na Polisi Morogoro.
Aliongeza kusema kusema tayari mechi ya majaribio ya tiketi za elektroniki imeshafanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ambapo timu za Tanzania Prisons na Mbeya City zilichuana na kutoka sare.
Alisema mechi nyingine za majaribio ya tiketi za elektroniki zinatarajiwa kuchezwa Agosti 30 mwaka huu.
Alisema katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kutakuwa na mechi kati ya Coastal Union na Mgambo Shooting wakati katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ni Kagera Sugar dhidi ya mabingwa wa Mkoa wa Kagera, Eleven Stars.
Wambura alisema Septemba 6 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa kutakuwa na mechi kati ya Simba na Mtibwa Sugar.
Alisema mchezo wa ngao ya Jamii utakaozikutanisha timu ya Azam FC na Yanga afrika umepangwa kufanyika Septemba 13 katika Uwanja wa Taifa,uliopo jijini Dar es Salaam.
Mtibwa inatarajiwa kuanza ligi kwa kuikaribisha Yanga kwenye uwanja wa Jamhuri wakati Polisi Moro itakaribishwa tena katika ligi kwa kuumana na Azam kwenye uwanja wa Chamazi Septemba 20.
Wakati huo huo waamuzi wanaotarajia kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu huu watafanya mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) mwezi ujao.
Mtihani huo utahusisha waamuzi wa daraja la kwanza (class one) wakiwemo wale wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la soka duniani (FIFA).
Alisema mbali ya mtihani huo unaotarajiwa kufanyika kabla ya Septemba 10 mwaka huu, kutakuwa na semina ya makamishna ambao watasimamia mechi za VPL na FDL.
Alisema waamuzi wote wanatakiwa kutumia muda uliobaki kufanya maandalizi kwa ajili ya mtihani huo.