STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, August 4, 2012

Mfano yaingiza sokoni Jasho la Mnyonge

FILAMU mpya iliyoandaliwa na kampuni ya uandaaji na usambazaji wa filamu ya Mfano Entertainment na kupewa jina la 'Jasho la Mnyonge' imeingizwa sokoni. Mkurugenzi wa kampuni hiyo na mtunzi wa filamu hiyo, Said Muinga 'Dk. Mfano', alisema filamu hiyo yenye ujumbe mahususi kwa jamii kuhusiana na vitendo viovu tayari ipi sokoni katika mikoa mbalimbali. Alisema kuwa filamu hiyo inaonyesha jinsi gani imani haba za kutaka utajiri wa haraka haraka inavyoweza kupelekea mauaji ya kutisha hasa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino). Muinga alisema kuwa kupitia katika filamu hiyo Watanzania watajionea jinsi wanavyoweza kujiingiza kwenye vitendo vya mauaji kwa ajili ya kujipatia utajiri wa haraka kutokana na kudanganywa na waganga 'feki' wa kienyeji. "Tumeingiza sokoni filamu yetu mpya ya 'Jasho la Mnyonge' , hivyo wapenzi wa filamu nchini ambao walikuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa wanaweza kuipata kupitia kwenye maduka mbalimbai yanayojihusisha na uuzaji wa filamu, "alisema Muinga ambaye miezi kadhaa iliyopita aliingiza sokoni filamu nyingine ya 'Yai Viza' ambayo inaendelea kufanya vizuri kwa mauzo. Alisema kuwa zoezi la upigaji picha za filamu hiyo lilifanyikia katika maeneo mbalimbali kulingana na ujumbe husika ikiwemo kwenye misitu mikubwa, maeneo ya vijijini na mjini. Muinga alisema kuwa katika filamu hiyo amewashirikisha wasanii 'mastaa' pamoja na chipukizi lakini ambao wamefanya vizuri katika nafasi zao walizocheza.

Mwanahawa Ally 'Chipolopolo'; Binamu wa Mchizi Mox anayemzimia Barthez, Yanga

HAKUNA kinachomliza muimbaji anayekimbiza nchini kwa sasa katika miondoko ya taarab, Mwanahawa Ally 'Chipolopolo' kama kumshuhudia baba yake mzazi, Ally Rashid 'Mwana Zanzibar' akitelekezwea na baadhi ya wadau na wanamuziki wenzake. Mwanahawa alisema baba yake aliyewahi kutamba na bendi za Urafiki Jazz, Bima Lee, Shikamoo Jazz na Msondo Ngoma, kama mpuliza 'saksafone', alipatwa na kiharusi karibu miaka mitatu iliyopita alipoanguka ghafla akienda mazoezi ya bendi ya Msondo. Alisema tangu apate maradhi hayo baba yake hawezi kutembea wala kuzungumza akijiuguza nyumbani kwake, Keko Machungwa huku hakuna yeyote anayeenda kumjulia hali. Mwanahawa alisema kitendo hicho mbali na kumtia simanzi, pia kinampa somo kubwa katika shughuli zake za muziki akiamini thamani ya msanii huwa ni pale tu anapokuwa mzima kiafya na si vinginevyo. Alisema, cha kustaajabisha ni kwamba baadhi ya wanamuziki aliofanya kazi na babaye wanaishi karibu eneo la Keko Machungwa, lakini hawana muda wa kwenda kumjulia hali kujua anaendeleaje. "Kwa kweli hali inayomkuta baba inaniumiza na kuonyesha jinsi gani wanamuziki tusivyopendana wala kuthaminiana, tunapendana kinafiki hasa tukiwa wazima, wakati wa matatizo kila mtu hujifanya yupo 'bize', hii sio sawa inaondoa upendo baina yetu." Mwanahawa aliyepitia makundi ya Dar Modern, Zanzibar Stars, Super Shine kabla ya kupaishwa na kundi King's Modern 'Wana Kijoka Chazima Taa', alisema lazima wadau na wasanii nchini wabadilike. "Tubadilike na kusaidia kwa hali na mali muda wakati wote, kila nimuonapo baba jinsi anavyoshindwa kutembea na kuzungumza roho inaniuma kwa uchungu," alisema. URITHI Mwanahawa Ally aliyebatizwa jina la Chipolopolo alipokuwa Dar Modern ili kutofautishwa na mkongwe Mwanahawa Ally, alizaliwa mwaka 1986, Jang'ombe Zanzibar akiwa ni mtoto wa pili kati ya wanne kwa mamaye na wa saba kati ya tisa kwa baba yake aliyeoa zaidi ya mke mmoja. Alisoma Shule ya Msingi Mgulani, kabla ya kutumbukia kwenye muziki akifuata nyayo za babaye na binamu yake Taikun Ally 'Mchizi Mox'. Licha ya kurithi kipaji cha muziki toka familia yake, alikiri kuvutiwa kisanii na Zuhura Shaaban na kupenda kuimba nyimbo za wajina wake, Mwanahawa Ally kulichangia kujitosa kwake kwenye uimbaji. "Tangu utotoni nilipenda kusikiliza na kuimba nyimbo za Mwanahawa Ally na nilivutiwa na Zuhura Shaaban ninayemzimia mpaka leo kuliniingiza kwenye uimbaji, ingawa wazazi wangu hasa baba walichangia mimi kuingia katika fani," alisema. Safari yake kisanii ilianza mwaka 2005 wakati mama yake alipompeleka East African Melody kufanyiwa usaili na aliposhindwa kuchukuliwa alikimbilia Zanzibar Stars na kupokewa akipewa nafasi ya kuimba nyimbo za 'kopi'. Mwaka 2009 aliondoka ZNZ Stars na kutua Super Shine ambako pia hakupewa nafasi na lilipoanzishwa kundi la Victoria Modern mwaka 2010, alitua huko na kufyatua nao nyimbo mbili za 'Mtoto Kibamba Best' na 'Habib Chocolate'. Victoria liliposambaratika mwaka jana kulimfanya Mwanahawa anayependa kula wali 'ndondo' kwa samaki na kunywa juisi ya embe, kujiunga na King's Modern na jina lake kung'ara kupitia nyimbo za 'Dunia Duara' na 'Mchumia Juani'. Baada ya King's kumng'arisha jambo ambalo linamfanya kutolisahau kundi hilo na hasa mkurugenzi wake, Hamis Mshewa 'Majaliwa' wiki iliyopita alinyakuliwa na T-Moto kwa alichodai kusaka masilahi zaidi akitarajiwa kutambulishwa rasmi Sikukuu ya Idd. "Ukiwaondoa wazazi wangu, anayefuatia kwa shukrani ni Mkurugenzi wangu wa zamani Majaliwa na mchumba'ngu Juma Majala kwa walivyonisaidia kisanii," alisema. BARTHEZ Mwanahawa, anayekerwa na baadhi ya wasanii wa taarab kutojiheshimu na kupenda kuimba 'vijembe', alisema yeye ni 'kichaa' wa soka akiishabikia klabu ya Yanga. Alisema anayemzimia katika kikosi hicho ni kipa Ally Mustafa 'Barthez' hasa kwa alivyoisaidia Yanga kutwaa taji la michuano ya Kagame 2012. "Naipenda Yanga na ninamzimia Barthez, sio siri kipa huyu na wachezaji wengine walitubeba katika Kagame kwa kutimiza wajibu wao uwanjani," alisema. Mwanahawa anafurahia sanaa kumwezesha kununua kiwanja kilichopo Gongolamboto na kumiliki 'Video Library', alizungumzia muziki wa Bongofleva akidai ni mzuri akimtaja Ally Kiba kama anayemzimia kisanii. Hata hivyo alisema muziki huo na wasanii wake wanapaswa kubadilika kwa kuachana na tabia ya kufanya maonyesho yao kwa 'play back' badala yake wapige 'live'. "Wakiachana na mtindo huo watatamba sana, ila kwa sasa itawachukua muda mrefu kutufikia sisi wengine mahali tulipo kimuziki," alisema. KIDUKU Mwanahawa ambaye hajaolewa ingawa ana watoto wawili, Salma, 8 anayesoma darasa la nne na Mahmoud,4 aliyepo chekechea, alisema ubunifu uliofanywa na makundi ya taarab ya kuwa na vijana wa kucheza 'kiduku' umesaidia kuinua soko la muziki huo. Alidai wanaoponda mtindo huo wanashindwa kuelewa kuwa dunia imebadilika, licha ya kukiri suala la kutojiheshimu kwa baadhi ya wanamuziki na mashabiki wa taarab hasa katika mavazi na uchezaji unapunguza ustaarabu uliozoeleka. Mwanadada huyo anayechizishwa na rangi nyekundu, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama aliposhindanishwa na wakali wa taarab nchini Khadija Kopa, Mariam Khamis 'Paka Mapepe na Isha Mashauzi katika shindano la Nani Mkali. Matarajio ya kimwana huyo anayependa kutumia muda wake za mapumziko kujitenga na watu ili kutuliza kichwa chake, ni kuja kutamba kimataifa na kupanua biashara zake pamoja na kuanzisha asasi ya kusaidia watu wenye matatizo. Mwanahawa aliyekitaja kibao cha 'Dunia Duara' kama bomba kwake, alizungumzia ugonjwa wa Ukimwi, akisema ni tishio na jamii iache kuuchezea akiwataka watu wawe makini kwa kujiheshimu na kujikinga nao akisisitiza watu kuwa waaminifu. Mwisho