|
Drogba akifunga mkwaju wa penati kuiandikia Chelsea bao la pili |
|
Messi akishangilia bao lake dhidi ya Ajax jana |
KLABU za Chelsea na Bayern Munich zimefanya mauaji katika mechi zao za Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, huku Barcelona nayo wakitakata nyumbani katika mfululizo wa mechi hizo.
Bayern iliitambia As Roma nyumbani kwao kwa kuilaza mabao 7-1, wakati Chelsea ikiiua Malboro kwa mabao 6-0 huku mkongwe Didier Drogba akishuhudiwa akifunga bao kwa mkwaju wa penati.
Mabao mengine ya Chelsea katika mchezo wao yalifungwa na Loic Remy dakika ya 13 kabla ya kuumia na kutoka dakika tatu baadae na kuingia Drogba aliyefungwa bao la pili dakika ya 23 kwa penati.
Beki John Terry aliiongezea Chelsea bao la tatu dakika ya 31 akimalizia kazi ya Cesc Fabregas mabao yalidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Waswidish kujifunga kupitia mchezao wao Viler dakika ya 54 na Eden Hazard akaongeza mengine mawili dakika ya 77 kwa mkwaju wa penati na dakika ya 90.
Katika pambano jingine Bayern Munich ilitoa kipigo kikali kwa AS Roma ikiwa kwao Italia kwa mabao 7-1 Arjen Robben akianza kuandika bao dakika ya 8 akimalizia kazi nzuri ya Phillip Lahm kabla ya Mario Gotze kuongeza la pili dakika ya 23 kwa pande la Thomas Muller.
Dakika mbili baadaye Robert Lewandowski aliongeza bao la tatu kwa pande la Juan Bernat kabla ya Robben kurudi tena kambani kwa mabao la nne kwa kazi nzuri ya Lewandowski na mkwaju wa pwanti uliopigwa na Thomas Muller uliifanya wageni iende mapumziko ikiwa mbele kwa 5-0.
Gervinho aliifuta machozi Roma kwa kufunga bao dakika ya 66 kabla ya Wajerumani kurudi tena kuwaadhibu kwa mabao mawili mengine ya Franck Ribery aliyefunga dakika ya 78 na Xherdan Shaqiri dakika ya 80.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo la E, Manchester City iling'ang'aniwa na CSKA Moscow na kutoka nao sare ya 2-2.
Katika mfululizo wa mechi nyingine PSG ikiwa ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APOEL, huku Barcelona ikishinda nyumbani mabao 3-1 dhidi ya Ajax, Schalke 04 ikitamba nyumbani mabao 4-3 dhidi ya Sporting na Shakhtar Donetsk ikishinda ugenini mabao 7-0 dhidi ya BATE na Porto iliitambia Athletic Bilbao 2-1.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea tena usiku wa leo kwa michezo kadhaa ya kusisimua.
Atlético Madrid itakuwa nyumbani kuvaana na Malmö FF, wagiriki wa Olympiakos Piraeus itaikaribisha Juventus, Ludogorets itaumana na Basel wakati Liverpool itaumana na Real Madrid katika pambano la aina yake, huku Bayer Leverkusen itaikaribisha Zenit.
Klabu ya Monaco ambayo bado haijasimama vema itavaana na Benfica wakati Anderlecht itakuwa wenyeji wa Arsenal na Galatasaray itaumana na Borussia Dortmund.