Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are 'Mzee Kinesi' |
WAKATI uongozi ukiupinga mkutano wa wanachama uliopangwa kufanyika kesho ukidai sio halali, wanachama waliouandaa mkutano huo wamesisitiza kesho piga ua lazima wakutane kwani wala kila baraka za kufanyika kwake.
Mratibu wa mkutano huo wa dharura, Mohammed Wandi amesisitiza kuwa kauli za uongozi kuupinga uongozi huo ni kutaka kuwayumbisha wanachama kwani ukweli mkutano huo utafanyika kama ulivyopangwa na tayari wanachama mbalimbali toka ndani na nje ya Dar wameshawasili jijini.
Wandi alisema wamepata baraka zote za kufanyika kwa mkutano huo ikiwemo vibali toka Manispaa ya Ilala na Jeshi la Polisi na kwamba mkutano huo ni wa amani na utulivu na kushangaa uongozi wa Simba kupitia Kaimu Makamu Mwenyekiti, Joseph Itang'are 'Kinesi' kuukana.
"Mkutano upo kama kawaida kesho na wanachama wa Simba wajitokeze kwa wingi kwenye Hoteli ya Starlight, wasisikie propaganda kwa vile tumezingatia katiba," alisema Wandi.
Wandi alisema kuwa mkutano wao wameuitisha kwa kuzingatia katiba na hivyo hawaoni sababu ya uongozi kuwa na presha wakati wenyewe waliridhia ombi lao la kutaka mkutano kwa lengo la kuinusuru timu yao.
Alisema kabla ya kuamua kuitisha mkutano huo, Mzee Kinesi na Mwenyekiti wa Kamati ya ushindi Simba, Rahma Al Kharoos 'Malkia ya Nyuki' walikutana nao na kuwaeleza wamemaliza tofauti zao hasa baada ya kuamua kulifungua Tawi la Mpira Pesa lililokuwa limefungiwa na kuruhusu mkutano.
"Mkutano huu sio wa kufukuza viongozi, tutawasilisha hoja mezani na viongozi wakishindwa kuzijibu basi ndiyo itakuwa kwaheri yao," alisema.
Pia alisisitiza kuwa mkutano wao haukuitishwa na tawi lao la Mpira Pesa, bali umeitishwa na wanachama wa Simba na wamewaalika viongozi wahudhurie na kujibu maswali ya wanachama hao.