STRIKA
USILIKOSE
Monday, December 10, 2012
Peter Manyika: 'Straika' wa zamani anayefuata nyayo za baba yake
HANA muda mrefu tangu alipotumbukia katika soka, lakini kipaji kikubwa cha alichonacho cha soka kimeanza kumtabiria kuja kuwa nyota kama baba yake aliyewahi kung'ara na timu za Mtibwa Sugar, Yanga na Taifa Stars.
Peter Manyika, ndiye kipa namba moja kwa sasa wa timu ya taifa ya vijana ya U17 'Serengeti Boys' iliyozikosa kiduchu fainali za Afrika zitakazochezwa mwakani nchini Morocco baada ya kujikwaa kwa vijana wenzao wa Kongo.
Manyika, mtoto wa kwanza wa nyota wa zamani, Manyika Peter ndiye aliyekaa langoni katika mechi zote dhidi ya Kondo ikiwemo ile ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kipigo cha mabao 2-0 ugenini wiki iliyopita.
Kipa huyo anasema mechi ya pili dhidi ya Kongo ndiyo mechi itakayobaki kichwani mwake kama tukio la huzuni kwa kushindwa kuisaidia Serengeti Boys kurejea tukio la mwaka 2004 kufuzu fainali za Afrika kabla ya kutolewa.
Manyika aliyeanzia kucheza kama mshambuliaji wa kati kabla ya kubadilishwa namba akiwa Shule ya Msingi, baada ya kipa wao kuumia na yeye kuhamishiwa langoni na kung'ara, anasema vurugu walizofanyiwa Kongo hatazisahau.
"Kwa kweli fujo na vitimbi tulivyofanyiwa Kongo ni mambo yanayonifanya nishindwe kuisahau mechi hiyo kwani hatukutarajia kama tungerudi salama kwa namna walivyotufanyia 'unyama' ndani na nje ya uwanja," anasema.
Manyika, anayetarajiwa kuibukia timu ya U20 ya Mgambo Shooting katika michuano ya Kombe la Uhai baada ya kuachana na JKT Ruvu, anasema kwa tukio la furaha hakuna kama alipoitwa timu ya taifa na kuwa kipa namba moja.
"Sio siri kuitwa kwangu Serengeti Boys kulikuwa kwa kushtukiza sikutarajia na furaha zaidi ni kuwa kipa namba moja wa timu hiyo," anasema.
Manyika anasema japo anajiamini ana kipaji cha soka cha kuzaliwa na kurithi toka kwa baba yake, lakini hakutarajia mafanikio hayo ya mapema.
CASILLAS
Manyika anayemtaja mjomba wake, David 'Mzee wa Yeah' na Method kama walioibua na kukiendeleza kipaji chake kabla ya baba yake kutia nguvu, anasema alivutiwa kisoka na nyota wa zamani wa Brazil, Ronaldo de Lima na kujikuta akicheza kama mshambuliaji wa kati.
Anadai hata hivyo alipohamia kwenye ukipa amehamisha mapenzi kwa kipa Joe Hart na Ike Casillas aliyedai ndiyo kiigizo chake huku akimzimia pia Yew Berko wa Yanga.
Manyika anayependa kula ugali kwa dagaa na mlenda na kunywa Fanta, anadai japo Ronaldo kastaafu soka bado anaendelea kuwa mchezaji bora kwake kuwahi kumuona kutokana na umahiri wake wa kufumania nyavu.
Akiwa na ndoto za kucheza soka la kulipwa, Manyika anayesoma kidato cha tatu kwa sasa katika Shule ya Sekondari Kizuka iliyopo Morogoro, anasema kipindi kifupi alichokuepo katika soka amenufaika kwa mambo mengi.
Anadai kutumainiwa na taifa, kumudu maisha kwa kujinunulia vitu bila kutegemea wazazi na kusafiri sehemu mbalimbali ni baadhi ya mafanikio hayo.
Manyika anasema donge nono kulipata ni Sh 540,000 alizopata hivi karibuni na kutumia kununua godoro, runinga na deki yake na matumizi mengine.
"Nashukuru fedha hizo zimenifanya niwe kila kitu cha kuanzia maisha kwani mama yangu alinichongea pia kitanda. Huwezi amini awali hakupenda kabisa nicheze soka ila kwa sasa ananiunga mkono," anasema.
NDOTO
Manyika anayezishabikia Yanga, Barcelona na Real Madrid akiwazimia Dimitar Babatov na Ronaldo, anasema japo Serengeti Boys imeshindwa kufuzu fainali za Afrika anadhani itafanya hivyo baadaye.
Pia anasema anaamini Taifa Stars chini ya Kim Poulsen ikijipanga vema inaweza kufuzu fainali za Kombe la Dunia na za Afrika kwa vile kocha huyo ni mjanja, mjuzi na mwenye malengo mazuri.
"Kim nimefanya naye kazi ni bonge la kocha na watanzania tunapaswa kumuunga mkono na kumkumbatia kwani anaweza kutupeleka mbali, hata fainali za Dunia, muhimu tujipange, japo watu wanaona ni ngumu."
Manyika anayemtaja John Bocco kama nyota anayemzimia Bongo, anadai wakati anaibukia katika soka hakutaka kabisa kutumia mgongo wa baba yake mpaka alipogundua kama amejitosa kwenye mchezo huo.
"Huwezi amini aliyenisaidia kufika hapa ni mjomba wangu Mzee Yeah, baba alikuja kuwa msaada wa kuninunulia vifaa baada ya kutambua nimejitosa kurithi kipaji chake."
Anaongeza kwa kuwashukuru wawili hao, pia mama yake kipenzi, Method na, ndugu, jamaa na rafiki wote wanaomuunga mkono.
KIPAJI
Peter Manyika 'Casillas' alizaliwa Agosti 13, 1996 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza kati ya wawili wa familia yao, elimu yake ya Msingi aliisoma Shule ya Rutihinda kabla ya kujiunga na Kizuka Sekondari.
Kisoka, alianza makeke yake tangu shule ya msingi akicheza kama 'straika' kabla ya kuhamia kwenye ukipa, timu yake ya kwanza ya kueleweka ikiwa ni Zaragoza ya Magomeni kabla ya kutua kituo cha soka cha Twalipo.
Anasema akiwa na kituoni hapo mwaka jana aling'ara katika michuano ya Airtel akiichezea Shule ya Jitegemee kisha kutua JKT Ruvu U20 na kuichezea katika Kombe la Uhai.
Baadaye Juni mwaka jana aliitwa Serengeti Boys na kumudu nayo mpaka sasa na hivi karibuni ameelekea Mgambo Shooting U20 atakaoicheza katika michuano ya Uhai 2012.
Akiowa na ndoto za kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa, Manyika hutumia muda wake wa ziada kusikilia muziki, kuangalia muvi na anadai soka la Bongo lipo juu hasa baada ya vijana kupewa nafasi ya kuonyesha vipaji vyao.
Anasema kama hali hiyo ikiendelea Tanzania itafika mbali, japo ametaka wadau wa soka kuwekeza zaidi na kudhamini klabu zote bila ubaguzi pia akitaka kuongezeka kwa michuano mingi zaidi ya ile ya ligi.
Juu ya Simba na Yanga, kinda hilo linalowasihi wachezaji wenzake kuzingatia mazoezi na kulitumaini soka kama ajira zao zinazoweza kuwatoa kimaisha anasema hana papara za kuzikimbilia kwa vile anataka kwanza kujenga jina.
"Simba na Yanga kwa sasa ni kubwa mno kwangu, labda baadaye tena kwa kuridhishwa na masilahi, napenda zaidi kucheza nje ya nchi au klabu isiyo na presha kubwa kama vigogo hao," anasema.
MESSI AVUNJA REKODI YA GERD MULLER, FALCAO NOMA
Asante Mungu nimempita Gerd Muller... mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi akishangilia goli lake la 86 msimu huu jana usiku dhidi ya Real Betis. |
Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake matano dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0. |
Shujaa wa mabao MATANO, Radamel Falcao wa Atletico Madrid akishangilia moja ya mabao yake dhidi ya Deportivo Coruna jana usiku. Atletico walishinda 6-0. |
MADRID, Hispania
LIONEL Messi asiyezuilika ameweka rekodi mpya ya kufunga mabao mengi zaidi kwa mwaka mmoja wa kalenda katika historia ya soka duniani na kuwasaidia vinara ambao hawajapoteza mechi katika La Liga, Barcelona, kuendelea kuongoza kwa tofauti ya pointi sita juu ya Atletico Madrid kufuatia ushindi mgumu 2-1 ugenini dhidi ya Real Betis jana.
Mwanasoka Bora wa Dunia Messi alifunga goli lake la 85 na la 86 kwa mwaka 2012 katika mechi iliyojaa ushindani kwenye uwanja wa Benito Villamarin mjini Seville na kuipiku rekodi ya mabao 85 iliyowekwa na Mjerumani Gerd Mueller mwaka 1972.
Tukio hilo la kihistoria la Messi lilifunika mambo makubwa yaliyofanywa jana usiku na mshambuliaji Atletico, Radamel Falcao, ambaye mapema alifunga magoli matano peke yake wakati walipoisambaratisha timu inayoburuta mkia ya Deportivo Coruna kwa mabao 6-0 nyumbani.
Mshambuliaji huyo wa Colombia, anayefahamika kama 'the tiger' na ambaye anagombewa na klabu tajiri zaidi za Ulaya, alifikisha jumla ya mabao yake msimu huu kuwa 16 katika mechi 15 wakati Atletico ikidumisha tofauti ya pointi tano juu ya mahasimu wao wa mji mmoja Real Madrid.
Kikosi cha Jose Mourinho cha Real kililazimika kuzinduka kutoka nyuma mara mbili na kupata ushindi mgumu wa 3-2 ugenini dhidi ya Real Valladolid Jumamosi ambao uliwasaidia kupunguza pengo la pointi dhidi ya Atletico, ambao waliwafunga 2-0 wikiendi iliyopita, kuwa pointi mbili kwa usiku huo.
Hata hivyo, Atletico walijibu kwa kushinda mechi yao ya 12 katika 15 za ligi msimu huu dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Depor ambayo iko hatarini kurejea moja kwa moja daraja la pili.
Barca wameshinda mechi zao zote msimu huu ukiacha sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Real Madrid Oktoba na magoli mawili ya Messi yaliwafanya wafikishe pointi 43, huku Atletico wakiwa na pointi 37 na Real wana pointi 32. Betis ni wa tano wakiwa na pointi 25, sawa na wanaoshikilia nafasi ya nne Malaga, ambao waliwasambaratisha Granada 4-0 Jumamosi.
"Inaonekana kama jambo lisilowezekana kwamba yeye (Messi) anaweza kufunga magoli mengi kiasi hiki ndani ya mwaka mmoja lakini kuna mechi tatu zimebaki na tunatumai kwamba ataendelea kuongeza jumla ya mabao yake," kocha wa Barca, Tito Vilanova, aliuambia mkutano na waandishi wa habari.
"Tunatumai kwamba atakwenda mbali sana katika maisha yake ya soka kwa sababu bado ni mdogo sana," aliongeza. "Sidhani kama tutaona mchezaji mwingine kama yeye."
BETIS WASIO NA BAHATI
Kikosi cha Vilanova kiliwatawala Betis kama ilivyotarajiwa katika kipindi lakini wakapoteza umiliki baada ya mapumziko na mwamba wa lango uliinyima timu hiyo goli mara tatu.
Messi aliifikia rekodi ya Mueller wakati alipochukua mpira katika eneo la katikati katika dakika ya 16 na akaiacha safu ya ulinzi ya Betis ikiwa imesimama kabla ya kufunga kwa shuti la pembeni chini kulia.
Pasi ya 'akili' ya kisigino ya Andres Iniesta ilimpikia Messi goli la pili dakika tisa baadaye kwa shuti kali kutokea katika eneo lile lile la kwanza ndani kidogo ya boksi na mpira ukatumbukia kwenye kona ile ile ya lango.
Ruben Castro alirudisha goli moja kwa wenyeji katika dakika ya 39 na kufanya kipindi cha pili kuwa kigumu zaidi kwa wageni.
Messi alikaribia kufunga 'hat-trick' dakika tano kabla ya mechi kumalizika wakati alipopiga 'tikitaka' ya jirani na lango lakini kipa wa Beti, Adrian alipangua mpira huo ambao ulimrudia Jordi Alba ambaye shuti lake liligonga 'besela' na mpira kutoka nje.
Kipigo kilikuwa kigumu kwa Betis, ambao waliwachapa Real 1-0 nyumbani mwezi uliopita na kuwapa Barca moja ya mitihani migumu zaidi kufikia sasa msimu huu ambao ulistahili japo pointi moja.
Mshambuliaji wa Atletico, Diego Costa alirekebisha makosa ya kadi nyekundu aliyopewa Alhamisi kwenye Ligi ya Europa wakati alipofunga goli la kuongeza kwenye Uwanja wa Calderon kwa kichwa kutokana na kona iliyopigwa na Koke katika dakika ya 23.
Kiungo wa Depor, Juan Valeron alipiga kichwa kilichogonga nguzo dakika nne baadaye lakini Atletico waliongeza la pili wakati Falcao alipoikimbilia vyema pasi ya Koke na kufumua shuti la chini lililotinga kwenye kona ya wavu.
Mpira uliorushwa haraka kutokea kushoto dakika tatu kabla ya mapumziko ulimpikia goli la pili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 na akafumua shuti kali lililomshinda kipa Daniel Aranzubia kutokea kwenye kona ya eneo la penalti.
Falcao kisha akaangushwa ndani ya boksi na akafunga penalti hiyo katika dakika ya 64 na kukamilisha 'hat-trick' yake, akafunga kwa kichwa la nne na akakamilisha lake la tano katika dakika ya 71.
Yeye ni mchezaji wa kwanza kufunga magoli matano katika mechi ya La Liga tangu Fernando Morientes alipofanya hivyo kwa Real Madrid dhidi ya Las Palmas mwaka 2002.
MALLORCA AIBU
Real Mallorca waliendelea kuporomoka kuelekea kushuka daraja wakati walipofungwa 4-0 ugenini Levante, kikiwa ni kipigo cha nane katika mechi 10 walizocheza bila ya ushindi.
Obafemi Martins aliwafungia Levante goli la kuongoza kabla ya mapumziko na David Navarro, Ruben Garcia na Vicente Iborra walifunga katika kipindi cha dakika 10 katika kipindi cha pili.
Levante, ambao wamefuzu hatua ya 32-Bora ya Ligi ya Europa, wako katika nafasi ya sita wakiwa na pointi 24, huku Mallorca wakiwa katika nafasi ya 17 kwa pointi 13.
Timu inayochechemea ya Athletic Bilbao ilipata ushindi wa tano tu msimu huu wakati waliposhinda 1-0 nyumbani dhidi ya Celta Vigo.
Goli la kichwa la Aritz Aduriz katika dakika ya 33 liliamua mechi kwenye uwanja wa San Mames na kuiinua Bilbao hadi nafasi ya 13 wakiwa na pointi 18 points. Celta wako katika nafasi ya 15 kwa pointi 15.
Manyika Jr bado aliota pambano la Kongo
KIPA namba moja wa timu ya taifa ya vijana U17 'Serengeti Boys', Peter Manyika 'Casillas' amesema itamchukua muda mrefu kusahau matukio waliyofanyiwa na wenyeji wao Kongo katika pambano lao la marudiano la kuwania kucheza fainali za Afrika.
Manyika, alisema vitisho na fujo walizofanyiwa na wenyeji wao kabla na baada ya kuanza kwa pambano hilo, kwa kiasi kikubwa vilichangia timu yake kupokea kipigo cha mabao 2-0 na kung'olewa mashindano na kuzima ndoto za kufuzu fainali hizo za 2013.
Akizungumza na MICHARAZO katika mahojiano maalum nyumbani kwao, Kigogo jijini Dar es Salaam juzi, Manyika alisema ingawa hilo ndilo pambano lake la kwanza la kimataifa nje ya nchi, lakini hakuwaza kama angekutana na vitimbi kama hivyo ikizingatiwa michuano yenyewe ni ya vijana, pia wenzetu walipokewa vema hapa nchini.
"Kwa kweli niliingiwa na woga na hofu kubwa kwa namna wenyeji wetu walivyotufanyia vituko na fujo ambazo kwa kiasi fulani zilitupotezea umakini uwanjani, licha ya makocha kututia moyo kulipigania taifa," alisema.
Manyika, alisema anadhani kuna haja ya shirikisho la soka Afrika kuyaangalia matukio hayo waliyofanyiwa ikiwemo kupigwa kwa kocha wao msaidizi, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ili kuyakemea yasiweze kurudia tena kwani yanaweza kujenga uhasama usio na maana.
Serengeti Boys, walishindwa kurejea rekodi iliyowekwa na wenzao mwaka 2004 walipofuzu fainali hizo za Afrika za U17 kabla ya kuenguliwa kwa kosa la kuchezesha 'kijeba' Nurdin Bakar na nafasi yao kupewa Zimbabwe waliokuwa wamewatoa.
Mwisho
Miyeyusho, mtwanga Nassib na kutwa taji la WBF
Bondia Fransic Miyeyusho akionesha ufundi wake kwa kumtupia masumbwi Nassibu Ramadhani wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com |
Bondia Mohamed Matumla kulia akimuhadhibi Doi Miyeyusho wakati wa mpambano huo usiku wa kuamkia leo Matumla alishinda kwa K,O raundi ya pili Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com |
Bondia Juma Fundi kushoto na Fadhili Majia wakioneshana umwamba wa kutupiana masumbwi wakati wa mpambano wao uliofanyika mwishoni mwa wiki Majia alishinda kwa pointiPicha na www.superdboxingcoach.blogspot.com |
Bondia Fransic Miyeyusho kushoto akimwazibu mpinzani wake Nassibu Ramadhani kwa kumtupia makonde mazito wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com |
Bondia Fransic Miyeyusho akionesha ufundi wake kwa kumtupia masumbwi Nassibu Ramadhani wakati wa Mpambano wao wa kugombania ubingwa wa WBF uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Miyeyusho alishinda kwa T.K.O ya raundi ya kumi picha nawww.superdboxingcoach.blogspot.com |
Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara kulia akimvisha mkanda wa ubingwa wa WBF bondia Fransic Miyeyusho baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani kwa T.K.O raundi ya kumi kushoto ni promota wa mpambano huo Mohamed Bawaziri www.superdboxingcoach.blogspot.com |
Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mkangara kulia akimpongeza Bingwa wa ubingwa wa WBF bondia Fransic Miyeyusho baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani kwa T.K.O raundi ya kumi kushoto ni promota wa mpambano huo Mohamed Bawaziri www.superdboxingcoach.blogspot.com |
bondia Fransic Miyeyusho akiwa amebebwa juu akiwa na mikanda miwili alioshinda baada ya kumtwanga Nassibu Ramadhani picha nwww.superdboxingcoach.blogspot.coma |
BONDIA machachari wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Miyeyusho juzi alifanikiwa kutetea taji lake la Mabara la UBO na kunyakua taji jipya pia la Mabara la WBF baada ya kumtwanga kwa TKO 10 mpinzani wake Nassib Ramadhani.
Miyeyusho alimtwanga Nassib TKO hiyo katika raundi ya 10 katika pambano kali lililofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam na ikuhudhuriwa na viongozi na wanamasumbwi mbalimbali nyota nchini.
Pambano hilo lililoandaliwa na mratibu Mohammed Bawazir na lililokuwa la kwanza kwa mabondia hao lilikuwa na jumla ya raundi 12 uzito wa bantam na lilianza kwa Nassib kumpeleka puta mpinzani wake kwa makonde makali.
Hata hivyo kadri raundi zilivyokuwa zikisonga mbele Nassib alianza kuonekana kuishiwa pumzi hasa kuanzia raundi ya nane na kumpa nafasi mpinzani wake nafasi ya kusimama imara kabla ya kusalimu amri katika raundi ya 10.
Mara baada ya Miyeyusho kutangazwa kuwa mshindi alikabidhiwa mataji yake mawili na aliyekuwa mgeni ramsi, Waziri wa Habari Utamaduni, Vijana na Michezo Dk Funella Mukangara na kuamsha hoi hoi ukumbini hapo.
Kabla ya pambao hilo, kulikuwa na mapambano mengine ya utangulizi ambapo Mohammed Matumla ' Snake Boy Jr' alimpiga kwa KO Doi Miyeyusho, Deo Samuel alitoka sare na Freddy Sayuni ,Fadhil Majiha alimpiga kwa pointi Juma Fundi na Ibrahim Classic alimpiga kwa pointi Said Mungi.
Baadhi ya mashabiki waliofurika kwenye ukumbi huo waliwapongeza waratibu wa pambano hilo sawia na kuwasifu mabondia wote waliopigana siku hiyo husuisani kumwagia sifa Nassib wakidai ni 'bonge' la bondia licha ya kupoteza mchezo huo.
Mwisho
Subscribe to:
Posts (Atom)