STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 10, 2013

Prisons yazinduka, Toto, Mtibwa ngoma nzito

Kikosi cha Prisons Mbeya

WAKATI timu ya Toto African ikijitutumua mjini Manungu na kulazimisha sare ya mabao 2-2, vijana wa maafande wa Prisons Mbeya imezinduka nyumbani kwa kuicharaza Mgambo JKT ya Tanga kwa bao 1-0,
Toto ambayo kupitia kocha wake, John Tegete waliwatupia lawama waamuzi wa pambano hilo kwa kuyakataa mabao yao mawili na kisha wenyeji kupewa penati ya kitatanishi na kufanya Mtibwa kuongoza mabao 2-0 hadi wakati wa mapumziko.
Tegete alisema walifanikiwa kurejesha mabao hayo kipindi cha pili na kuambulia pointi moja iliyowafanya waendelee harakati zao za kujinusuru kushuka daraja.
Nao Prisons ikicheza nyumbani na kuilaza Mgambo kwa bao 1-0 katika pambano jingine la Ligi Kuu Tanzania Bara lililochezwa kwenye uwanja wa Sokoine, Mbeya, huku maafande wa Polisi Morogoro walishindwa kutamba nyumbani kwa kulazimishwa suluhu na Ruvu Shooting  kwenye uwanja wa Jamhuri.
Matokeo ya ya mechi hizo yameifanya Prisons kuchupa hadi nafasi ya 10 ya msimamo wakiishusha JKT Ruvu, huku Toto na Polisi wameendelea kusalia katika nafasi zao za awali, ila Mtibwa imeiporomosha Coastal Union kwa kufikisha pointi 33.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho kwa pambano moja tu litakalowakutanisha wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azama itakayoikaribisha African Lyon.
Mechi hiyo itachezwa kwenye uwanja wa Chamazi ambapo matokeo yoyote kwa Azam itaelekea kupunguza pengo lake la pointi dhidi ya vinara wa ligi hiyo Yanga.
 1.  Young Africans     21     15     4     2     37     12     +25    49 
2.  Azam                     21     13     4     4     36     16     +20    43    
3 . Kagera Sugar         22     10     7     5     25     18     +7      37     
4.  Simba                     21      9     8     4     30     19     +11     35
5.  Mtibwa Sugar         23      8     9     6     26     24     +2      33   
6. Coastal Union          22      8     8     6     23     20     +3     32    
7.  Ruvu Shooting        22      8     6     8     21     19     +2     30     
8.  JKT Oljoro FC        22      7     7     8     22     24      -2     28     
9. JKT Mgambo           22      7     3    12    14     22      -8     24
10.Tanzania Prisons     23      5     8     10     12     21     -9    23          11.Ruvu Stars               21     6     4     11     19     34     -15   22
12. Toto Africans          24    4    10     10     22     32     -10   22
13.  African Lyon         22     5     4     13     15     32     -17   19
14. Polisi Morogoro      23     3     10   10     11     21     -10   19

            

Rungu la TFF yazikong'ota Villa Squad, Kocha Rhino Rangers


Na Boniface Wambura
KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23 mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Pia klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.

Mchezaji wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh. 200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa Machi 16 mwaka huu.

Nao wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.

Klabu ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.

Vilevile Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.

Pia uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa mechi za FDL msimu ujao.

MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 11 mwaka huu) litakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF.

Barca, PSG ni kufa ama kupona leo, Juve kuizua Bayern?


Messi alipoichachafya PSG wiki iliyopita


BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi ameondolewa kutoka kuwa wa kwanza katika orodha ya nyota wa kikosi cha Barcelona hadi kuwa wa mwisho wakati klabu yake ikilazimika kusubiri taarifa ya mwisho ya daktari kuhusiana na hali yake kabla ya kuteremka dimbani katika mechi yao ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris St Germain (PSG) itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nou Camp leo.
Mwanasoka huyo bora wa mwaka wa Dunia anaendelea kuuguza jeraha la msuli wa paja alilopata mjini Paris wiki iliyopita, wakati alipofunga katika mechi yao ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya 2-2, ingawa Barca walithibitisha kuwa wanaweza kufanya vizuri pia bila kuwa naye baada ya kuisambaratisha Real Mallorca kwa mabao 5-0 katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania Jumamosi.
Licha ya kuchezesha kikosi dhaifu, vinara hao wa La Liga walionyesha kiwango cha juu kwenye Uwanja wa Nou Camp kutokana na 'hat-trick' ya Cesc Fabregas na mabao mengine mawili kutoka kwa Alexis Sanchez lakini PSG ni wagumu kulinganisha na 'vibonde' Mallorca wanaokamata mkia kwenye msimamo wa La Liga.
Barca wanaopewa nafasi kubwa ya kusonga mbele wanafukuzia taji lao la nne la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika misimu nane na Messi ndiye huwabeba kwa kuwatoka mabeki wa upinzani kwa chenga katika mechi zao kubwa na kuwatengenezea wenzake nafasi za kufunga au kuifanya mwenyewe kazi hiyo ya kupachika mabao.
Ule uwapo wa Messi tu uwanjani huwachanganya wapinzani kisaikolojia, wakiumiza vichwa juu ya namna ya kumdhibiti.
Muargentina huyo alifanya mazoezi mepesi ya viungo Jumapili na vyombo vya habari vya Hispania viliripoti kwamba alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliojitokeza kufanya mazoezi juzi licha ya timu hiyo kuwaruhusu wachezaji wote kupumzika .
Huku wakiwa tayari wamejihakikishia kutwaa ubingwa wa La Liga kutokana na kuongoza kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid wanaokamata nafasi ya pili wakati kila timu ikiwa imebakiza mechi nane, kocha  Tito Vilanova anaweza kuiongoza timu hiyo leo dhidi ya PSG.
Vilanova pia anatarajiwa kuamua ni nani amchezeshe na Gerard Pique katika sehemu ya ulinzi wa kati baada ya Javier Mascherano kuwa nje kutokana na jeraha na Carles Puyol yuko shakani kucheza baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.
Beki yosso asiye na uzoefu, Marc Bartra alicheza vizuri na Pique Jumamosi lakini beki kiraka wa pembeni, Adriano Correia anakaribia kuwa 'fiti' na hivyo anaweza kucheza au kupangwa tena kwa kiungo Alex Song katika nafasi hiyo ya beki wa kati.
"Tutaangalia wachezaji gani tulio nao dhidi ya PSG," kocha msaidizi wa Barca, Jordi Roura alisema jana.

SILVA APONA
Beki wa kati aliye tegemeo PSG, Thiago Silva amejumuishwa kikosini kufuatia unafuu alio nao wa jeraha la goti alilolipata katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Barca na kukosa mechi ya Jumamosi waliyoshinda 2-0 dhidi ya Rennes kwenye Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa.
Kocha wa PSG, Carlo Ancelotti alikuwa na wachezaji saba wa kikosi cha kwanza ambao aliwaanzisha benchi au kutowajumuisha kabisa katika kikosi kilichochea Jumamosi wakati wakijiandaa kwa mechi ya leo.
Ancelotti, hata hivyo, atakuwa na kazi ya kuziba pengo la kiungo wake 'ngangaro' Blaise Matuidi ambaye ataikosa mechi ya leo kwa sababu ya kutumikia adhabu.
David Beckham anatarajiwa kuanza baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi yao ya kwanza, huku viungo wengine wakitarajiwa kuwa kati ya Muitalia Marco Verratti na Mfaransa Clement Chantome.
Kiungo wa kimataifa wa Italia, Thiago Motta anaweza pia kuziba nafasi ya Matuidi lakini hadi sasa amecheza mechi moja tu katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili iliyopita kwa sababu ya jeraha.
Kiwango cha juu alichoonyesha Jeremy Menez dhidi ya Rennes hakitoshi kumfanya apate namba katika kikosi kitakachoanza na kuwaweka kando Ezequiel Lavezzi au Lucas Moura. Beki wa kati, Alex amepona pia jeraha la goti na amejumuishwa kikosini.
"Tunapaswa kuichukulia kuwa ni siku muhimu kwetu. Tuko katika hatua isiyokuwa ya kawaida kwetu," mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo aliviambia vyombo vya habari vya Ufaransa.
"Barcelona wako katika mwaka wa 20 wa mradi wa kujenga timu yao. PSG imeanza ukurasa mpya katika historia yao lakini timu yao imeanza kujifua pamoja miezi 20 tu iliyopita."
Mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya leo itakuwa ni kati ya Bayern Munich na Juventus. Katika mechi yao ya kwanza wiki iliyopita, Bayern waliutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0. 

Juve maarufu kama kibibi kizee cha Turin watakuwa wakihitaji ushindi mnono ili kuwang'oa mabingwa hao wapya wa Ujerumani ambao msimu huu wameonekana kuwa moto mkali.

Filamu ya After Death kutolewa hadharani Mei



FILAMU maalum kwa ajili ya kumuenzi marehemu Steven Kanumba iitwayo 'After Death' iliyozunduliwa kwa kishindo wakati wa hafla ya 'Kanumba Day' inatarajiwa kuachiwa rasmi mwezi ujao.
Kwa mujibu wa waandaaji, filamu hiyo itatoka Mei kwa lengo la kutoa fursa ya kazi mpya ya marehemu Kanumba ya 'Love & Power' iliyozinduliwa pamoja Aprili 7 kwenye viwanja vya Leaders itambe sokoni ikitarajiwa kuachiwa rasmi sokoni Ijumaa hii.
Muongozaji wa filamu hiyo ilitungwa na Jacklyne Wolper, Leah Richard 'Lamata', alisema licha ya mashabiki waliofika Leaders kushuhudia uzinduzi wa filamu hizo kuitaka kuinunua, walikwama kwa vile muda wake wa kuitoa bado.
Lamata alisema mashabiki hao wanapaswa kuwa na subira mpaka mwezi ujao kazi hiyo itakapoachiwa rasmi kulingana na ratiba iliyopo.
"Tunashukuru tumefanikiwa kuwaonjesha ladha na kupokewa vyema kwa filamu hii, lakini mashabiki wanapaswa kusubiri hadi Mei tutakapoiachia rasmi," alisema Lamata.
Filamu hiyo inayoakisi maisha baada ya Kanumba kufariki, imewashirikisha wasanii kadhaa wakiwamo chipukizi waliotamba katika 'This is It' na 'Uncle JJ', Khanifa Daud 'Jennifer' na Othman Njaidi 'Patrick'.
Wengine walioigiza filamu hiyo ni Philemon Lutwazi 'Uncle D', Irene Paul, Patcho Mwamba, Mainda Suka, Shamsa Ford, Jacklyne Wolper na Stanley Msungu.

Victoria Sound yakamilisha mpya za albamu yake

 
Mwinjuma Muumin anayeiongoza Victoria Sound

BENDI ya Victoria Sound imekamilisha wimbo mpya wa albamu yao ya kwanza wanayotarajia kuitoa hivi karibuni, pia wakiwa mbioni kurekodi video yao ya pili ya wimbo wa 'Mwisho wa Siku'.
Mkurugenzi wa bendi hiyo, Mwinjuma Muumin 'Kocha wa Dunia' aliiambia MICHARAZO jana kuwa wimbo unaokamilisha albamu umetungwa na muimbaji wao Januari Mavoko haujapewa jina na unaendelea kufanyiwa mazoezi.
Muumin alisema wimbo huo utarekodiwa siku chache zijazo ili kukamilisha jumla ya nyimbo sita na sebene moja kama bonasi kwa mashabiki zitakazokuwa katika albamu ya kwanza.
"Victoria Sound tunaendelea kuufanyia mazoezi wimbo mpya unaokamilisha albamu yetu uliotungwa na Januari Mavoko, ikiwa ni siku chache tangu tutoke kurekodi wimbo wa 'Maisha' uliotungwa na Atosha One," alisema Muumin.
Alisema kuwa Victoria wameamua kurekodi video ya wimbo mmoja mmoja mpaka wamalize zote saba kabla ya uzinduzi baadaye mwaka huu.
Kwa sasa bendi hiyo imerekodi na 'kushuti' video ya wimbo wa 'Shamba la Bibi' ambao mbali na huo pia wamesharekodi nyimbo za 'Utafiti wa Mapenzi' utunzi wa Muumin, 'Mama Bahati' wa Yohana Mbatizaji na 'Maisha'.

Sunzu, Kazimoto warejesha Msimbazi

Sunzu (kulia)
WAKATI wachezaji Felix Sunzu na Mwinyi Kazimoto wakirejea katika kikosi cha Simba kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam utakaofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kikosi cha timu hiyo kinaingia kambini leo Bamba Beach, Kigamboni.
Sunzu na Kazimoto walitarajiwa jana jioni kuanza mazoezi na wachezaji wenzao kwenye Uwanja wa Kinesi, Sinza jijini na lengo la kuwarejesha baada ya kuomba msamaha ni kukiongezea nguvu kikosi kitakachopambana kuivaa Azam.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, alisema jana kuwa wachezaji wote wataingia kambini leo asubuhi na wanaamini kambi hiyo itawaongezea morali ya kufanya vizuri katika mechi hiyo.
Mtawala alisema kuwa maandalizi  ya mechi hiyo yamekamilika na wachezaji wamepatiwa mahitaji yote muhimu kuelekea mchezo huo muhimu kwa timu yao ambayo imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa.
"Kila kitu kinachotakiwa kuandaliwa kimeshafanyiwa kazi na wachezaji wote wanaingia kambini kesho saa nne asubuhi, tunaamini wakiwa huko watapata utulivu na kumsikiliza mwalimu," alisema Mtawala.
Naye daktari wa Simba, Cosmas Kapinga, alisema jana kuwa beki tegemeo wa timu hiyo, Shomary Kapombe, ameshapona na jana jioni alitarajiwa kuanza mazoezi na wenzake.
Kapinga alisema kwamba vipimo vya mwisho vya uchunguzi alivyofanyiwa juzi Jumatatu vimeonyesha kuwa eneo la mfupa kati ya bega na kifua lililokuwa na maumivu limepona.
Simba itashuka dimbani Jumapili ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Azam walioutapata katika mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Oktoba 27 mwaka jana.
Mabingwa watetezi Simba ni wa nne katika msimamo wa ligi wakiwa na pointi 35 wakati Azam ambao ni wenyeji wa mechi ya Jumapili wako kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi 43 huku Yanga ndiyo vinara kwa pointi 49.

Real Madrid yafuzu nusu fainali kwa kipigo, Dortmund yawafuata

Ronaldo akishangilia bao lake la kwanza usiku wa jana
MABINGWA wa kihistoria wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid usiku wa kuamkia leo imefuzu hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya mwaka huu ikipokea kipigo ugenini cha mabao 3-2 toka kwa Galatasaray ya Uturuki.
Real chini ya kocha wao Jose Mourinho walifanikiwa kufuau hatua hiyo kwa faida ya mabao iliyopata katiika mechi ya nyumbani wiki iliyopita walipoizima Galatasaray kwa mabao 3-0 hivyo kufuzu kwa jumla ya mabao 5-3.
Nyota wa klabu hiyo ya Hispania, Mreno Cristiano Ronaldo ndiye aliyesaidia kuiokoa Real Madrid baa ya kufunga mabao mawili moja kila kipindi na kusaidia kuivusha timu yake hatua hiyo.
Ronaldo alifunga bao la kuongoza dakika saba tu ya mchezo huo uliochezwa Uturuki  na kufanya hadi mapumziko matokeo yawe bao 1-0.
Kipindi cha pili wenyeji waliingia wakiwa wamecharuka na kusawazisha bao kupitia kwa Emmanuel Eboue katika dakika ya 57, kabla Wesley Sneijder hajaongeza bao la pili dakika ya 70.
 
Wesley Sneijder, akishangilia bao lake dhidi ya Real Madrid
Katika dakika ya 72, Didier Drogba aliifungia Galatasaray bao la tatu kabla ya  Ronaldo kufunga  goli la pili la kufutia machozi la Real Madrid dakika ya 90.
Katika pambano jingine la michuano hiyo lililochezwa usiku wa jana nchini Ujerumani wenyeji Borussia Dotmund walifanikiwa kusonga mbele kwenye michuano hiyo baada ya kuwalaza wageni wao mabao 3-2.
Borussia Dortmund wakipongezana kufuzu nusu fainali dhidi ya Malaga

Wageni walionyesha kama wangewaadhiri wenyeji wao baada ya kutangulia kupata bao dakika ya 25 kupitia Joaquin kabba ya Robert Lewandowski kusawazisha dakika tano kabla ya mapumziko.
Eliseu aliiongezea Malaga bao la pili dakika ya 82 na kuwafanya wageni hao kuamini wamemaliza kazi katika pambano hilo kabla ya wenyeji wao kucharuka na kuandika mabao mawili dakika za nyongeza.
Iliwachukua dakika mbili tu za ziada kwa wenyeji hao kujipatia mabao hayo mawili kupitia kwa Marco Reus kumalizia kazi nzuri ya Felipe Santana kabla ya Santana kutupia la pili na kuwavusha mabingwa hao wa Ulaya wa mwaka 1997 kuungana na Real Madrid kucheza hatua ya nusu fainali.