Na Boniface Wambura
KAMATI
ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempiga faini
ya sh. 400,000 na kumfungia mechi sita Kocha wa Rhino Rangers, Renatus
Shija kwa kushiriki vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina na
kumdhihaki mwamuzi kwenye mechi za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Adhabu
hizo zimetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 31(1)(a) na (b) cha Kanuni za
FDL ambapo Kocha huyo aliyeipandisha daraja Rhino Rangers kucheza Ligi
Kuu ya Vodacom (VPL) alifanya vitendo hivyo kwenye mechi mbili tofauti.
Mechi
hizo ni kati ya Kanembwa JKT na Rhino Rangers iliyochezwa Februari 23
mwaka huu Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, na ile kati ya Rhino
Rangers na Morani iliyochezwa Machi 17 mwaka huu Uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora.
Pia
klabu ya Rhino Rangers imepigwa faini ya sh. 200,000 kutokana na Polisi
Wanajeshi- MP kuwapiga walinzi milangoni kwenye mechi hiyo dhidi ya
Kanembwa JKT ili kupisha washabiki wa timu hiyo waingie bure uwanjani.
Mchezaji
wa timu ya Pamba ya Mwanza, Leonard Nahole amepigwa faini ya sh.
200,000 na kufungiwa mechi nne baada ya kumrushia chupa ya maji mwamuzi
kwa madai amependelea kwenye mechi dhidi ya Polisi Tabora iliyochezwa
Machi 16 mwaka huu.
Nao
wachezaji Joseph Mapalala, Yohana Mirobo, Noel Makunja, Mkome Pastory
na Rudenzi Kilinga wa Polisi Mara wamepigwa faini ya sh. 200,000 kila
mmoja na kufungiwa mechi tatu kwa kufanya vitendo vinavyoshiria
ushirikina na kumkimbiza mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Morani
iliyochezwa Machi 9 mwaka huu. Adhabu za wachezaji hao ni kwa mujibu wa
kifungu cha 27(1)(g) cha Kanuni za FDL.
Klabu
ya Villa Squad imepigwa faini ya sh. 150,000 kwa kuchelewa uwanjani
kwenye mechi yake dhidi ya Ashanti United wakati Majimaji imepigwa faini
ya sh. 200,000 kutokana na washabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi
dhidi ya Mbeya City iliyochezwa Uwanja wa Majimaji.
Vilevile
Msimamizi wa Uwanja wa Majimaji aliyetambulika kwa jina moja la Mapunda
aliwatukana waamuzi kwenye mechi hiyo, na suala lake litafikishwa
kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua za kinidhamu.
Pia
uongozi wa Uwanja wa Mafinga unaotumiwa na timu ya daraja la kwanza ya
Kurugenzi umetakiwa kuufanyia marekebisho, vinginevyo hautatumika kwa
mechi za FDL msimu ujao.
MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 11 mwaka huu) litakuwa
na Mkutano na Waandishi wa Habari. Mkutano huo utafanyika saa 5 asubuhi
kwenye ofisi za TFF.
No comments:
Post a Comment