STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, April 10, 2013

Barca, PSG ni kufa ama kupona leo, Juve kuizua Bayern?


Messi alipoichachafya PSG wiki iliyopita


BARCELONA, Hispania
LIONEL Messi ameondolewa kutoka kuwa wa kwanza katika orodha ya nyota wa kikosi cha Barcelona hadi kuwa wa mwisho wakati klabu yake ikilazimika kusubiri taarifa ya mwisho ya daktari kuhusiana na hali yake kabla ya kuteremka dimbani katika mechi yao ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Paris St Germain (PSG) itakayochezwa kwenye Uwanja wa Nou Camp leo.
Mwanasoka huyo bora wa mwaka wa Dunia anaendelea kuuguza jeraha la msuli wa paja alilopata mjini Paris wiki iliyopita, wakati alipofunga katika mechi yao ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya 2-2, ingawa Barca walithibitisha kuwa wanaweza kufanya vizuri pia bila kuwa naye baada ya kuisambaratisha Real Mallorca kwa mabao 5-0 katika mechi yao ya La Liga, Ligi Kuu ya Hispania Jumamosi.
Licha ya kuchezesha kikosi dhaifu, vinara hao wa La Liga walionyesha kiwango cha juu kwenye Uwanja wa Nou Camp kutokana na 'hat-trick' ya Cesc Fabregas na mabao mengine mawili kutoka kwa Alexis Sanchez lakini PSG ni wagumu kulinganisha na 'vibonde' Mallorca wanaokamata mkia kwenye msimamo wa La Liga.
Barca wanaopewa nafasi kubwa ya kusonga mbele wanafukuzia taji lao la nne la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya katika misimu nane na Messi ndiye huwabeba kwa kuwatoka mabeki wa upinzani kwa chenga katika mechi zao kubwa na kuwatengenezea wenzake nafasi za kufunga au kuifanya mwenyewe kazi hiyo ya kupachika mabao.
Ule uwapo wa Messi tu uwanjani huwachanganya wapinzani kisaikolojia, wakiumiza vichwa juu ya namna ya kumdhibiti.
Muargentina huyo alifanya mazoezi mepesi ya viungo Jumapili na vyombo vya habari vya Hispania viliripoti kwamba alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliojitokeza kufanya mazoezi juzi licha ya timu hiyo kuwaruhusu wachezaji wote kupumzika .
Huku wakiwa tayari wamejihakikishia kutwaa ubingwa wa La Liga kutokana na kuongoza kwa tofauti ya pointi 13 dhidi ya mahasimu wao Real Madrid wanaokamata nafasi ya pili wakati kila timu ikiwa imebakiza mechi nane, kocha  Tito Vilanova anaweza kuiongoza timu hiyo leo dhidi ya PSG.
Vilanova pia anatarajiwa kuamua ni nani amchezeshe na Gerard Pique katika sehemu ya ulinzi wa kati baada ya Javier Mascherano kuwa nje kutokana na jeraha na Carles Puyol yuko shakani kucheza baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti.
Beki yosso asiye na uzoefu, Marc Bartra alicheza vizuri na Pique Jumamosi lakini beki kiraka wa pembeni, Adriano Correia anakaribia kuwa 'fiti' na hivyo anaweza kucheza au kupangwa tena kwa kiungo Alex Song katika nafasi hiyo ya beki wa kati.
"Tutaangalia wachezaji gani tulio nao dhidi ya PSG," kocha msaidizi wa Barca, Jordi Roura alisema jana.

SILVA APONA
Beki wa kati aliye tegemeo PSG, Thiago Silva amejumuishwa kikosini kufuatia unafuu alio nao wa jeraha la goti alilolipata katika mechi yao ya kwanza dhidi ya Barca na kukosa mechi ya Jumamosi waliyoshinda 2-0 dhidi ya Rennes kwenye Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa.
Kocha wa PSG, Carlo Ancelotti alikuwa na wachezaji saba wa kikosi cha kwanza ambao aliwaanzisha benchi au kutowajumuisha kabisa katika kikosi kilichochea Jumamosi wakati wakijiandaa kwa mechi ya leo.
Ancelotti, hata hivyo, atakuwa na kazi ya kuziba pengo la kiungo wake 'ngangaro' Blaise Matuidi ambaye ataikosa mechi ya leo kwa sababu ya kutumikia adhabu.
David Beckham anatarajiwa kuanza baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mechi yao ya kwanza, huku viungo wengine wakitarajiwa kuwa kati ya Muitalia Marco Verratti na Mfaransa Clement Chantome.
Kiungo wa kimataifa wa Italia, Thiago Motta anaweza pia kuziba nafasi ya Matuidi lakini hadi sasa amecheza mechi moja tu katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili iliyopita kwa sababu ya jeraha.
Kiwango cha juu alichoonyesha Jeremy Menez dhidi ya Rennes hakitoshi kumfanya apate namba katika kikosi kitakachoanza na kuwaweka kando Ezequiel Lavezzi au Lucas Moura. Beki wa kati, Alex amepona pia jeraha la goti na amejumuishwa kikosini.
"Tunapaswa kuichukulia kuwa ni siku muhimu kwetu. Tuko katika hatua isiyokuwa ya kawaida kwetu," mkurugenzi wa michezo wa PSG, Leonardo aliviambia vyombo vya habari vya Ufaransa.
"Barcelona wako katika mwaka wa 20 wa mradi wa kujenga timu yao. PSG imeanza ukurasa mpya katika historia yao lakini timu yao imeanza kujifua pamoja miezi 20 tu iliyopita."
Mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya leo itakuwa ni kati ya Bayern Munich na Juventus. Katika mechi yao ya kwanza wiki iliyopita, Bayern waliutumia vyema uwanja wao wa nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0. 

Juve maarufu kama kibibi kizee cha Turin watakuwa wakihitaji ushindi mnono ili kuwang'oa mabingwa hao wapya wa Ujerumani ambao msimu huu wameonekana kuwa moto mkali.

No comments:

Post a Comment