STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, October 19, 2013

Yanga watua Dar na matumaini kibao kuinyuka Simba kesho


MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imetua jijini Dar es Salaam leo ikitokea visiwani Pemba ilipoenda kuweka kambi kujiandaa na pambano lao la kesho dhidi ya Simba na kuapa 'mnyama' lazima afe kesho Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na mtandao wa klabu hiyo ya Yanga zinasema kuwa kikosi kamili cha mabingwa hao watetezi kimetua leo kikiwa na matumaini kibao ya kumchinja mnyama kesho katika pambano la kwanza la wapinzani hao wa jadi kwa msimu huu.
Taarifa hiyo inasema Yanga ilijifua asubuhi ya leo kabla ya kurejea jijini ikiwa ni maandalizi ya mwisho mwisho kwa ajili ya pambano hilo na kwamba kocha Ernie Brandts alisema hakuna mchezaji yeyote mgonjwa hali inayompa matumaini ya kucheka kesho.
"Sisi tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo, vijana wangu wapo safi kiafya, kifikra na morali ni ya hali ya juu, hivyo tuna kila sababu ya kuendeleza wimbi la ushindi ukizingatia uwezo wa kikosi chetu kwa ujumla hivi sasa" alinukuliwa Brandts Aidha Brandts alisema anatambua michezo ya watani wa jadi duniani kote huwa ni migumu lakini kwa sasa haoni sababu itakayowazuia kuibuka na ushindi katika mchezo huo japokuwa Simba timu nzuri pia.
Ushindi kwetu siku ya jumapili ni muhimu, ni muhimu kwa sababu tunapigania kutetea tena ubingwa wetu kwa awamu ya pili mfululizo, kikubwa tunawaomba wapenzi, washabiki na wanachama waje kwa wingi kuwashangilia vijana wao watakpokuwa wanapeperusha bendera ya watoto wa Jangwani.

Akina Samatta, Ulimwengu watinga Fainali Afrika

Mbwana Samatta atacheza Fainali ya Kombe la Shirikisho na timu yake ya TP Mazembe

Kikosi cha TP Mazembe kilichotangulia fainali za Kombe la Shirikisho Afrika
WASHAMBULIAJI nyota wa Tanzania, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wameweka rekodi baada ya timu yao ya TP Mazembe ya DR Congo kutinga hatua ya Fainali za Kombe la Washindi Afrika kutokana na ushindi wa bao 1-0 iliyopata jioni hii dhidi ya Stade Malien Bamako mjini Lubumbashi.
Bao pekee lililoipeleka fainali TP Mazembe na kuwafanya watanzania hao kuingia katika rekodi ya kukaribia kuwa Watanzania wa kwanza kunyakua taji kubwa barani Afrika, liliwekwa kimiani na Tresor Mputu kwa njia ya penati katika dakika ya 7 tu ya mchezo huo.
Kwa ushindi hio TP Mazembe imefuzu fainali kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya mechi ya awali iliyochezwa mjini Bamako, Mali kushinda mabao 2-1.
Mabingwa hao wa zamani wa Afrika wanasubiri kujua itacheza na nani katika fainali ya michuano hiyo kati ya timu mbili za Tunisia, CA Bizertin itakayovaana na CSSfaxien kesho katika pambano la marudiano huku matokeo ya mechi ya kwanza yakiwa 0-0.

Kun Aguero aizamisha West Ham, Manchester City ikiua x3

Sergio 'Kun' Aguero

MABAO mawili ya mshambuliaji nyota wa Argentina, Sergio 'Kun' Aguero, yalitosha kuisaidia Manchester City kuizamisha West Ham kwa mabao 3-1 katika pambano lililomalizika hivi punde la Ligi Kuu ya England.
Wakiwa ugenini, Manchester City waliwashtua wenyeji wao kwa kupata bao la kuongoza lililofungwa katika dakika ya 16 kupitia Kun Aguero na kudumu hadi wakati wa mapumziko.
Kipindi cha pili kilishiuhudia  Kun Aguero akiiongezea timu yao bao la pili dakika sita tu tangu kipindi hicho kianze kabla ya wenyeji West Ham kupata bao la kujifutia machozi kupitia kwa Ricardo Vaz Te dakika ya 58.
David Silva aliihakikishia Man City ushindi kwa kufunga bao la tatu dakika 10 kabla ya kumalizika kwa pambano hilo na kuifanya ichupe hadi nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 16 ikiwa nyuma ya timu ya Liverpool na Chelsea waliopo juu yao wakiifukuzia Arsenal inayoongopa baada ya jioni ya leo kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 wakiwa nyumbani Emirates.

Arsenal. Chelsea zaua, Man Utd yabanwa Ozil nouma!

Making the difference: Ozil celebrates doubling Arsenal's advantage
Mesut Ozil ni kama anawauliza mashabiki 'Kuna Maswali...?'
Delight: Dejan Lovren's 89th minute equaliser earned Southampton a valuable point at Old Trafford
Tumnechomoaaaa, Southampton wakishangilia bao lao la kusawazisha dhidi ya Manchester United

Level: Eden Hazard netted the equaliser for the hosts
Eto'o akishangilia bao na wachezaji wenzake wa Chelsea

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester United imeendelea kudorora baada ya leo kubanwa mbavu nyumbani na Southampton, huku Arsenal na Chelsea zikifanya mauaji.
Manchester Utd inayonolewa na David Moyes, ilibanwa mbavu kwenye uwanja wa Old Trafford na kulazimishwa sare ya bao 1-1 na wageni wao waliochomoa bao dakika za lala salama na kuvuna pointi moja muhimu.
Robin van Persie alianza kuwafungia wenyeji bao dakika ya 26, lililodumu kwa hadi wakati wa mapumziko, kabla ya wageni kucharuka na kurejesha bao hilo dakika ya 89 kupitia Dejan Lavren.
Katika mechi nyingine zilizochezwa jioni hii, Arsenal imeendeleza rekodi ya kushinda mwechi mfululizo baada ya kuitafuna Norwich City kwa mabao 4-1 kama ilivyofanya Chelsea iliyoumana na Cardiff City.
Mesut Ozil aliendelea kuonyesha ni 'lulu' Arsenal kwa kufunga mabao mawili, huku magoli mengine yakifungwa na Jack Wilshere na Aaron Ramsey, huku bao la kufutia machozi la wageni kufungwa na Jonathan Howson.
Chelsea iliyokwea hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo kwa ushindi iliyopata nyumbani Stanford Bridge, ilifumania nyavu zake kupitia kwaEden Hazard aliyefunga mawili, Oscar na Mcameroon, Samuel Eto'o.
Mechi nyingine zilishuhudiwa Everton ikipata ushindi wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya Hull City, huku Swansea City 'ikiiua' kwa mabao 4-0 timu ya Sunderland na timu za Stoke City na West  Bromwich zilitoka suluhu ya kutofungana.

Azam, Mbeya City, Mtibwa 'zaua', Ashanti yazidi kujitutumua, Coastal yafa Kaitaba, Luizio, Maguri wampumulia Tambwe

Mbeya City walioendelea kuonyesha maajabu

Azam walioiengua Simba na kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu
Mtibwa waliishusha Yanga ikiendelea 'kuua' VPL
 VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba na watani zao wa jadi Yanga wanaotarajiwa kuvaana kesho, wameporomoshwa katika nafasi walizokuwa wakizishikilia baada ya Azam na Mbeya City kushinda leo.
Azam imekwea hadi katika nafasi ya kwanza na kuitoa Simba baada ya kuinyuka Oljoro JKT kwa bao 1-0 uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Ushindi huo wa ugenini uliopatikana kwa bao la mtokea benchi, Khamisi Mcha 'Vialli' imeifanya Azam kufikisha pointi 20 kutokana na mechi 10 sawa na Mbeya City ambayo ikiwa nyumbani kwao jijini Mbeya ilishinda bao 1-0 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu.
Bao la Jeremiah John lilitosha kuwafanya wageni hao wa Ligi Kuu kuibuka na ushindia huo kwenye uwanja wa Sokoine na kuunga na Azam kileleni.
Timu hizo bado zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, Azam ikiwa na wastani mzuri.
Nao mabingwa wa zamani wa kandanda nchini, Mtibwa Sugar iliendelea kuzifanyia mauaji timu za majeshi baada ya jioni ya leo kuilipua Mgambo JKT kwa mabao 4-1 na kuiengua Yanga katika nafasi ya nne iliyokuwepo.
Mtibwa iliyopata ushindi wake wa tatu mfululizo, imefikisha jumla ya pointi 16 moja zaidi ya Yanga huku ikiwa na hazina kubwa ya magoli.
Magoli ya Mtibwa yalipachikwa wavuni na Nahodha Shaaban Nditti,Juma Luizio aliyefunga mawili na kumpumulia kinara wa mabao Amissi Tambwe wa Simba wakitofautiana kwa bao moja tu sasa. Luizio amefikisha mabao saba sawa na Elias Maguri aliyefunga mabao mawili jioni ya leo kuisaidia Ruvu Shooting kupata sare ya 2-2 dhidi ya Ashanti.
Bao jingine la Mtibwa lilifungwa na Mohammed Mkopi, huku Mgambo inayoburuza mkia kwa sasa ikipata bao la kufutia machozi kwa penati.
Katika mechi nyingine mkwaju wa penati uliopigwa na beki wa pembeni wa Kagera Sugar, Salum Kanoni uliisaidia timu yake kupata ushindi wa baoa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Coastal Union ambayo ilisafiri hadi kwenye uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji wao na kuwatungua bao hilo linaloifanya Kagera kufikisha pointi 14 na kushika nafasi ya saba.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho kwa pambano moja tu la kukata na shoka kati ya Simba itakayoumana na Yanga katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana tambo na ubora wa timu hizo mbili.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu wa kuchezea kichapo katika mechi yao ya mwisho dhidi ya watani wao hao Yanga waliowalaza mabao 2-0 kupitia 'mapro' Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza 'Diego'.

Liverpool chupuchupu kwa Newcastle, Gerrard afunga la 100 EPL

Liverpool striker Daniel Sturridge heads in a goal against Newcastle
Sturridge akisawazisha bao la pili la Liverpool (Picha:BBC Sport)

NEWCASTLE United ikiwa dimba lake la nyumbani ya St Jamed Park ikicheza pungufu ya mchezaji mmoja kwa dakika 50, imeing'ang'ania Liverpool na kulazimisha sare ya mabao 2-2, wageni wakichomoa mara mbili ili kuambulia sare hiyo iliyowapeleka kileleni kwa muda kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England ikifikisha pointi 17, moja zaidi ya Arsenal itakayokuwa nyumbani kuialika Norwich City jioni hii.
Beki Yanga Mbiwa alijikuta akilimwa kadi nyekundu katika dakika ya 40 ya mchezo huo baada ya kumwamgusha Luis Suarez aliyekuwa akienda kumsalimia kipa wake Tim Krul wakati Newcastle ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kosa hilo la Yanga-Mbiwa, lilisababisha Liverpool kupata penati iliyotumbukizwa wavuni katika dakika ya 42 na nahodha Steven Gerrard, likiwa ni bao lake la 100 katika Ligi Kuu ya England.
Kabla ya Gerrard kupata bao hilo la kusawazisha, awali Newcastle ilikuwa mbele kwa bao lililofungwa na Yohan Cabaye katika dakika ya 23 akimalizia kazi nzuri ya Cheikh Tiote.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na wenyeji kujipatia bao la pili dakika ya 57 kupitia Paul Dummett , lakini katika dakika ya 72 mfungaji anayoongoza kwa kufumani nyavu kwa sasa EPL, Daniel Sturridge aliiepushia aibu Liverpool kwa kufunga bao la pili la kusawazisha na matokeo hayo kudumu hadi mwisho wa mchezo.
Hata hivyo Liverpool itakaa kwa muda kileleni kwani mechi mbalimbali zinaendelea kuchezwa jioni hii ambapo tayari Arsena wanaoongoza kwa bao 1-0 dhidi ya wageni wao Norwich, bao likifungwa na Jack Wilshere.

AS Roma yaizima Napoli 2-0

Mfungaji wa mabao yaliyoizamisha Napoli, Miralem Pjanic

KLABU ya AS Roma usiku wa kuamkia leo iliweza kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Italia Seria A baada ya kuwanyuka Napoli kwa mabao 2-0, mjini Roma.
Mabao mawili ya Miralem Pjanic yalitosha kuzima ubabe wa Napoli ambayo ilikuwa haijapoteza mechi yoyote katika ligi hiyo.
Mfungaji huyo alifunga mabao hayo katika dakika za nyongeza kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza na jingine la mkwaju wa penati dakika ya 71 yalifanya Roma kukaa kileleni ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 24, na kuiporomosha Napoli hadi nafasi ya tatu ikiipisha Juventus wanaolingana nao pointi 19 kushika nafasi ya pili.
Juventus leo inatarajiwa kushuka dimbani leo ugenini kuumana na Fiorentina katika mfululizo wa ligi hiyo, ambapo hata kama itapata ushindi bado haijaweza kuwaondoa Roma kileleni.

Simba ina nafasi kubwa kuitungua Yanga kesho, japo...!

Heka heka za Simba na Yanga

INGAWA viongozi na hata wanachama na mashabiki wa Yanga wana imani kubwa kwa timu yao kuibuka na ushindi kesho katika pambano la watani wa jadi linalofanyika kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, bado mabingwa watetezi hao wanapaswa kuwa makini kwani Simba ina nafasi kubwa zaidi ya kuiangusha Yanga.
Yanga wanaamini wana kikosi imara na kinachoweza kuwazima mapema Simba inayonolewa na kocha King Abdallah Kibadeni, lakini kwa mashabiki wa soka wanaofuatilia mechi za watani wa jadi bado Yanga ina kazi kubwa kwa Simba hata kama wanaonekana siyo imara zaidi ya vijana wa Jangwani.
Kama nilivyomnukuu winga wa zamani wa timu ya Yanga na TAMCO-Kibaha aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Wilaya ya Kinondoni (KIFA) Ramadhani Kampira Yanga wasipokuwa makini huenda kesho wakakoga kipigo bila kutarajia na kuleta mtafaruku mkubwa klabuni kwao.
Unajua kwanini?
Rekodi zinaonyesha kuwa wakati Yanga inapokuwa ikonekana kuwa imara na bora ndipo wanapoadhiriwa na Simba, kadhalika Simba inapoonekana kuwa ngangari zaidi huishia kuumia kwa watani zao hao.
Zipo baadhi ya mechi ambazo ukizifuatilia baina ya timu hizo zinaonyesha wakati klabu moja ikiwa juu kisoka na kuundwa na wachezaji wakali ndipo ilipokuwa aikiibishwa na ile iliyoonekana nyonge kuibuka kidedea.
Kwa mfano pambano baina ya timu hizo mwaka Julai 1988, Yanga ikihitaji sare ili kutwaa ubingwa na Simba iliyokuwa chovu ikisaka ushindi ili isihuke daraja, nini kilitokea? Yanga ililala kwa mabao 2-1.
Orodha ya mechi hizo ni ndefu lakini kwa uchache kuanzia miaka ya 1990 mpaka sasa utagundua ukweli huu na kinachosababisha kutokea kwa hali hiyo ni upande unaojiona bora na imara kujiamini kupita kiasi na mwishowe kukumbana na matokeo wasiyotarajiwa uwanjani kitu kinachoweza kuikuta Yanga kesho.
Kwa mfano hivi sasa Yanga inaoonekana kujiamini kupita kiasi hadi kufikia wanachama na wazee wa klabu hiyo kutangaza kwamba wataitungua Simba mabao 3-0, lakini wanasahau kuwa Simba siyo timu ya kubeza na inanolewa na makocha wenye kujua fitina za Simba na Yanga kwa ufasaha zaidi wakiwa wenyewe wameshawahi kucheza mechi za wapinzani hao enzi zao za uchezaji.
Kibadeni na msaidizi wake na hata kocha wa makipa, James Kisaka wanajua 'in and out' ya fitina za mechi za Simba na Yanga kulinganisha na Brandts na wasaidizi wake wengine ukimuondoa Fred Felix Minziro.
Sidhani kama Kibadeni na Julio watapenda kuadhiriwa na Yanga katika mechi ya kesho uwanja wa Taifa, ikizingatiwa kuwa kipigo chochote kwao kitawaondoa kileleni na kuwapisha watani zao kuwatangulia kutegemea na idadi ya mabao watakayofungwa.
Pia, imani yangu makocha hao watawajaza upepo wachezaji wao kupigana kiume ili kumbeba katika pambano hilo na kujihakikishia nafasi katika kikosi mbele ya Kibadeni ambaye huwa haangalii ukubwa wa jina la mchezaji zaidi ya nidhamu, kujituma uwanjani na mazoezini na namna ya kuisaidia timu.
Aina na wastani wa umri wa wachezaji waliopo Simba kulinganisha na Yanga unaweza kubaini kuwa Simba wana nafasi kubwa ya kuwapeleka Yanga mchakamchaka dimbani, iwapo tu wachezaji hao wa Simba watazingatia maelekezo ya walimu wao sambamba na kuonyesha vipaji vyao halisi walivyonavyo.
Kadhalika ipo imani iliyojengeka na kuaminika kwa wengi na hata wana Msimbazi wenyewe kwamba siku ya Jumapili ni SIKU YAO kama ilivyo kwa Yanga wanaoamini mechi ikichezwa JUMAMOSI asimilia zote kushinda ni LAZIMA.
Hata hivyo kwa vile soka halipo hivyo kwa kuangalia imani na historia ni vyema tusubiri tuone hiyo kesho kati ya vijana wa Jangwani na Msimbazi nani watakaolala mapema kwa aibu na wapi watakaokesha kwa furaha kushangilia ushindi?
Chini ni orodha ya mechi za watani hao wa jadi katika michuano ya Ligi tangu mwaka 1965 hadi Mei, 2013
JUNI 7, 1965
Yanga v Sunderland (Simba)
1-0
MFUNGAJI: Mawazo Shomvi dk. 15).

JUNI 3,  1966
Yanga v Sunderland (Simba)
3-2
WAFUNGAJI:
Yanga: Abdulrahman Lukongo dk. 54, Andrew Tematema dk 67, Emmanuel Makaidi dk. 83. Sunderland: Mustafa Choteka dk 24, Haji Lesso dk. 86.

NOVEMBA 26, 1966
Sunderland v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mustafa Choteka dk. 44.

MACHI 30, 1968
Yanga v Sunderland
1-0
MFUNGAJI: Kitwana Manara dk. 28.

JUNI 1, 1968
Yanga v Sunderland
5-0
WAFUNGAJI:
Maulid Dilunga dk. 18 (penalti), Dilunga dk. 43, Salehe Zimbwe dk. 54, Zimbwe dk. 89, Kitwana Manara dk. 86.

MACHI 3, 1969
Yanga v Sunderland
(Yanga ilipewa pointi za chee na ushindi wa mabao 2-0, baada ya Sunderland kugoma kuingia uwanjani).

JUNI 4, 1972
Yanga v Sunderland
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Kitwana Manara dk. 19,
Sunderland: Willy Mwaijibe dk. 11.

JUNI 18, 1972
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Leonard Chitete.

JUNI 23,  1973
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Haidari Abeid 'Muchacho' dk. 68.

AGOSTI 10, 1974
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Gibson Sembuli dk. 87, Sunday Manara dk. 97.
Simba: Adam Sabu dk. 16.
(Mechi ya kihistoria iliyochezwa Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza).

JULAI 19, 1977
Simba v Yanga
6-0
WAFUNGAJI:
Abdallah Kibadeni dk. 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti' dk. 60 na 73, Selemani Sanga alijifunga dk. 20.

OKTOBA 7, 1979
Simba v Yanga
3-1
WAFUNGAJI:
Simba: Nico Njohole dk. 3, Mohammed Bakari 'Tall' dk. 38, Abbas Dilunga dk.72. Yanga: Rashidi Hanzuruni dk. 4.

OKTOBA 4, 1980
Simba v Yanga
3-0
WAFUNGAJI: Abdallah Mwinyimkuu dk. 29, Thuwein Ally dk. 82, Nico Njohole dk. 83.

SEPTEMBA 5, 1981
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Juma Hassan Mkambi dk. 42

APRILI 29, 1982
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Rashid Hanzuruni dk 2.

SEPTEMBA 18, 1982
Yanga 3-0 Simba
WAFUNGAJI:
Omar Hussein dk. 2 na 85, Makumbi Juma dk. 62.

FEBRUARI 10, 1983
Yanga v Simba.
0-0

APRILI 16, 1983
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Charles Mkwasa dk. 21, Makumbi Juma dk. 38, Omar Hussein dk. 84, Simba; Kihwelu Mussa dk. 14.

SEPTEMBA 10, 1983,
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Lila Shomari alijifunga dk. 72, Ahmed Amasha dk. 89.

SEPTEMBA 25, 1983
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Makumbi Juma dk. 75,
Simba: Sunday Juma dk. 72.

MACHI 10, 1984
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 72.
Simba: Idd Pazi kwa penalti dk 20.

JULAI 14, 1984
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 39.
Simba: Zamoyoni Mogella dk. 17

MEI 19, 1985
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Omar Hussein dk. 6
Simba: Mohammed Bob Chopa dk. 30.

AGOSTI 10, 1985
Yanga v Simba
2-0

MACHI 15, 1986
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Abeid Mziba dk. 44
Simba: John Hassan Douglas dk. 20.

AGOSTI 23, 1986
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Edward Chumila dk. 9, Malota Soma dk. 51
Yanga: Omar Hussein dk. 5.

JUNI 27, 1987
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Edgar 'Fongo' Mwafongo dk. 36.

AGOSTI 15, 1987
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Abeid Mziba dk. 14.

APRILI 30, 1988
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Justin Mtekere dk. 28
Simba: Edward Chumila dk. 25.

JULAI 23, 1988
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Edward Chumila 21, John Makelele dk. 58
Yanga: Issa Athumani dk. 36.

JANUARI 28, 1989
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Issa Athumani dk. 4, Abeid Mziba dk. 85
Simba: Malota Soma dk. 30.

MEI 21, 1989
Yanga v Simba
0-0

MEI 26, 1990
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mavumbi Omari dk 6.

OKTOBA 20, 1990
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Makumbi Juma dk 33, Thomas Kipese dk. 82, Sanifu Lazaro dk. 89
Simba: Edward Chumila dk. 58.

MEI 18, 1991
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Said Sued 'Scud' dk.  7.

AGOSTI 31, 1991
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Said Sued Scud.

OKTOBA 9, 1991
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Athumani China dk. 3, Abubakar Salum 'Sure Boy' dk. 54.

NOVEMBA 13, 1991
Yanga v Simba
2-0

APRILI 12, 1992
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Kenneth Mkapa dk. 10.

SEPTEMBA 26, 1992
Simba v Yanga
2-0

OKTOBA 27, 1992
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Damian Morisho Kimti.

MACHI 27, 1993
Yanga v Simba
2-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Said Mwamba Kizota dk. 47 na 57
Simba: Edward Chumila dk. 75.

JULAI 17, 1993
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Dua Said dk. 69.

SEPTEMBA 26, 1993
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Dua Said dk. 13.

NOVEMBA 6, 1993
Simba v Yanga
0-0

FEBRUARI 26, 1994
Yanga v Simba
2-0
MFUNGAJI: Mohammed Hussein 'Mmachinga' na James Tungaraza 'Boli Zozo'.

JULAI 2, 1994
Simba v Yanga
4-1
WAFUNGAJI:
Simba: George Masatu, Athumani China, Madaraka Selemani, Dua Saidi Yanga; Constantine Kimanda.

NOVEMBA 2, 1994
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Madaraka Selemani dk. 71

NOVEMBA 21, 1994
Simba v Yanga
2-0
WAFUNGAJI: George Lucas dk. 18, Madaraka Selemani dk. 42.

MACHI 18, 1995
Simba v Yanga
0-0

OKTOBA 4, 1995
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Said Mwamba 'Kizota' dk. 70, Mchunga Bakari dk. 79,
Yanga: Mohamed Hussein ÔMmachingaŐ dk. 40.

FEBRUARI 25, 1996
Yanga v Simba
2-0

SEPTEMBA 21, 1996
Yanga v Simba
0-0

OKTOBA 23, 1996
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Mohamed Hussein 'Mmachinga' dk. 46

NOVEMBA 9, 1996
Yanga v Simba
4-4
WAFUNGAJI:
Yanga: Edibilly Lunyamila (penalti) dk. 28, Mustafa Hozza alijifunga dk 64, Said Mwamba 'Kizota' dk. 70, Sanifu Lazaro dk. 75.
Simba: Thomas Kipese dk. 7, Ahmed Mwinyimkuu dk. 43, Dua Saidi dk. 60 na 90.
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha)

APRILI 26, 1997
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idelfonce Amlima dk. 16
Simba: Abdallah Msamba sekunde ya. 56

AGOSTI 31, 1997
Yanga v Simba
0-0

OKTOBA 11, 1997
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Sekilojo Chambua dk. 52
Simba: George Masatu dk. 89
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya)

NOVEMBA 8, 1997
Yanga v Simba
1-0
MFUNGAJI: Sekilojo Chambua dk. 85
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma)

FEBRUARI 21, 1998
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Akida Makunda dk. 46
Simba: Athumani Machepe dk. 88

JUNI 7, 1998
Yanga v Simba
1-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idelfonce Amlima dk. 28
Simba: Abuu Juma (penalti) dk. 32

MEI 1, 1999
Yanga v Simba
3-1
WAFUNGAJI:
Yanga: Idd Moshi dk. 59, Kalimangonga Ongala dk. 64, Salvatory Edward dk. 70, Simba: Juma Amir dk. 12.

AGOSTI 29, 1999
Yanga v Simba
2-0
WAFUNGAJI: Bakari Malima dk. 49, Mohamed Hussein 'Mmachinga' dk 71

JUNI 25, 2000
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Steven Mapunda dk. 59 na 72
Yanga: Idd Moshi dk. 4.

AGOSTI 5, 2000
Yanga v Simba
2-0
MFUNGAJI: Iddi Moshi 37 na 47. (Alifunga mabao hayo, akitoka kwenye fungate ya ndoa yake)

SEPTEMBA 1, 2001
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Joseph Kaniki dk. 76

SEPTEMBA 30, 2001
Simba v Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
Simba: Joseph Kaniki dk. 65,
Yanga: Sekilojo Chambua dk. 86
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza)

AGOSTI 18, 2002
Simba v Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
Simba: Madaraka Selemani 65
Yanga: Sekilojo Chambua (penalti). dk. 89

NOVEMBA 10, 2002
Simba v Yanga
0-0

SEPTEMBA 28, 2003

Simba v Yanga
2-2
WAFUNGAJI:
Simba: Emmanuel Gabriel dk. 27 na 36
Yanga: Kudra Omary dk. 42, Heri Morris dk. 55

NOVEMBA 2, 2003
Simba v Yanga
0-0

AGOSTI 7, 2004
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Shaaban Kisiga dk. 64, Ulimboka Mwakingwe dk. 76
Yanga: Pitchou Kongo dk. 48

SEPTEMBA 18, 2004
Simba v Yanga
1-0
MFUNGAJI: Athumani Machuppa dk. 82

APRILI 17,  2005
Simba v Yanga
2-1
WAFUNGAJI:
Simba: Nurdin Msiga dk. 44, Athumani Machupa dk. 64,
Yanga: Aaron Nyanda dk. 39
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)

AGOSTI 21, 2005
Simba v Yanga
2-0
MFUNGAJI: Nico Nyagawa dk. 22 na 56
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha)

MACHI 26, 2006
Simba v Yanga.
0-0

OKTOBA 29, 2006
Simba v Yanga
0-0

JULAI 8, 2007
Simba v Yanga
1-1 (dakika 120)
WAFUNGAJI:
Simba: Moses Odhiambo (penalti dk. 2)
Yanga: Said Maulid (dk. 55).
(Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare hiyo).
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)

OKTOBA 24, 2007:
Simba Vs Yanga
1-0
Mfungaji: Ulimboka Mwakingwe
(Mechi hii ilichezwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro)

APRILI 27, 2008:
Simba Vs Yanga
0-0

OKT 26, 2008
Yanga Vs Simba
1-0
MFUNGAJI: Ben Mwalala dk15.
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)

APRILI  19, 2009
Simba Vs Yanga
2-2
WAFUNGAJI:
SIMBA: Ramadhan Chombo dk 23, Haruna Moshi dk 62
YANGA: Ben Mwalala dk48, Jerry Tegete dk90
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)

OKTOBA 31, 2009
Simba Vs Yanga
1-0
MFUNGAJI: Mussa Hassan Mgosi dk 26
(Mechi hii ilichezwa Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam)

APRILI 18, 2010
Simba Vs Yanga
4-3
WAFUNGAJI:
SIMBA: Uhuru Suleiman dk 3, Mussa Mgosi dk 53 na 74, Hillary Echesa dk 90+
YANGA: Athumani Iddi dk 30, Jerry Tegete dk 69 na 89

OKTOBA 16, 2010:
Yanga Vs Simba
1-0
MFUNGAJI: Jerry Tegete dk 70

MACHI 5, 2011
Simba Vs Yanga
1-1
WAFUNGAJI:
YANGA: Stefano Mwasyika (penalti) dk 59.
SIMBA:  Mussa Mgosi dk 73.

OKTOBA 29, 2011
Yanga 1-0 Simba
MFUNGAJI: Davies Mwape dakika ya 75


MEI 6, 2012
Simba 5-0 Yanga
WAFUNGAJI:
Emmanuel Okwi dk 1 na 65, Patrick Mafisango pen dk 58, Juma Kaseja pen dk 69 na Felix Sunzu pen dk 74.

OKT 3, 2012
Yanga 1-1 Simba
WAFUNGAJI:
SIMBA: Amri Kiemba dk 3,
YANGA: Said Bahanuzi dk 64

MEI 6, 2013
Simba 0-2 Yanga
WAFUNGAJI:  Didier Kavumbagu dk 5 na Hamis Kiiza dk 62

Huyu ndiye Wema Isaac Sepetu 'Beautiful Onyinye'

Wema Sepetu oct 2013 
Swali: Wema ni nani?
Jibu: Wema Sepetu is a girl, i can say a Lady mwenye umri wa miaka 24 kutoka familia ya Isack Abraham Sepetu, a darling, a libra.. a girl who is very ambicious, i love my self…

Swali: Siku yako ya kwanza shuleni ilikuaje?
Wema: Siku ya kwanza tumeenda nikakutana na msichana flani hivi anaitwa Shubira nakumbuka mpaka leo, alikua rafiki yangu wa kwanza tulikutana shuleni nilikua na miaka minne… tumekaa nikaanza kulia kwa sababu ilikua sehemu mpya, mazingira mapya baada ya hapo tukazoea.

Swali:Shule ilikua vipi kipindi unasoma?
Wema: Naweza kusema kipindi ambacho niko shule, Mwalimu wangu sijawahi kukaa hata siku moja kumfikiria mara mbili na haijawahi kutokea kwamba hata mwalimu akaweza kufanya labda matamanio au kutaka kitu chochote, hamna kitu kama hicho

Swali: Utafanya nini ikitokea umerudi shule?
Wema: Ningepata nafasi ya kurudi shule, academic nini uniform na nini… ningejaribu kuifanya more fun, a place where everybody can be just himself or herself and just be Wema Sepetu kwa sababu right now this is my time!!

Swali: Ni nani ambaye uko karibu nae kwenye familia yenu?
Wema: Dada yangu wa kwanza kuzaliwa anaitwa Tunu, tunakwenda sawa kwenye many many ways, kipindi mama yangu alivyonizaa aliumwa akalazwa hivyo dada yangu ndio akawa ananihudumia kama mtoto wake, ananinywesha uji… anahakikisha nimekunywa maziwa on time na mpaka leo ananiita my baby and I call her my mami… mtu wa pili ni dada yangu wa tatu, she is my bestfriend… baba yangu atabaki kuwa baba yangu tu, mama yangu ni my guardian Angel, my heart my darling.
Swali: Ulishawahi kugombana na ndugu zako?
Wema: Yeah nimegombana na dada yangu mpaka sasa hivi hatuongei, sio kitu chepesi….

Swali: Unaamini Mama yako ni mkorofi?
Wema: Linapokuja swala la mama yangu huwezi ukasema kwamba ni mkorofi lakini hapendi nikikosea wala kufanya kitu ambacho sicho…. kutokupenda kwake inafikia point anakua na hasira sana alafu njia ya kuonyesha hasira yake ndio level ya juu, yeye anafikiria kwamba anatengeneza ila badala ya kutengeneza ndio anaharibu.

Wema akiwa na mama yake
Swali: Wema ni mkorofi?
Wema: Mimi sio mkorofi, mtu ambae hanijui ndio ataniita mkorofi ukishanijua yani tutafika mbali lakini usiponijua na hujui ninachonitaka ndio tatizo.

Swali: Unajisikiaje kuwa Wema Sepetu?
Wema: Kuwa Wema Sepetu sio kitu rahisi, haiwezi kuwa kama watu wanavyofikiria  na haitakua hivyo kwa sababu ni maisha ambayo naishi, ni mpaka uone maisha ninayoishi ndio unielewe… yani hata kujaribu kuieleza ili uielewe napata tabu… mashabiki wangu wananielewa sana na uhusiano wangu na wao ni mzuri na ni tofauti na uhusiano kati yangu na familia yangu’

Swali: Unachukulia vipi unaposemwa ama kuandikwa vibaya?
Wema: Katika vitu vyangu ambavyo mtu wa nje anaweza kuviona kama vile… Mungu wangu Wema ana nini, mi navichukulia kama changamoto… mi naona kuna kitu special kuhusu mimi, kwa nini wasiseme watu wengine?

Swali: Unaamini wewe ni mrembo?
Wema: I am beautiful, naamini kwamba mimi ni beautiful kwa sababu nina pure heart… ni kitu Mwenyezi Mungu alichonibariki nacho.


Beautiful Onyinye, Wema Isaac Sepetu, Kuna maswali....?!

Swali: Kitu gani unachojivunia kwamba kinakutofautisha na wasanii wengine?
Wema: Ninachojivunia… uelewa wangu, I am very very smart.. ni mtu ambae ukiniambia kitu, fasta…. na hata kama sijui kitu, kujiua itanichukua muda mfupi, ability kusimama na kuongea na nikasikika, lugha…. hivyo ni vitu ambavyo najivunia sana

Swali: Unavuta sigara?
Wema: Ndio, ninapokua na msongo wa mawazo sana huwa nafanya hivyo  ili kuondoa mawazo na inaweza kutokea mara moja kwa mwezi.

Swali: Ni kweli kwamba wewe ni limbukeni wa umaarufu?
Wema: Sijaacha ustaa uniendeshe, unajua kuna wale watu wanaacha ustaa uwameze mpaka wanabadilisha kuongea, watu wengine wanaacha ule ustaa unawaendesha mwisho wa siku unaanza kuishi maisha ambayo hawana inafika point unaishi kama mtumwa mwisho wa siku unaishi maisha ambayo huna, unaanza kuumia Mungu wangu nimeshazoea kuishi maisha yale,  ishi vile ambavyo unaweza… huna pesa, huna! mimi ni mtu ambae ninaweza kuamka nasikia hamu ya kula mihogo, nafanya kitu ninachopenda na sio anachotaka mwingine’

Swali: Gucci na Vanny ni kina nani kwako?
Wema: My precious, kipenzi changu ni Vanny, katakufanya tu ukapende…. Gucci staa anajifanyaga kama yeye mtu tu wa kuchil!

Swali: Unaamini katika ushirikina?
Wema: Ushirikina najua kwamba upo, uchawi kama uchawi upo worldwide ila sipendi kujishirikisha manake sitaki siku moja kuwa mtumwa, mimi mtoto wa Kiislamu nafanya kisomo nachinja kila baada ya muda so naamini ukifanya hivyo unajikinga na vitu vingi.
Swali: Umeshawahi kurogwa?
Wema: Nimeshawahi kurogwa, imeshawahi kunitokea kabisa yani… ni kitu kingine ambacho huwa sipendi kukizungumzia.

Swali: Ulishawahi kwenda kwa Mganga?
Wema: Siwezi kuficha, wamekuja wengi ambao wanataka kunipeleka wengine mpaka kuniletea Waganga nyumbani kwangu lakini Quran mimi ndio mganga wangu namba moja.

Swali: Unafikiri kuna Wasanii wenzako ambao wanakuchukia?
Wema: Unategemea nini once ukishakua katika spotlight, hautegemei kuwa na watu wazuri karibu yako lazima wengine watakua ni wabaya na sio kila mmoja atakua anakuchekea kwa uzuri, wengine sio kutoka moyoni, wanakuchekea tu kwa sababu hawana choice.

Swali: Nani alikua mpenzi wako wa kwanza?
Wema: Sitaki kumtaja bwana….
wema na Diamond
Swali: Inasemekana unapenda mahusiano ya kimapenzi na watu maarufu?
Wema: Sio kwamba Wema anapenda kuwa na wapenzi maarufu, ni field ambayo tuko, tuko kwenye kiwanda kimoja kwa hiyo kwangu imekua iko hivyo, ni watu ambao mtakua mna interest zinaendana..

Swali: Umeshawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wangapi?
Wema: Wanne, watano au Wanaume sita hehhehe!!

Swali: Mlianza vipi mapenzi na Diamond?
Wema: Tulikua na hii Chemistry inaendana ilikua crazy, baada ya yeye kuniandikia msg kwenye facebook na kuniambia ananipenda, ni mtu ambae nilipata uzoefu mapenzi yanaweza kuwaje, nilipitia kwenye furaha na huzuni nikiwa na yeye…. kilichotokea kimetokea

Swali: Kuna ushindani wowote kati yako na Diamond?
Wema: Once upon a time kulikua na Diamond na Wema, na hawa watu walifall inlove…. watu wanajaribu sana kutulinganisha au tunaonekana tunashindana labda kwa sababu yeye anafanya vizuri kwenye industry yake na mimi nafanya vizuri kwenye industry yangu, mi sijawahi hata siku moja kushindana na Diamond…. mi kuimba siwezi.

Wema na Kajala
Swali: Kajala Masanja ni nani kwako?
Wema: Kajala ni rafiki, dada…. ndugu ambae hayuko kwenye ukoo wa Sepetu lakini uhusiano wangu na wake kwenye urafiki toka mwanzo sidhani kama nimewahi kuwa na uhusiano huu na mtu yeyote, watu wanadhani kwamba nimeanza kumjua juzi… tokea mwaka 2007 mi nimeanza kumfahamu Kajala mpaka tukawa marafiki sana hadi tunajikuta tumevaa sare.

Swali: Wazo la kumtolea Kajala dhamana ya milioni 13 lilitoka wapi?
Wema: Nilimuangalia Kajala analia pale kizimbani, aidha ilipwe faini au aende jela…. kilikua ni kitu ambacho hakijapangwa, ilikua suprise kwetu wote ila nilichokua nataka ni Kajala kuwa huru kwa hiyo kilichoweza kufanyika kilifanyika.

Wema wakati wa kesi yake iliyomalaza mahabusu
Swali: Ulijisikiaje siku tatu ulizolala Mahabusu?
Wema: Haikua nzuri kabisa, ni siku tatu mbaya kwenye maisha yangu… hakuna binadamu ambae hapendi uhuru, kwanini nilimsaidia Kajala na kupata nguvu ya kutoa hizo milioni 13? kwa sababu nimekuepo hapo… mimi siku tatu zilikua balaa sasa mwenzangu mwaka mmoja naa? ingekuaje? hata kama nisingemsaidia Kajala alafu Kajala ndio angekaa miaka hiyo 7 sijui 8 jela mimi nisingeweza kuishi, sio Wema Sepetu alivyo’

Swali: Best Werema ni nani katika kampuni yako?
Wema: Bestizzo ni blogger wangu na mpiga picha wangu, anarun kila kitu kinachohusu kampuni kwenye social network Website nini…

Swali: Kwanini uliamua kufanya nae kazi?
Wema: Kipindi cha kwanza niliona kumpa kazi ingeleta matatizo flani lakini nikafikiria, namjua Bestizzo alikua akifanya kazi kwa Diamond na alikua mfanyakazi mzuri, sijui ni kitu gani kilimfanya aondoke kwa Diamond kwa sababu mimi wakati sikua kwenye uhusiano mzuri na Diamond, Best bado alikua kwa Diamond na kipindi hicho hata bado nilikua sijafungua kampuni, hata alikua haniombi kazi ila alihitaji nimuunganishe na wengine’

Wema akiwa na Kadinda
Swali: Uko vipi na Tinny Dad, Pettman na Martin Kadinda?
Wema: Tiny na Petti ni watu wangu wa karibu sana, nimewajua kwa muda mrefu na wananijua na ninawajua.. Kadinda kabla ya kuwa meneja wangu alikua rafiki yangu, hakua rafiki yangu wa hivyo… tulikua hatuonani hata miezi sita lakini tukikutana namwambia yote yaliyopita, mwaka juzi ndio Martin akasema ngoja niwe Meneja wako, hatukua hata na mikataba mwanzoni… tukajaribisha na tukafanikiwa mpaka leo niko nae.


credit: millardayo

Jambazi la kike lapigwa kichwa kudhibitiwa lisipore fedha


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
JARIBIO la kupora fedha katika kituo cha M-Pesa lililofanywa na Anita Kaburu (27),  pamoja na mwenzake wakitumia bastola na bunduki, lilishindikana baada ya mteja mmoja kumpiga kichwa na kufanikiwa kumdhibiti.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema jana kuwa Anita ambaye ni mkazi wa Usa River wilayani Arumeru, alivamia kituo cha M-Pesa kinachomilikiwa na Stela Mrema akiwa na mwanamume mmoja.

Alisema watu hao wanaodaiwa kuwa ni majambazi, baada ya kufika kwenye kituo cha huduma hiyo maeneo ya Shamsi jijini hapa majira ya saa 6:00 mchana wakijifanya wateja,  ghafla mmoja wao (Anita) alichomoa bastola kwenye mkoba wake na mwenzake akatoa bunduki na kuamrisha wapewe fedha.

“Baada ya kuingia walijifanya kuhitaji huduma ya M-Pesa, ghafla yule mwanamke alitoa bastola kwenye mkoba wake na mwanaume naye alitoa bunduki na kuwaamuru watoe pesa na simu… ndipo yule mteja alimpiga kichwa yule mwanamke na kisha kupiga kelele za kuomba msaada hivyo walifanikiwa kumdhibiti,” alisema.

Hata hivyo, alisema mwenzake alifanikiwa kukimbia. Alisema baada ya polisi kumtaka Anita awataje wenzake, polisi waliwakamata watuhumiwa wanne waliokuwa wamepanga kufanya uporaji huo.

Kamanda Sabas aliwataja waliokamatwa kuwa ni Abdulahman Jumanne Idd (27) ambaye ni mwangalizi wa Kampuni ya Ulinzi ya KK na mkazi wa Shamsi, Simon Martine au Mapanki (45) mkazi wa Kwa Mrombo, Hashimu Ally (30) ambaye ni mpanda milima na mkazi wa Ngarenaro na Charles Luangano (24) ambaye pia ni mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya KK.

Alisema watuhumiwa hao baada ya kufanyiwa upekuzi walikamatwa na bunduki aina ya shotgun, bastola aina ya bereta na risasi sita za bastola. Alisema watafikishwa mahakamani Jumatatu.
CHANZO: NIPASHE

Mdogo wa Super Nyamwela akwaa kashfa nzito


Juma Nyamwela (nyuma) anayedaiwa kulawiti mtoto

MNENGUAJI wa kiume wa Mashujaa Band, Juma Nyamwela (Nyamwela Jr) amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa kiume wa umri wa miaka sita.

Kwa sasa mnenguaji huyo yupo kituo cha polisi cha Mabatini Kijitonyama jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya tatu tangu akamatwe kwa tuhuma hizo.

Habari za uhakika kutoka kituoni hapo zinasema katika maelezo ya awali, mnenguaji huyo amekiri kosa.

Chanzo cha Chetu kimeeleza kuwa huenda mnenguaji huyo akafikishwa mahakamani siku ya Jumatatu.
Nyamwela Jr (wa tatu toka kulia) akiwa na wasanii wenzake wa Mashujaa
 Nyamwela ambaye ni mdogo wake na Super Nyamwela wa Extra Bongo, aliwahi kuitumikia TOT Plus kabla ya kujiunga na Mashujaa Band. 

Mwaka 2007 aliibuka bingwa wa mashindano ya dansa bora wa kiume yaliyoandaliwa na Usher Family na kujinyakulia zawadi ya gari.

Source:- Salute5