Mbeya City walioendelea kuonyesha maajabu |
Azam walioiengua Simba na kukalia kiti cha uongozi wa Ligi Kuu |
Mtibwa waliishusha Yanga ikiendelea 'kuua' VPL |
Azam imekwea hadi katika nafasi ya kwanza na kuitoa Simba baada ya kuinyuka Oljoro JKT kwa bao 1-0 uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Ushindi huo wa ugenini uliopatikana kwa bao la mtokea benchi, Khamisi Mcha 'Vialli' imeifanya Azam kufikisha pointi 20 kutokana na mechi 10 sawa na Mbeya City ambayo ikiwa nyumbani kwao jijini Mbeya ilishinda bao 1-0 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu.
Bao la Jeremiah John lilitosha kuwafanya wageni hao wa Ligi Kuu kuibuka na ushindia huo kwenye uwanja wa Sokoine na kuunga na Azam kileleni.
Timu hizo bado zinatofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, Azam ikiwa na wastani mzuri.
Nao mabingwa wa zamani wa kandanda nchini, Mtibwa Sugar iliendelea kuzifanyia mauaji timu za majeshi baada ya jioni ya leo kuilipua Mgambo JKT kwa mabao 4-1 na kuiengua Yanga katika nafasi ya nne iliyokuwepo.
Mtibwa iliyopata ushindi wake wa tatu mfululizo, imefikisha jumla ya pointi 16 moja zaidi ya Yanga huku ikiwa na hazina kubwa ya magoli.
Magoli ya Mtibwa yalipachikwa wavuni na Nahodha Shaaban Nditti,Juma Luizio aliyefunga mawili na kumpumulia kinara wa mabao Amissi Tambwe wa Simba wakitofautiana kwa bao moja tu sasa. Luizio amefikisha mabao saba sawa na Elias Maguri aliyefunga mabao mawili jioni ya leo kuisaidia Ruvu Shooting kupata sare ya 2-2 dhidi ya Ashanti.
Bao jingine la Mtibwa lilifungwa na Mohammed Mkopi, huku Mgambo inayoburuza mkia kwa sasa ikipata bao la kufutia machozi kwa penati.
Katika mechi nyingine mkwaju wa penati uliopigwa na beki wa pembeni wa Kagera Sugar, Salum Kanoni uliisaidia timu yake kupata ushindi wa baoa 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Coastal Union ambayo ilisafiri hadi kwenye uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji wao na kuwatungua bao hilo linaloifanya Kagera kufikisha pointi 14 na kushika nafasi ya saba.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea kesho kwa pambano moja tu la kukata na shoka kati ya Simba itakayoumana na Yanga katika mechi inayotarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana tambo na ubora wa timu hizo mbili.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu wa kuchezea kichapo katika mechi yao ya mwisho dhidi ya watani wao hao Yanga waliowalaza mabao 2-0 kupitia 'mapro' Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza 'Diego'.
No comments:
Post a Comment