HATMA ya Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Mtemvu kuendelea kutambuliwa kama Mshindi wa Shindano la Urembo la mwaka huu au la inatarajiwa kufahamika kesho.
Sitti alitangazwa mshindi wa Miss Tanzania
2014 wiki iliyopita na kuvishwa taji la mtangulizi wake Happyness Watimanywa, Miss
Tanzania 2013.
Hata hivyo tangu atangazwe mshindi kumekuwa na tuhuma kwamba mrembo huyo ambaye ni mtoto wa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu alidanganya kuhusu umri wake halisi.
Inadaiwa kuwa mrembo huyo ni 'bibi' akiwa na miaka 25 na siyo 23 kama inayosisitizwa na Kamati ya Miss Tanzania ambayo imetuhumiwa 'kumpa' taji Sitti, huku mwenyewe akinukuliwa awali akisema ana miaka 18 tu.
Mpaka kufikia kutwaa taji hilo na kuwa mrembo wa 21 wa shindano hilo tangu liliporejeshwa tena mwaka 1994 na Aina Maeda kukata utepe, Sitti alishinda mataji mawili
likiwemo la Miss Chang'ombe na Miss Temeke yote ya mwaka 2014.
Pia ataiwakilisha Tanzania katika shindano la Miss World 2015.
Warembo 30 waliingia katika kinyang'anyiro cha Miss Tanzania 2014.
Lillian Kamazima alikuwa mshindi wa pili, ambapo Jihhan Dimachk alishika nafasi ya tatu.
Mara baada ya kutwaa taji hilo kumeibuka utata juu ya umri wa Miss Tanzania 2014.
Habari
zimezagaa katika mitandao ya kijamii, ambapo anatuhumiwa kudanganya
umri wake. Kuna taarifa zinasema Bi Sitti alitaja kuwa ana umri wa miaka
18, jambo linalobishaniwa.
Lakini ukweli utajulikana Jumanne
tarehe 21 Oktoba 2014, ambapo waandaji rasmi wa mashindano ya urembo ya
Miss Tanzania, Lino International wameahidi kulitolea ufafanuzi suala
hilo.
Mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga 'Uncle' alinukuliwa na kituo kimoja cha Radio kwamba wao wanajua mrembo huyo ana miaka 23 na siyo 25 inayotajwa, japo alishindwa kubainisha miaka 18 aliyotaja mrembo huyo siku ya fainali hizo.