|
Absalom Kibanda akiwa mahututi baada ya tukiwa na kujeruhiwa kwake |
UTANGULIZI:
Usiku wa Jumanne ya Machi 5 kuamkia Machi 6, 2013,
Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Ltd, ambaye pia Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda alivamiwa na
kujeruhiwa vibaya akiwa nje ya lango la kuingilia nyumbani kwake Mbezi
Juu, Dar es Salaam.
Tukio hilo liliishtua na kutikisa taifa kwa kiwango
kikubwa si tu katika tasnia ya habari nchini, bali pia jamii kwa ujumla
hasa baada ya aina ya utekaji, utesaji na usiri uliotumika katika
kufanikisha uhalifu huu kufanana kwa karibu na tukio lilomkuta
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madkatari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka
lililotokea karibu miezi tisa kabla ya tukio la Kibanda yaani, usiku wa
Juni 26, 2012.
Ukiacha matukio hayo, miezi sita kabla ya Kibanda kutekwa
na kuteswa Mwandishi Daudi Mwangosi, aliuawa akiwa mikononi mwa vyombo
vya dola Septemba 2, 2012 huko Nyololo, Iringa akiwa kazini.
Tukio la
Kibanda limekuwa na sura ya mwendelezo wa mauaji au utesaji wa
wanahabari, hasa ikitiliwa maanani kuwa Mwandishi Issa Ngumba (45) wa
Radio Kwizera aliyekuwa anafanyia kazi zake katika Wilaya ya Kakonko,
Kigoma, Januari mwaka huu, alipigwa risasi na kuuawa katika mazingira ya
kutatanisha.
Kama hiyo haitoshi, tukio la kutekwa na kudhuriwa kwa
Kibanda limetokea mwezi mmoja tu baada ya Mwandishi wa Gazeti la
Tanzania Daima, Shaaban Matutu kupigwa risasi na polisi akiwa nyumbani
kwake Dar es Salaam kwa maelezo kuwa kimakosa polisi walidhani Matutu ni
jambazi.
Mazingira ya kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda yalitia wasiwasi
kuwa upo uwezekano, na dalili zilionyesha kwamba waliofanya kitendo
hicho cha kinyama hawakuwa wezi wala majambazi kutokana na ukweli kwamba
licha ya kuwa na fedha zipatazo shilingi milioni tatu taslimu ndani ya
gari, laptop, simu tatu za gharama (ipad, iphone na Blackberry),
watekaji hawa hawakuchukua chochote baada ya kukamilisha uhalifu
wao.
Kibanda aliumizwa kwa kiwango kikubwa. Alitobolewa jicho la kushoto,
akaumizwa vibaya kichwani kiasi cha kusababisha kuvunjika kwa baadhi ya
mifupa ya kichwa. Aling’olewa meno mawili na kucha mbili, tena bila
gazi.
Watekaji hawa, katika unyama wa ajabu kabisa, walimkata pingiri ya
kidole cha pete chini ya kucha na kuondokana nayo.
Hali hiyo iliibua
maswali mengi, watu wengi wakajiuliza na kutafuta sababu za kutekwa na
kuumizwa kwa Kibanda kiasi hiki.
Kutokana na kuwapo kwa maelezo mengi
yanayotofautiana kuhusu tukio hilo, ikabidi Jukwaa la Wahariri Tanzania
lifanye uamuzi.Katika kikao cha Machi 8, 2013 Jukwaa la Wahariri
Tanzania liliunda TIMU ya watu watano na kuipa hadidu rejea za kufanya
uchunguzi wa kihabari juu ya shambulio hilo kubaini limetokana na
nini.
Timu hiyo iliundwa kufuatia uamuzi wa Jukwaa la Wahariri kufanya
uchunguzi huo na baada ya kukubalika kwa ombi la ruzuku ya kufanya
uchunguzi huo wa kihabari kutoka Mfuko wa Vyombo Vya Habari Tanzania
(TMF).
Ruzuku ya TMF ililenga kiujumla kutumia tukio la Kibanda kuwa
chanzo cha kutengeneza mazingira salama zaidi kwa waandishi na wahariri
na kwamba kiwango cha matukio ya kuteswa, kupigwa na kuuawa kwa
waandishi yanapungua kila mwaka.
Timu hii imefanya kazi usiku na mchana
kwa kwa zaidi ya
mwezi. Timu imezungumza na wadau 26. Kati ya hawa yumo
Kibanda mwenyewe, mke wake, ndugu zake, wasaidizi wake, waajiri wake wa
zamani na wa sasa, viongozi wa kisiasa na vyombo vya dola kutafuta
ukweli wa jambo hili.
Pia tumesoma matamko na habari zilizochapishwa
kwenye mitandao ya kijamii na magazeti ya kati ya Machi 5, 2012 na
Aprili 5, 2012 kwa nia ya kufanya ulinganishi wa taarifa tulizozipata
kutokana na uchunguzi na habari zilizochapishwa baada ya kutekwa
kwake.
Vyombo vya dola akiwamo Waziri mwenye dhamana walikataa kuhojiwa
wakisema kuna tume ya serikali inayofanya kazi hiyo na kwamba kuhojiwa
kungeonyesha kutokuwa na imani na tume hiyo.
Leo tunawasilisha muhtasari
wa ripoti hii. Ripoti kubwa pamoja na viambatanisho vyake, itachapishwa
na kuwekwa katika kitabu kimoja.
Utaratibu mwingine wa kuchapisha habari
ambazo hazijachapishwa kuhusiana na tukio hili (untold stories) pia
utaandaliwa kwa ushirikiano na Jukwaa la Wahariri kwa nia ya kuieleza
jamii maajabu juu ya kadhia hii.Tulipewa Hadidu Rejea ziafuatazo:
HADIDU REJEA:
1. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la
kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama
kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya
mashambulizi dhidi yake.
2. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa
kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5,
2013.
3. Kuangalia mazingira ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari
(2006), Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa kumulika sababu za kuhama kwake
kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka jana na kuhamia New Habari.
4.
Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za
kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.5. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi
kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile
kitakachobainika
YALIYOJIRI KATIKA
UCHUNGUZI:
1.0. Kuchunguza mazingira ya kabla na baada ya tukio la
kushambuliwa kwake. Kabla ya kushambuliwa kwa maana ya kufahamu kama
kulikuwa na viashiria vyovyote vinavyoelekea kuwapo kwa mipango ya
mashambulizi dhidi yake.
Timu ya uchunguzi ilitumia muda mwingi katika
eneo hili, kubaini iwapo kulikuwapo viashiria, sababu au matukio ya wazi
yenye mwelekeo wa kujitokeza kwa shambulio hili. Tuliangalia pia iwapo
wapo watu au makundi yaliyokwishapata kuonyesha ishara kwa matendo au
kwa kauli juu ya uwapo wa nia hii.
Uchunguzi umebaini kuwa kuliwapo
viashiria vingi, isipokuwa Kibanda au watu wake wa karibu hawakupata
kufikiri kuwa huenda vingeweza kuleta madhara makubwa kiasi hiki kama
ifuatayo:-
1.1. Wiki tatu kabla ya Kibanda
kuvamiwa, kutekwa na kuumizwa, gari la polisi aina ya gofu Na PT 180
liliwafuatilia kwa muda mrefu Absalom Kibanda na Ofisa Mtendaji Mkuu wa
New Habari (2006) Ltd, Hussein Bashe likiwa limeegeshwa nje ya ofisi zao
Sinza Kijiweni na baadaye likawafuatilia hadi Sinza Makaburini, ambapo
walisimamisha magari yao na kuzungumza na polisi hao waliosema walikuwa
wanatilia shaka magari yao. Baada ya kuzungumza kwa muda polisi
waliondoka.
1.2. Usiku wa Februari 25, mwaka huu majira
ya saa 09:00 usiku, Kibanda walivamiwa na watu walioingia kwenye uzio wa
nyumba yao wakavunja kioo cha gari analotumia, lakini kioo kilipovunjwa
‘alarm’ ilipiga kelele, Kibanda akatoka nje na watu hao wakakimbia.
1.3.
Kutokana na uvamizi huo, Kibanda na wapangaji wengine katika nyumba
zilizopo kwenye uzio mmoja, waliona hatari ya kuvamiwa hivyo wakaanza
mazungumzo na kampuni ya Ulinzi ya Kiwango, iliyowataka kufunga kamera
za usalama na kuweka walinzi watano. Hadi Kibanda anatekwa, walikuwa
hawajahitimisha mazungumzo na kampuni hii ya Kiwango.
1.4. Kuna
askari anayefanya kazi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) miezi minane
kabla alipata kumpa Kibanda taarifa za kinteligensia, kuwa kulikuwapo
mpango wa kumteka na kumuumiza.
Taarifa kama hizo pia alipewa na
wasamaria wanaofanya kazi katika Jeshi la Polisi. Kwa maneno yake
Kibanda alisema:
“Kuna rafiki yangu askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), kama miezi minane au tisa hivi aliwahi kuniambia ‘unaandika sana
usidhani kama watu wanakupenda. Chukua tahadhari hasa unapofika getini
nyumbani kwako’.
Tangu wakati huo nimekuwa nikichukua tahadhari
sana.“Wiki mbili kabla ya tukio, niliwahi kuhisi kitu kama hicho [cha
kuvamiwa] nikiwa getini. Nilipiga honi wakachelewa kuja kunifungulia,
niliogopa sana. Hata nilipoingia ndani nilikuwa nimekosa raha
kabisa.“Pia kuna rafiki zangu polisi waliwahi kuniambia kwamba
ninatafutwa na kwamba watu wananifuatilia na ikibidi wanitengenezee
ajali au kunifanyia kama Ulimboka au Kubenea.”
1.5. Ndani ya
miezi mitatu mbele ya mlango wa ofisi yake Kibanda (Free Media Limited)
ilikuwa mara kwa mara muda wa asubuhi anapofika ofisini anakuta damu.
Haikufahamika kama damu hiyo ilikuwa ni ya binadamu, kuku, ng’ombe,
kunguru au mbuzi, bali waliipuuza wakidhani ni masuala ya ushirikina.
Mhariri Mtendaji wa sasa, Ansbert Ngurumo, amethibitisha kuwapo kwa
tukio hilo.1.6. Mfanyakazi mwandamizi wa Kampuni ya New Habari
anakofanya kazi sasa Kibanda ndani ya wiki mbili kabla ya kutekwa na
kuumizwa kwake alipata kumwabia Kibanda maneno mazito mara tatu, na hapa
tunamnukuhu Kibanda:
“Aliniambia Danny Mwakiteleko [aliyekuwa Naibu
Mhariri Mtendaji wa New Habari] hakufa kwa ajali, bali alikufa kutokana
na blood clotting (kuganda kwa damu). Hivyo ikitokea mtu ukapata ajali
au ukapigwa na kuumizwa sana sehemu za kichwa hivi au tumbo, ni lazima
madaktari wadhibiti sana blood clotting.
“Na kweli, nilivyoletwa hapa
Milpark hospitalini, madaktari walikuwa wananidunga sindano sita kila
siku kwenye kitovu kuzuia blood clotting. .... (jina linahifadhiwa)
aliniambia maneno haya mara tatu, katika mazingira yasiliyotarajiwa na
kwa msisitizo ambao sikujua maana yake. Nasema .... (jina linahifadhiwa)
naye achunguzwe kwa kina. Inawezekana kuna jambo analijua.”
Ofisa huyu,
alipishana dakika chache na Kibanda muda wa kutoka ofisini baada ya
kipindi cha kwanza cha mechi kati ya Real Madrid na Manchester United
kumaliza nusu ya kwanza (half time). Dakika ishirini baadaye Kibanda
alishambuliwa.
2.0. Kuchunguza mazingira ya tukio lenyewe kwa
kujikitika katika mwenendo wake hasa siku nzima ya Jumanne Machi 5,
2013.
2.1. Familia ya Kibanda na Kibanda Mwenyewe hawakuwa na wasiwasi
wowote siku hiyo kwani hawakuwa na hisia wala wazo kuwa ungetokea
uvamizi huo.
2.2. Kibanda alipopiga honi, mlinzi alisogea langoni
kumfungulia. Ghafla akasikia kishindo kikubwa. Akasikia kelele za
Kibanda akiomba msaada. Kijana huyu Baraka Ibrahim mwenye umri wa miaka
27, aliogopa.
Aliogopa kwa mana hakuwa na silaha yoyote mkononi. Hakuwa
na panga, kisu, rungu, wala filimbi. Kwa maneno yake anasema:“Nilivyoona
ningefungua geti hata mimi ningekufa, nilikimbia kuwaamsha majirani.
Sikuwa hata na namba ya simu ya mtu yeyote kati ya mabosi wangu
ninaowalinda.
Nilikuwa mimi tu, imani yangu na Mungu wangu.... kutokana
na maisha naifanya hivyo hivyo tu. Vinginevyo milele nisingefanya kazi
hii ya ulinzi.”Mlinzi huyo alikimbilia kwa majirani katika nyumba
aliyoamini yumo mwanaume, lakini akaanza kumwamsha House Girl, ili house
girl amwamshe baba mwenyenyumba.
Kitendo cha kuamshana na kuwapa
taarifa kilichukua dakika tano hadi saba, na ndani ya muda huo, Mlinzi
anasema watekaji wa Kibanda walifanya unyama na uasi huo na
kuondoka ndani ya muda mfupi kiasi hicho. “Watu hawa wana mafunzo
maalumu,” anahitimisha.
2.3. Mke wake alikwenda kazini asubuhi na
kurejea nyumbani jioni, lakini tofauti na utaratibu wake wa kawaida
ambapo huwa anaangalia televisheni sebuleni hadi Kibanda anaporejea
nyumbani, siku hiyo alikwenda kuangalia televisheni akiwa chumbani na
usingizi ukampitia.
Anasema hakusikia honi wala tukio la Kibanda
kutekwa. “Hii inanitesa sana moyoni. Najiuliza kwa nini siku hiyo tu
sikukaa sebuleni? Kwa nini siku hiyo tu nimelala mapema kabla Baba
Joshua hajarudi (machozi yanamlengalenga). Najiuliza sipati jibu.”
2.4.
Mmoja kati ya wasaidizi wawili wa nyumbani kwa Kibanda, alisikia kelele
za Kibanda akiomba msaada. Alimwamsha mwenzake na kumwambia.
“Nasikia
Baba Joshua anapiga kelele kama amevamiwa hivi.” Mwenzake alimwambia
“Unaota maana kuna kelele za mpira.” Siku hiyo kulikuwa na mechi kati ya
Real Madrid na Manchester United.
Ni kweli zilikuwapo pia kelele za
wanaoshangilia mpira siku hiyo, hivyo Kibanda alipoomba msaada, hata
waliosikia walidhani watu wanashangilia mpira. Binti aliwaamsha Angela
na mwenzake, wakaenda sebuleni, wakakaa na kuchungulia dirishani,
wakaona mwanga wa gari getini, lakini baada ya kutosikia kelele yoyote
wakarejea kulala wakidhani siye.
Lakini binti mmoja alibaki sebuleni.
Baada ya muda jirani mmoja akampigia simu Angela kumweleza kuwa mumewe
ameshambuliwa.
2.5. Kibanda kwa upande wake, anasema alipofika getini,
alipiga honi, ghafla akaona watu wawili wamesimama pembeni mwa gari lake
na mtu wa tatu akiwa kwa mbali. Kisha akasikia kishindo kikubwa,
akidhani wanataka kuiba gari, aliatokea mlango wa abiria na kuanza
kukimbia huku akiita.
“Mama Joshua nisaidieeeeee.”Katika kukimbia,
aliteleza akaanguka. Huku watesaji wake wakisema mara tatu “Afande piga
risasi.”
Kibanda alijaribu kupambana, akashika rungu, akawahoji
amewakosea nini hadi wampige kiasi hicho, lakini hawakumjibu lolote.
Waliendelea kumpiga, hadi akapoteza fahamu. Hakujua jicho limetobolewa
saa ngapi, meno yameng’olewaje na wala pingiri ya kidole chake
imekatawaje. Ifuatayo ni sauti ya Kibanda mwenyewe. Inasikitisha ila
tuwe wavumilivu na tuisikilize.
3.0. Kuangalia mazingira ya kazi
ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd na nje ya kampuni hiyo kwa
kumulika sababu za kuhama kwake kutoka Free Media mwishoni mwa mwaka
jana na kuhamia New Habari.
3.1. Mazingira ya kazi ndani ya New
Habari (2006) Limited na Freemedia Limited, yanaacha maswali kadhaa
yenye kustahili majibu. Kama ilivyoelezwa kwenye Hadidu Rejea Na: 1,
ndani ya kampuni ya New Habari imekuwapo misuguano isiyo na afya kwa
kazi ya Kibanda kama mwandishi na tasnia ya habari kwa ujumla.
3.2.Mazingira
ya kazi ndani ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd ni utata. Uhusiano
katika chumba cha habari si mzuri. Ndani ya kampuni hawaaminiani na
imefikia hatua wanatuhumiana kuwa huenda baadhi ya viongozi ndani ya New
Habari wamehusika kumteka na kumuumiza Kibanda.
Haya yameandikwa ndani
ya mitandao ya kijamii, ikidai kwamba kiongozi mmoja ndani ya kampuni
hiyo alihusika na utekaji wa Kibanda. Mkurugenzi wa Uhariri, Prince
Bagenda anasema waliohusika kusambaza taarifa chafu dhidi ya kiongozi
huyo wa New Habari wanatoka ndani ya kampuni hiyo.
3.3. Timu ya
uchunguzi ilibaini kuwapo mgawanyiko mkubwa ndani ya New Habari (2006)
Ltd kwa kuwapo kundi la ‘Habari Wazawa’ na ‘Habari wa Kuja’. Malalamiko
mengi yanajikita katika msingi kuwa ajira hazitangazwi na watu
wanaajiriwa bila kuzingatia sifa za kitaaluma.
3.4. Kibanda
hakuhama Free Media kwa amani. Uchunguzi unaonyesha kuwa miezi kadhaa
kabla ya kuondoka kwake alianza kupoteza mamlaka. Mwenyekiti wa Kampuni
ya Free Media Ltd, Freeman Mbowe alianza kumsikiliza zaidi msaidizi wake
ambaye alikuwa Naibu Mhariri Mtendaji, Ansbert Ngurumo kuliko yeye
Kibanda.
Kwa maneno yake, anasema:“Nilihofu kuwa Mbowe anaweza
kutugombanisha. Nikaona ni bora niondoke nisije nikagombana na Mbowe au
Ngurumo.”
Anasema alianza kupoteza mamlaka yake na kutoaminika kwa
mwajiri wake baada ya kuandika makala kuhusu Abdulrahman Kinana ambayo
kabla ya kuiandika hakuwa na wazo la kuondoka. Yaliyofuata baada ya
makala hiyo, yalimshukuma aondoke.
4.0. Kuchunguza jambo jingine lolote linaloweza kutoa mwanga wa sababu za kuvamiwa na kupigwa kwa Kibanda.
4.1.
Uchunguzi ulifuatilia masuala mbalimbali ikiwamo miendendo ya watu
waliotajwa kwa njia moja au nyingine kuhusinaa na tukio hili.
Hata
hivyo, karibu watu wote waliohojiwa, akiwamo Kibanda mwenyewe
aliyeumizwa walimtaja kwa kutilia shaka mwenendo wa kijana Joseph
Ludovick. Hofu yao, iliongezwa nguvu na maandishi aliyoyachapisha
Ludovick kwenye mitandano ya kijamii siku ya Machi 6, 2013.
4.2.
Usiku aliotekwa na kuumizwa Kibanda, Ludovick naye alidai kuwa
ametekwa katika eneo la Shekilango na kupelekwa hadi Kigogo. Baada ya
kutekwa aliibiwa kila kitu, ikiwamo begi, laptop, simu mbili, fedha
taslimu Sh 35,000, akavuliwa nguo na kubaki na chupi tu. Pia alieleza
kuwa alitoa taarifa hizo kituo cha polisi Mabibo.
4.3. Maelezo ya
Ludovick yalitiliwa shaka na watu wengi hasa baada ya kuleeza kuwa
watekaji walitumia muda wa saa mbili kumtoa Shekilango hadi Mabibo,
umbali ambao kwa kawaida mwendo wake hauwezi kuzidi dakika 10.
4.4.
Daniel Chongolo aliiambia timu kuwa alfajiri ya Machi 6, siku anayodai
kutekwa Ludovick yeye alimuona eneo la Mabibo wakati anatoka Muhimbili.
Chongolo alikwenda kituo cha polisi Mabibo na kupewa taarifa kuwa
Ludovick alitoa taarifa polisi kuwa alikuwa ametekwa ila akarudishiwa
mali zake zote.
“Alipouliza amefuata nini polisi, akawaambia kama raia
mwema amefika kuandikisha kumbukumbu kwa nia ya kuonyesha kiwango cha
uhalifu kinavyoongezeka nchini,” anasema Chongolo. Timu ya uchunguzi
ilikataliwa kupitia leja ya polisi kama itakavyoelezwa hapa chini.
4.5.
Pia taarifa za uchunguzi wa timu hii zinathibitisha kuwapo kwa utata
juu ya madai ya kuibwa kwa simu za Joseph Ludovick, kwani simu yake ya
tigo (inayodaiwa kuibwa) ilitumika saa 01:21 asubuhi siku ya Machi 6,
2013. Muda huu ofisi za Serikali na Kampuni ya Tigo zilikuwa
hazijafunguliwa
5.0. Kuchunguza mazingira ya sasa ya kazi kwa wanahabari na kupendekeza hatua za kuchukua kutokana na kile kitakachobainika.
5.1.
Uchunguzi umebaini kuwa maisha ya wanahabari yapo hatarini. Hatari hii
inatokana na makundi mengi yenye masilahi kuwaona wanahabari
wanaosimamia ukweli kuwa maadui wa masilahi yao haramu. Kuna hatari
kubwa inayowakabili waandishi wakati nchi inapoelekea kwenye uchaguzi wa
mwaka 2015.
5.2. Uchunguzi umebaini kuwa usiri umepungua katika
vyombo vya habari. Tofauti na zamani ambapo habari nyeti ziliandikwa kwa
kuhifadhi majina ya waandishi wakitumia jina la MWANDISHI WETU. Simu
hizi hata habari za kutisha waandishi wanaweka majina yao na hata
wasipoweka, ndani ya vyumba vya habari vingi waandishi wapo tayari
kutaja nani ameandika habari fulani.
5.3. Usaliti miongoni mwa
waandishi wenyewe ndani ya vyumba vya habari unazidi kuongezeka na
usipodhibitiwa hali itazidi kuwa mbaya zaidi. Mwenyekiti wa MOAT, Dk.
Reginald Mengi anasema: “Hili ni jambo muhimu sana. Tuache usaliti
vinginevyo wengi wataumia.”
5.4. Pia alishauri waandishi wa
habari kurejea katika msingi wa taaluma, ambayo inawataka wao kuwa ndio
wenye kuendesha vyombo vya habari badala ya kutegemea matakwa ya
wamiliki au makundi yenye masilahi binafsi.
6.0. KILICHOBAINIKA:
6.1.
Uchambuzi uliofanywa ni timu hii umebaini kuwa hoja nne zinazungumzwa
kuhusiana na kutekwa na kuumizwa kwa Kibanda.
Hoja hizi ni:-
(i) Kazi
yake ya uandishi wa habari
(ii) Uhusiano wa kisiasa na vyama au wanasiasa
mbalimbali
(iii)Uhusiano wa kijamii ikiwamo mapenzi
(iv) Vitendo vya
rushwa.
6.2. Timu imejiridhisha kutokana na majibu ya wengi kuwa
dhana ya mapenzi na rushwa, havina nafasi yoyote katika tukio hili. Wote
waliohojiwa walieleza pasi na shaka kwamba suala hili la kushambuliwa
na kuumizwa kwa kiwango kikubwa kwa Kibanda, halina uhusiano wowote na
rushwa au mapenzi.
6.3. Kutokana na yaliyotajwa hapo juu kazi
yake na siasa vikiunganishwa vimechangia kwa kiasi kikubwa kuvamiwa kwa
Kibanda. Timu imebaini kuwa kuna kutupiana mpira kati ya vyombo vya dola
na vyama vya siasa. Mchezo huu mchafu unaweza ukawa mwanzo wa kuumizwa
kwa Kibanda na waandishi wengine.
6.4. Baadhi ya waliohojiwa
walidai kuwa utekaji huu umefanywa na vyombo vya dola ukiwa sehemu ya
mpango mkakati wa vyombo hivi kukihusisha Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) na vitendo vya ugaidi.
6.5. Wanayataja matukio ya
Uchaguzi Mdogo wa Igunga, maandamano ya Morogoro na Mkanda anaodaiwa
kurekodiwa Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare kuwa
vililenga kukifanya CHADEMA kichukiwe na Watanzania kwa kukitaja kama
chama cha kigaidi ambacho kinateka watu na kinawaumiza.
6.6.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anadai kwamba mpango kama huo
vyombo vya dola viliutumia kwa NCCR Mageuzi vikakisambaratisha, Chama
cha Wananchi (CUF) kilisingiziwa udini kikapoteza mwelekeo na sasa
vyombo hivyo vililenga kukifanya CHADEMA kionekane cha kigaidi mbele ya
macho ya jamii ndiyo maana imerekodiwa mikanda kwa nia ya kuitumia
kujenga hoja hiyo.
6.7. Wakati Mbowe akisema hayo, baadhi ya watu
waliohojiwa wanadai kuwa CHADEMA kimepewa mafunzo na ushauri kutoka nje
ya nchi kuwa kikitumia baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wasiokuwa
waaminifu kuteka, kuumiza na hata kuua baadhi ya watu maarufu nchini
wakiwamo waandishi na wanasiasa, basi wananchi wataamini kuwa Chama Cha
Mapinduzi na Serikali yake kimeshindwa uongozi na sasa kimeanza kazi ya
kuua wanaowapinga.
6.8. Kwa njia hiyo, inaelezwa kuwa hesabu za
Chadema ni kuwa wananchi wataichukia CCM na Serikali yake na kukipa
nafasi ya kuingia madarakani. Hapa kauli ya Chadema kuwa NCHI
HAITATAWALIKA itakuwa imetimia.
6.9. Dhana nyingine iliyojitokeza
ni kuwa wapo wafanyabiashara ambao wana vita binafsi, hivyo wanaamua
kuumiza watu wasiowaunga mkono katika mipango yao na hilo ndilo
limemkumba Kibanda, baada ya kuwa ameepusha mauaji ya mwandishi mmoja na
aliyekuwa ameandaa mpango wa kuua mwandishi huyo hakuridhika hivyo
akaamua amshughulikie Kibanda.
7.0. MAPENDEKEZO:
Baada ya Timu kupata taarifa hizi na nyingine nyingi, inapendekeza yafuatayo:-
7.1. Taarifa hii ichukuliwe kama chanzo cha uchunguzi zaidi wa vyombo husika.
7.2. Yanahitajika
marekebisho makubwa na ya haraka katika mifumo ya uendeshaji wa vyumba
vya habari kwa nia ya kurejesha misingi ya uandishi wa habari
inayokubalika.
7.3. Usalama wa wanahabari unapaswa kupewa
kipaumbele na wamiliki, wanahabari wenyewe na jamii kwa ujumla. Hapa
Timu inapendekeza yawepo mafunzo ya kuwawezesha wanahabari kutambua
viashiria vya hatari na kuchukua hatua mara moja.
7.4. Kwa
kiwango alichoumizwa Kibanda iwapo mwajiri wake asingejitolea kugharamia
matibabu, hatujui hatima yake ingekuwaje leo hii.
Tunapendekeza taasisi
na mifuko mbalimbali inayojihusisha na masuala ya wanahabari kama
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) , Baraza la Habari Tanzania (MCT),
Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) na Umoja wa Klabu za Waandishi
wa Habari Tanzania (UTPC) kuanzisha mfuko wa pamoja utakaotumika
kugharamia matibabu ya waandishi watakaoumia wakiwa kazini.
7.5.
Tukio la kutekwa kwa Kibanda limeonyesha mwanga kuwa wahariri
tumegawanyika mno. Habari zilizochapishwa katika magazeti mbalimbali na
mitandao ya kijamii zimeonyesha haja ya kuwafanya wahariri kuwa kitu
kimoja kwa kuondoa tofauti zao zisizo na masilahi kwa tasnia ya habari.
7.6.
Kuna viashiria vingi kuwa kuelekea mwaka 2015 matukio ya waandishi
kuumizwa au kutekwa yanaweza kuongezeka kutokana na wanasiasa na vyama
kuwania madaraka huku wakitumia baadhi ya watumishi katika vyombo vya
dola. Kwa mantiki hiyo, vyombo vya habari na waandishi wa habari
wachukue tahadhari kuanzia sasa.
7.7. Taasisi za habari zifanye
juhudi za makusudi kukutana na vyama viwili vya siasa vya CCM na CHADEMA
haraka iwezekanavyo, kuzungumzia viashiria hivi vya hatari
vinavyoelekea kuvuruga amani ya Tanzania.
8.0. HITIMISHO:
Ni
dhahiri kuwa kupigwa na kuteswa kwa Kibanda kumejiegemeza katika siasa
na kazi yake, hali inayofanya makundi muhimu kuchukua wajibu wa msingi.
Kwa upande wa Serikali ni muhimu kufuatilia viashiria katika taarifa hii
kwa nia ya kupata ukweli zaidi na kuchukua hatua stahiki za kisheria
dhidi ya wahusika.
Na kwa upande wa vyombo vya habari na taasisi za
kihabari zinapaswa kutambua viashiria vinavyohatarisha usalama wa
waandishi wa habari na wahariri na kutengeneza mazingira yatayokuwa
salama zaidi kwa waandishi kufanya kazi zao.
9.0. SHUKRANI:
9.1.
Tunapenda kulishukuru Jukwaa la Wahariri Tanzania, kwa kufanya uamuzi
sahihi wa kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi huu ulioanza kuonyesha
mwanga wa nini kilitokea.
9.2. Tunapenda kulishukuru Baraza la
Habari Tanzania (MCT) kwa kushiriki kikamilifu na kuiwezesha timu hii
kwa Rasilimali Watu na Mali kufanikisha kazi hii.
9.3. Tunapenda
kuwashukuru Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) kwa uwezeshaji wa
ruzuku, uliofanikisha kufanya uchunguzi wa kihabari uliohusisha kwenda
nchini Afrika Kusini kufanya mahojiano na Kibanda. Uwezeshaji huo pia
unahusisha kutengeneza mwongozo kwa waandishi wenye lengo la kuwaepusha
na hatari za kiusalama.
9.4. Tunawashukuru Kibanda, mkewe Angela,
wanafamilia, ndugu na jamaa wa Kibanda na wanahabari wote waliohojiwa
kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa Timu hii.
9.5. Tunawashukuru
wahariri wote kila mtu kwa nafasi yake, kutokana na ushauri wa mara kwa
mara mliotupatia katika kufanikisha uchunguzi huu.
10.0. WAJUMBE
WA TIMU:
Timu hii iliundwa na wajumbe watano ambalo ni:1. Deodatus
Balile – Mwenyekiti
2. Pili Mtambalike – Mjumbe
3. Jane Mihanji – Mjumbe
4.
Tumaini Mwailenge – Mjumbe
5. Rashid Kejo – Katibu
Mwisho
NB:TAARIFA YA UCHUGUZI JUU YA KUTEKWA NA KUUMIZWA KWA ABSALOM KIBANDA IMEWASILISHWA NYUMBANI HOTEL - TANGA MEI 30, 2013