Kikosi cha Simba kinachotarajiwa kushuka dimbani leo |
MABINGWA wa soka nchini, Simba iliyorejea jana kutoka Oman ilipokuwa kwenye kambi ya mazoezi, inatarajiwa kushuka dimbani leo kuonyesha mambo ya umangani itakapovaana na Black Leopards ya Afrika Kusini katika pambano la kirafiki la kimataifa.
Pambao hilo litakalopigwa majira ya jioni kwenye dimba la Taifa, jijini Dar es Salaam itakuwa pambano la mwisho kwa Simba kabla ya kuanza kwa duru la pili la Ligi Kuu Tanzania Bara itakayoanza Jumamosi.
Simba inatarajiwa kuanza duru hilo kwa kuvaana na African Lyon kwenye uwanja wa Taifa.
Black Leopards inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ipo nchini kwa ziara ya kujipima nguvu wakisubiri kuendelea na ligi yao iliyosimama kwa sasa kupisha michuano ya AFCON-2013 inayofanyika nchini mwao.
Timu hiyo jana iliendelea kuwa mnyonge kwa Yanga kwa kulazwa mabao 2-1 ikiwa ni siku chache tangu ichezee kichapo cha kukandikwa mabao 3-2.
Simba iliyoenda moja kwa moja kambini mara baada ya kuwasili jana mchana, imetamba kuwapa raha mashabiki wake ambao walimaliza duru la kwanza la ligi kuu kwa masononeko.
Mabingwa hao hiyo itakuwa mechi yao ya nne ya kujipima nguvu baada ya awali kucheza mechi tatu ughaibuni nchini Oman ikishinda mechi moja na kupoteza mbili.
Mashabiki wa soka wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi katika pambano hilo la leo ili kutaka kushuhudia makali ya timu yao, baada ya watani zao Yanga waliokuwa Uturuki, walivyokonga nyoyo za mashabiki wao kwa kuisasambua Blac Leopards mara mbili.