Ramadhani Kampira, mmoja wa wanachama wa Yanga |
BAADHI ya wanachama wa Yanga wameibuka na kuelezea hofu waliyonayo juu ya kupitishwa kwa vipengele vya katiba inayowapa madaraka makubwa Mwenyekiti na Makamu wake klabu hapo.
Wanachama hao walisema kupitishwa kwa vipengele vinavyowapa viongozi hao uwezo wa kumfuta uanachama mwanachama yeyote wa Yanga ni sawa na kuruhusu udikteta pamoja na kuivuruga Yanga.
Mmoja wa wanachama hao, Ramadhani Kampira, alisema japo wanachama wenzake waliafiki vipengele hivyo katika mkutano mkuu ulioitishwa mwishoni mwa wiki, lakini ukweli hakubaliani navyo.
Kampira aliyewahi kuichezea timu hiyo na kung'ara na TAMCO Kibaha na Sifa United, alisema kuruhusu hali hiyo inaweza kutumiwa vibaya na viongozi katika suala la chuki binafsi.
"Mtu anaweza kuamka usingizi au kutoka nyumbani akiwa kagombana na mkewe kisha kuamua kumfukuzisha mtu uanachama kwa chuki na kusiwepo wa kuwahukumu kwa vile lipo kwenye katiba," alisema Kampira.
Naye Mwinjuma Muumini, ambaaye ni mmoja wa waimbaji nyota wa muziki wa dansi, alisema hakubaliani na maamuzi hayo japo alikiri hajui kitu gani kilichowakumba wanachama wenzake na kuafiki jambo hilo.
Muumini, anayefahamika kama 'Kocha wa Dunia' au 'Mzee wa Chelsea' alisema kuwa maamuzi hayo ni kurejesha ukoloni na kuruhusu udikteta katika Yanga kwani haikubaliki hata kwa sheria ya nchi.
"Sijajua ajenda za mkutano huo zilikuwa zipi, lakini kilichofanywa na wanachama wenzetu ni msiba ambao utakuja kuigharimu na kuivuruga Yanga mbele ya safari, huo ni udikteta,:" alisema.
Juu ya suala la kutimuliwa kwa wanachama wenzao waliokuwa waajiriwa wa klabu hiyo, Louis Sendeu na Celestine Mwesigwa, Kampira yeye alisema taratibu na sheria za kazi zizingatiwe na zisiingizwe katika masuala ya michezo.
"Wale walikuwa waajiriwa na kama walitimuliwa kazi bila kuzingatiwa taratibu au kulipwa haki zao stahiki, walikuwa na haki ya kutafuta jasho lao mahali pengine, hivyo suala hilo lisitumiwe kuwaonea watu waliotendwa sivyo ndivyo,": alisema Kampira.
Wanachama wa Yanga waliafiki kwa kauli moja kuwatimua uanachama akina Sendeu kwa madai ya kosa la kukimbilia mahakamani ya usuluhishi kudai haki zao za malimbikizo na misharaha.
Pia mkutano huo uliafiki kubadilishwa kwa vipengele vya katiba yao kwa kuwaruhusu viongozi hao wa juu kuwatimua wanachama mara watakapobainika kufanya makosa bila kusubiri maamuzi ya wengi.
No comments:
Post a Comment