STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 28, 2014

Moto wazuka na kuua wagonjwa 21

MOTO uliozuka hospitalini wauwa watu 21 nchini Korea Kusini, ikielezwa wagonjwa wapatao 20 pamoja muuguzi wameuawa.
Moto huo mkubwa kuwaka hospitalini katika jimbo la Janseong nchini Korea Kusini, na inaelezwa watu wengine 6 wakiwa hali mahututi baada ya moto huo katika hospitali ya Hyosarang iliyoko kilomita 300 kusini mwa Seoul.
Wengi wa walioaga dunia wanafikiriwa kuwa wazee wenye umri wa kati ya miaka 70 na 80 na wasioweza kutembea.
Maafisa walisema kuwa wengi waliokufa walikosa hewa kutokana na gesi zenye sumu.
Moto huo ulizimwa kwa takribani nusu saa.
Moto huo ulianza muda mfupi tu baada ya saa sita usiku katika hilo jumba lenye orofa tatu.
Vyombo vya habari vinaarifu kuwa wengi wa wagonjwa waliokuwa katika orofa ya juu ya jumba hilo walishindwa kujiokoa kwa sababu vyuba vyao vilikuwa vimejaa moshi uliotokana na moto huo.
Muuguzi huyo aliyekufa alikuwa akijaribu kuzima moto kwa kutumia kizima moto kulingana na shirika la Agence-France Presse.
Ripoti ya shirika la Yonhap ilisema kuwa polisi walisema kuwa jumba hilo lilikuwa limefanyiwa uchunguzi wa kiusalama majuzi.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo Lee Hyung Seok aliomba msamaha na kuwaambia wanahabari kuwa alikuwa ametenda dhambi kubwa, na kuwa hangetoa visababu wakati watu wameaga dunia.
Tukio hili limekuja wakati wananchi wa Korea kusini wakiendelea kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 300 waliofariki katika ajali ya feri iliyotokea mwezi uliopita.
Rais wa taifa hilo Park Geung-Hye ameliomba taifa radhi kirasmi kwa ajali hiyo ya feri, huku akiahidi kuimarisha viwango vya usalama.
Waziri mkuu Chung Hong-won wakati huo alijiuzulu kwa madai ya jinsi serikali ilivyokuwa ikikabiliana na majanga.
Ajali hiyo ya hospitali pia imetokea siku moja tu baada ya watu 7 kuuwawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mkasa wa moto uliozuka katika kituo cha mabasi jijini Goyang.
BBC

Marehemu Recho kuzikwa kesho Dar, soma historia yake fupi

Msanii Rachel Haule 'Recho' enzi za uhai wake
Msanii Recho enzi za uhai wake
Recho akiwa na mchumba wake enzi za uhai wake
STAA wa filamu za The Passion, Vanesa in Dillema, Bed Rest, Unpredictable, Rachel Haule 'Recho' aliyefariki wakati wa kujifungua anatarajiwa kuzikwa siku ya Alhamis kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar badala ya kusafirishwa kwenda kuzikwa kwao mkoani Ruvuma kama ilivyokuwa imeelezwa awali.
Kwa mujibu wa taarifa toka Bongo Movie na kuthibitishwa na Rais wa Umoja huo, Steve Nyerere, marehemu Recho sasa hatasafirishwa kwenda kuzikwa Songea badala yake atazikwa Dar na shughuli za kuagwa zitafanyika viwanja vya Leaders kabla ya kuzikwa Kinondoni yeye na kichanga chake na msiba hupo nyumbani kwa marehemu Sinza Palestina.
"Tymekubaliana marehemu azikwe Dar na shughuli nzima za kuaga miili ya marehemu itafanyika viwanja vya Leaders kuanzi  saa 4 asubuhu kabla ya saa nane kwenda kuzikwa makaburi ya Kinondoni, " Steve Nyerere alisema hivi punde alipozungumza na MICHARAZO.
Recho alifariki asubuhi ya jana muda mchache baada ya kujifungua kwa njia ya upasuaji ambapo kichanga chake nacho kilipoteza maisha, ameondoka wakati Bongo Movie ikiwa bado hawajasahau machungu ya kuondokewa na muigizaji na muongozaji mahiri, Adam Kuambiana aliyefariki wiki iliyopita.
Enzi za uhai wake Recho aliwahi kufanya mazungumzo na MICHARAZO MITUPU na kuweka bayana historia ya maisha yake namna alipojikuta akiingia kwenye fani hiyo aliyoipenda tangu akiwa mdogo.
Mwenyewe alisema alianza kuonyesha kipaji cha sanaa tangu akiwa Shule ya Msingi Ndugumbi, lakini hakuweza kupata nafasi ya kutambulika hadi miaka miwili iliyopita alipoibuliwa na filamu iitwayo 'The Passion'.
Filamu hiyo ilimsaidia mwanadada huyo kuweza kufahamika na kupata tenda ya kucheza kazi nyingine zilizosaidia kumtangaza vema na kumuinua kimaisha.
Recho, alisema kabla ya kutoka na filamu hiyo aliwahi kujiunga na kundi la sanaa la  Lumila Arts na alivutiwa kisanii na waigizaji Blandina Chagula 'Johari' na Genevieve Nnaji wa Nigeria.
Mwanadada huyo aliyeuza sura katika kazi nyingine kama Candy, Life to Life, Rude, Mtihani, Time After Time, Confussion, Mwalimu Nyerere na Mke Mwema, alisema anashukuru fani hiyo ilimsaidia kwa mambo mengi kimaisha.
MOja ya aliyokuwa akijivunia ni kuweza kufahamika na kujiingizia kipato cha kila siku, akiweza pia kufungua maduka matatu katika mikoa mitatu.
Aliyataja maduka yake hayo yanayohusika na kuuza DVD na nguo za wanawake na watoto yapo Arusha, Songea na Dodoma.
Recho aliyekuwa akipenda kula ugali kwa dagaa na wali kwa maharage na kunywa kinywaji cha Savanah, alisema fani ya filamu kwa sasa inalipa na kuwataka wasanii wenzake kuchapa kazi na kuepukana mifarakano pamoja na kujihusisha na matendo yanayowachafua mbele ya jamii.
Msanii huyo aliyekuwa na ndoto za kutamba kimataifa na kupanua miradi yake ya biashara, alisema hakuna tukio la furaha kwake kama alipoanza kuuza sura katika filamu na kusikitishwa na kifo cha mama yake mdogo aliyemlea tangu akiwa mdogo.
Nyota huyo aliyekuwa hajaolewa ingawa alikuwa mchumba wa George Segunda, alidai angetamani sana kama angekuja kuzaa watoto wasiozidi watatu, ingawa bahati haikuwa yake kwa kupoteza uhai akitekeleza 'sunna' hiyo ya kuiongeza dunia.
Kihistoria, Rachel Haule alizaliwa Aprili 4, 1988 mjini Songea akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto watano wa familia yao. Alisoma Shule ya Msingi Ndugumbi kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya bweni iitwao Hanga Montesory ya mjini Songea.
Mara alipohitimu masomo yake ya sekondari alijiunga na Chuo cha Uhazili cha Magogoni kusomea Ukatibu Mhutasi kabla ya kutumbukia kwenye masuala ya sanaa ya uigizaji aliyoendelea kuifanya mpaka mauti yalipomkuta.
Kwa hakika kifo kinauma, kifo kinaumiza...tulimpenda sana marehemu Recho, lakini aliyemuumba alipenda zaidi tunamuombea kwa Mungu roho yake iwekwe mahali pema yeye katangulia sisi tu nyuma yake.