|
Man Bizo akiwa kwenye kiti chake cha magurudu |
|
Man Bizo akiwa na 'swahiba' zake, Mama Shotii na Kazi |
KWA mashabiki wa filamu hasa za vichekesho ama wafuatiliaji wa kipindi cha 'vituko show', jina la Man Bizo huenda sio geni masikioni mwao kwa jinsi wanavyosuuzwa roho na umahiri wa msanii huyo mwenye ulemavu.
Man Bizo ambaye majina yake kamili ni Ally Boffu, amejizolea umaarufu mkubwa kwa namna ya uigizaji wake na umbile lake analolitumia vema katika kazi mbalimbali alizoshiriki pamoja na wasanii wenzake.
Msanii huyo amekuwa akikitendea haki kipaji chake cha sanaa sambamba na kile alichodai kutaka kuwaonyesha mfano walemavu wengine kwamba hali walizonazo sio mwisho wa kila kitu katika maisha yao.
Anasema walemavu wakiamua, kuthubutu na kujituma kama anavyofanya yeye ni wazi wanaweza kufika mbali kimaisha na kuepuka utegemezi.
Man Bizo anasema kama asingezingatia mambo hayo huenda kipaji chake kingepotea hivi hivi.
"Kujiamini, kuthubutu na kutaka kuonyesha mfano kwa wengine, ndiko kulikonifikisha hapa," anasema.
Anasema licha ya kukutana na changamoto nyingi, hajakata tamaa kwa vile anatamani kufika mbele zaidi katika fani hiyo na kubwa kuja kuanzisha asasi ya kuwasaidia walemavu wenzake.
Man Bizo anayefahamika pia kama Kapeto, Jini Mahaba na Kipwinto, anasema tangu utotoni na hata alipokuwa shuleni alipenda kuchekesha watu, lakini hakuota kuja kuwa muigizaji nyota.
"Sikuota kuja kuwa muigizaji mkali kwa mazingira niliyokulia, ila kuvutiwa na msanii aitwae Zimwi na kujiamini kulinifanya nijitose rasmi mwaka 2007 na ninashukuru yapo mafanikio ya kujivunia" anasema.
Anasema licha ya umaarufu, sanaa pia imemwezesha apate ajira katika kampuni ya Al Riyamy na kumiliki maktaba ya kuuzia na kukodia kanda za filamu (video library) inayomuingizia pato la ziada.
"Nashukuru Mungu tangu nijitose kwenye sanaa, nimepata umaarufu, kupata ajira na kumiliki 'video library' na nina kila kitu katika nyumba yangu," anasema.
MUZIKI
Man Bizo anayependa kula ugali kwa mboga za majani na kunywa kinywa juisi, ni mshabiki wa klabu ya Simba akiwazimia manahodha, Juma Kaseja na Haruna Moshi 'Boban'.
"Huniambii kitu kwa Simba, naipenda mno klabu hii na navutiwa na Kaseja na Boban, ila kimataifa mie ni mnazi wa Manchester United," anasema.
Msanii huyo anasema mbali na uigizaji, pia ni mahiri katika muziki akiwa mbioni kwa sasa kupakua albamu akitanguliza kwanza nyimbo tatu mpya.
Anasema nyimbo hizo tatu ameziimba akishirikiana na wasanii wakali kama Karapina, Dully Sykes na Prince Amigo na kudai kuwa kujitosa kwake kwenye fani hiyosio kwa kubahatisha bali ni kipaji alichonacho.
"Nilipokuwa nasoma Shule ya Jeshi la Wokovu, nilikuwa naimba hivyo kuibukia kwangu kwenye muziki sio kwa kubahatisha ila najua ninachokifanya," anasema.
Muigizaji huyo mwenye matumaini ya kuja kutamba zaidi ndani na nje ya nchi katika fani zote za muziki na uigizaji, anasema hakuna tukio la furaha kwake kama siku alipokabidhiwa nyumba ya urithi wa baba yake.
MTOTO
Man Bizo anasema hakuna tukio la huzuni linalomuuma mpaka leo kama lile la kukataliwa na kunyang'anywa mtoto kwa kile alichodai hali yake ya ulemavu.
Anasimuliwa kuwa, alikuwa na mahusiano na msichana mmoja aliyekataa kumtaja jina la kumpa ujauzito aliokuja kujifungua mwaka 2009 mtoto wa kike ambaye alimtaja kwa jina la Lilian, ambaye ana umri wa miaka mitatu kwa sasa.
Anasema hata hivyo familia ya msichana huyo ilionyeshwa kuchukizwa na kitendo cha msichana huyo kuzaa naye na hivyo kumkana na kumnyima mtoto huyo anayedai anampenda kupita maelezo.
Hata hivyo Man Bizo anasema kwa sasa familia hiyo imemkubali kwa shingo upande na mama watoto wake wamekuwa wakimpeleka mwanae kwake kumuona, kitu kinachomfariji ingawa bado hajasahau tukio alilofanyiwa siku za nyuma.
"Lilian ni mwanangu na ninampenda mno, kwa sasa mie najipanga kufunga ndoa ili niweze kumtunza vema," anasema.
Akaongeza kuwa, suala la unyanyapaa dhidi ya walemavu ndani ya jamii ni kitu kinachokatisha tamaa na kuonyesha namna gani baadhi ya watu wanashindwa kuitambua uwepo wa Mungu na fani yake ya uumbaji.
"Nadhani jamii inapaswa kubadilika na kuwaona walemavu kama watu wengine licha ya kasoro za maumbile," anasema.
MAN BIZO
Ally Boffu 'Man Bizo' alizaliwa Julai 7, 1984 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto wa nne wa familia yao na Elimu ya Msingi aliisoma katika Shule ya Jeshi la Wokovu alipohitimu darasa la saba.
Alijitosa kwenye sanaa mwaka 2007 katika kundi la MCAP, na filamu yake ya kwanza ikiwa ni 'Olopong', kabla ya kushiriki 'Kiroba' na 'Vyumba Vimejaa' anayodai ndiyo iliyomtangaza zaidi na kumpa nafasi ya kucheza filamu nyingine zinazokaribia 50.
Baadhi ya kazi aliocheza msanii huyo anayeiomba serikali kuisaidia fani ya sanaa nchini kutoa tija kwa wasanii na kuondoka na unyonyaji wanaofanyiwa na baadhi ya watu wachache ni pamoja na 'Kitimtim', 'Hekaheka', 'Mishemishe', 'Kichefuchefu', 'Jazba' na 'Koziman'.
Man Bizo, anayewashukuru bosi wake, Khalfan Abdallah, Madhila Piana na wasanii wenzake wote anasema kubahatika kuigiza na wasanii wakubwa na wenye majina kama King Majuto, Kitale, Mzee Jangala, Sharo Milionea na wengine kwake ni fahari kubwa.
Juu ya ugonjwa wa Ukimwi, Man Bizo anasema kila mtu ndani ya jamii anapaswa kupambana nao kwa sababu umekuwa na madhara na kukatisha ndoto za watu wengi.
Msanii huyo anasema kitu cha muhimu watu ni kuwa waaminifu katika ndoa zao, kumcha Mungu na kuepuka anasa zinazoweza kuywapelekea kuangukia katika mapenzi yasiyo salama.
|
Man Bizo (aliyekaa kulia) akiwa na wasanii wenzake wa 'Vituko Show' |
|
Man Bizo (kulia) akiwa na 'swahiba' yake Seleman Kazi |