STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Saturday, December 1, 2012

Sare tu kuivusha Kilimanjaro Stars ribi fainali

Kikosi cha Kilimanjaro Stars


Na Somoe Ng'itu, Kampala

Kilimanjaro Stars leo inahitaji angalau sare dhidi ya Somalia katika mchezo wa mwisho wa Kundi B la Kombe la Chalenji mjini hapa ili kukata tiketi ya kucheza robo-fainali.
Endapo itapata sare, Stars yenye pointi tatu sawa na Sudan katika kundi hilo inaweza kufuzu kama moja ya 'best liza' wawili katika mchezo utakaoanzia saa 8:00 kwenye Uwanja wa Lugogo jijini hapa, baada ya ushindi wa Kenya dhidi ya Somalia jana kumaanisha mshindi wa tatu wa Kundi A ana pointi tatu tu.
Kocha Mkuu wa Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen, alisema jana kuwa ameiona Somalia katika mechi zake mbili zilizopita hivyo hatawadharau kwa sababu ni timu inayoimarika kadri inavyocheza mechi.
Poulsen alisema amejipanga kupata ushindi, hata hivyo, ili kujiweka kwenye nafasi nzuri katika kundi hilo baada ya kupoteza mechi yake ya pili dhidi ya Burundi iliyofanyika Jumatano kwenye uwanja wa Namboole ambao ulijaa maji na matope kufuatia mvua zinazonyesha mfululizo jijini  hapa.
"Wapinzani wetu wanaimarika kila siku zinavyokwenda, tutaingia uwanjani ili kusaka ushindi na si kuwadharau," alisema kwa sababu "timu zote zimekuja kupambana na ndio maana hakuna anayekata tamaa hata  kama amefungwa mechi zote."
Poulsen alisema hali ya beki wake, Shomary Kapombe na kiungo, Mwinyi Kazimoto zinaendelea vyema na watakuwepo kwenye kikosi kitakachoshuka dimbani kuivaa Somalia.
Naye Kocha Mkuu wa Somalia, Sam Ssimbwa, aliliambia gazeti hili juzi kwamba wamekuja Kampala kupambana ingawa wachezaji wake hawana uzoefu wa mechi za kimataifa ukilinganisha na wapinzani wao.
Ssimbwa ambaye alikuwa akiifundisha Sofapaka ya Kenya alisema hana majeruhi kwenye timu yake na amejiandaa kucheza kwenye hali yoyote kwa sababu mazingira ya viwanja vya Afrika yanajulikana.
Mbali na mechi hiyo, leo pia saa nane mchana Burundi na Sudan zilizoko kundi B zitashuka kwenye uwanja wa Wankulukuku na baadaye Malawi itakutana na Zanzibar wakati Rwanda itaikaribisha Eritrea kuanzia saa 10:00 jioni kwenye uwanja huo.
Mabingwa watetezi na wenyeji Uganda Cranes, Zanzibar na Burundi tayari wameshakata tiketi ya kucheza robo fainali ya mashindano hayo ya kila mwaka.

No comments:

Post a Comment