Atletico Madrid wakipongezana baada ya Raul Garcia kufunga bao pekee dhidi ya Valencia |
Raul Garcia akishangilia bao lake |
Bao pekee la kichwa lililofungwa na Raul Garcia katika dakika ya 43 lilitosha kuipaisha Atletico kwa klufikisha pointi 88, sita zaidi ya wapinzani wao Real Madrid wanaowafukuzia kwenye nafasi ya pili.
Washindi hao wanaotarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kuumana na Chelsea kwenye mechi ya mkondo wa pili ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya umeifanya kusaliwa na mechi mbili tu kati ya tatu kutawazwa kuwa mabingwa wapya.
Katika mchezo huo beki wa Atletico Juanfran alijikuta akitolewa nje dakika za lala salama kwa kadi nyekundu kutokana na madhambi aliyofanya.
Watetezi wa taji hilo Barcelona waliopo nafasi ya tatu watashuka dimbani baadaye kuumana na Villarreal ikiwa ugenini kujaribu kurejesha matumaini yao.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Athletic Bilbao ikiwa nyumbani ilipata ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya wageni wao Sevilla.
Mabao ya washindi yalitupiwa kimiani na Susaeta dakika ya tano kabla ya Muniain kuongeza la pili dakika ya 53 na Ander Herrera kufunga la tatu dakika ya 73 kabla ya wana nusu fainali wa Ligi Ndogo ya Ulaya Sevilla iliyocheza pungufu ya mchezaji mmoja kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Gameiro katika dakika ya 79.
Ushindi huo umeifanya Bilbao kuzidi kujiweka pazuri katika mbio zao za kuwania ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya mtoani ikiishusha Sevilla katika nafasi ya nne.