Maiti inayodaiwa ilikuwa ikisafirishwa ikiwa na dawa za kulevya |
Gari lililonaswa na dawa na maiti hiyo |
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Faustine Shilogile, watuhumiwa hao walikamatwa usiku wa kuamkia jana baada ya msamaria mwema kutoa taarifa kwa polisi kuwa kuna wanasafirisha maiti hiyo inayohisiwa kuwekwa dawa hizo tumboni.
Shilogile alisema baada ya kupata taarifa hizo, waliweka mtego katika kizuizi cha polisi cha Barabara ya Mikumi- Iringa kilichopo wilayani Kilosa.
Kamanda Shilogile aliwaambia waandishi wa habari kuwa ilipofika saa saa 3.26 usiku, askari wa jeshi hilo katika kizuizi hicho, alisimamisha gari aina ya Spacio lililokuwa likiendeshwa na madereva wawili kwa kupokezana.
Aliwataja madereva hao kuwa ni Teddy Sichilima (27), mkazi wa Mtaa wa Mwaka Tunduma na Lucas Swila (32), mkazi wa mtaa Sogea mkoani Mbeya.
Kamanda Shilogile alisema katika gari hilo pia kulikuwa na abiria aliyetambuliwa kwa jina la Hamad Mbano (36), mfanyabiashara na Mkazi wa Mtaa wa Jangwani Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Alisema watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha maiti hiyo ya Khalid Abdul Kitala (47), aliyekuwa mfanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam.
Alisema baada ya upekuzi, polisi waliitilia mashaka maiti hiyo kutokana na mazingira ya kuisafirisha yalivyokuwa.
Kamanda Shilogile alieleza kuwa mmoja wa watuhumiwa alidai kusafirisha maiti hiyo ya mkwe wake aliyefia mkoani Mbeya.
Alisema polisi walililishikilia gari hilo na watuhumiwa hao na kuwapeleka Kituo cha Polisi Mkoa wa Morogoro kwa upekuzi zaidi.
Alisema baada ya kulifanyia upekuzi gari hilo, walikuta pipi saba za dawa hizo.
Alisema baadaye waliamua kuipeleka maiti hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro kufanyiwa uchunguzi na kukuta pipi nyingine saba zimefichwa tumboni.
Kamanda Shilogile alisema baada ya kufuatilia kwa kina zaidi, walibaini kuwa mtu huyo alifariki dunia Desemba 23, mwaka huu katika Hospitali ya Vwawa iliyopo Wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya kutokana na kumeza dawa hizo na kusafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kutolewa.
Alisema thamani ya dawa hizo haijafahamika hadi zitakapopelekwa kufanyiwa uchunguzi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.
Alisema watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi wa tuhuma dhidi yao kukamilika.
Kamanda huyo, alisema maitio hiyo imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Dk. Ritha Liamuya, alilithibitisha NIPASHE kupokea maiti hiyo, kuifanyia uchunguzi na kukuta dawa hizo za kulevya. Hata hivyo, hakutoa maelezo zaidi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment