Juma Kaseja |
Akizungumza na MICHARAZO juzi katika mahojiano maalum, Awadh aliyetua Simba akitokea Mtibwa Sugar, alisema goli alilomfunga Kaseja angeweza kufungwa kipa yeyote, hivyo mashabiki wa Yanga wasimtupie lawana kipa huyo.
Awadh alimnyang'anya mpira Kaseja aliyekuwa akiurudisha langoni mwake ili audake na kuifungia Simba bao la tatu wakati wakiitungua Yanga mabao 3-1 na akasema: "Kaseja ni kipa bora na anapaswa aheshimiwe badala ya kudhalilishwa".
"Kaseja ni kipa bora, kufungwa bao lililotokana na kosa la kawaida mchezoni isiwe sababu ya kusakamwa na kudhililishwa, sioni sababu ya kufanya hivyo wakati kipa yeyote angeweza kufanya kosa kama lile kwa bahati mbaya," alisema.
Awadh alisema kitu alichofanya siku ya pambano hilo na kufanikiwa kumzidi ujanja kipa huyo ni kule kutokata tamaa na kujiamini kuwa angemnyang'anya Kaseja mpira hasa alipobaini hawezi kuudaka katika eneo alilokuwapo.
"Kujiamini kwangu na kumkabili Kaseja ndiko kulikonifanya niweze kumzidi maarifa na kufunga, hakuja kingine," alisema na kuongeza;
"Wakati mwingine wachezaji wanapaswa kutokata tamaa kuifuata mipira kwani hutokea bahati kama ilivyoniangukia mimi siku ile, " alisisitiza Awadh anayeichezea pia timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes).
Tangu Yanga ifungwe dhidi ya Simba katika pambano hilo la kirafiki baadhi ya wanachama na mashabiki wa Yanga wamekuwa wakimsakama kipa huyo wakiamini 'aliwauza' kwa klabu yake ya zamani aliyoitumikia kwa miaka 10.
Hata hivyo, wadau mbalimbali akiwamo kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro wameibuka na kumtetea na kitendo cha Awadh kumtetea kipa huyo ni muendelezo wa Kaseja kuungwa mkono na watu wengi.
No comments:
Post a Comment