STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Tuesday, April 30, 2013

Simon Mberwa kuzihukumu Yanga, Coastal Union

Wachezaji wa Yanga wataendelea kushangilia ushindi kama hivbi kesho kwa Coastal Union?

Na Boniface Wambura
MWAMUZI Simon Mberwa ndiye atakayezichezesha timu za Yanga na Coastal Union katika pambano lao namba 172 la Ligi Kuu Tanzania Bara inayoingia raundi ya 25 kesho kwa michezo mitano tofauti katika miji ya Dar es Salaam, Turiani, Morogoro na Mlandizi.

Licha ya kuwa tayari Yanga imetawazwa kuwa mabingwa wa VPL msimu huu (2012/2013), mechi dhidi ya Coastal Union itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni moja kati ya zitakazovuta macho na masikio ya washabiki wa mpira wa miguu nchini.

Mechi hiyo namba 172 itachezeshwa na mwamuzi Simon Mberwa kutoka Pwani akisaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara wakati mwamuzi wa mezani atakiwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni David Lugenge kutoka Iringa.

Viingilio katik mechi hiyo itakayoanza saa 10.15 jioni ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh. 8,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani siku ya mchezo.

Mtibwa Sugar itakuwa mwenyeji wa African Lyon katika mechi namba 170 itakayochezeshwa na mwamuzi Dominic Nyamisana wa Dodoma kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro. Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000 uko tayari kwa mechi kati ya JKT Ruvu na Tanzania Prisons. Nayo Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini ulioko Mlandizi, Pwani kuikabili Oljoro JKT kutoka Arusha.

Mtanzania apewe ITC ya kucheza Msumbiji


Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Yusuf Kunasa kucheza nchini Msumbiji.

Shirikisho la Mpira wa Miguu cha Msumbiji (FMF) lilituma maombi TFF kumuombea hati hiyo Kunasa anayekwenda kujiunga na timu ya Estrela Vermelha da Beira inayocheza Ligi Kuu nchini humo.

Kunasa ambaye msimu huu hakuwa na timu (free agent) amejiunga na timu hiyo akiwa mchezaji wa ridhaa (amateur). Zaidi ya wachezaji kumi kutoka Tanzania hivi sasa wanacheza katika klabu mbalimbali nchini Msumbiji.

Simba na Polisi Moro wavuna Mil 18 tu!


 
Na Boniface Wambura
PAMBANO namba 163 la Ligi Kuu ya Vodacom lililochezwa juzi (Aprili 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Simba kuibuka ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Morogoro limeingiza sh. 18,014,000.

Watazamaji 3,145 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,564,252.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,747,898.31.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 2,841 na kuingiza sh. 14,205,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 36 na kuingiza sh. 720,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 1,812,331.75, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 1,087,399.05, Kamati ya Ligi sh. 1,087,399.05, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 543,699.53 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 422,877.41.

Coastal Unioni kutibua sherehe za ubingwa Jangwani kesho?




Coastal Union
KIVUMBI cha Ligi Kuu Tanzania Bara kinatarajiwa kuendelea tena kesho kwa michezo sita, likiwamo la Mabingwa wapya wa ligi hiyol, Yanga dhidi ya wagosi wa Kaya, Coastal Union walioapa kuwatibulia wana Jangwani sherehe zao za ubingwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ilitawazwa kuwa mabingwa Ijumaa iliyopita baada ya wapinzani wao wa karibu Azam kulazimishwa sare ya bao 1-1 na wagosi hao wa kaya waliokuwa kwenye uwanja wao wa Mkwakwani-Tanga.
Uongozi wa Yanga na benchi la ufundi la timu hiyo, liemsisitiza kuwa kunyakua kwao ubingwa hakuwafanyi walegeze makali yao ambapo tangu kuanza kwa duru la pili hawajapoteza mechi yoyote.
Hata hivyo kocha wa Coastal, Hemed Morocco amenukuliwa juzi akisema kuwa wamekuja Dar kwa ajili ya kutibua furaha ya ubingwa ya Yanga na kwamba mabingwa hao wasitarajie mteremko kwani lengo lao kuona wakimaliza ligi wakiwa kwenye Tatu au Nne Bora.
Wakati Yanga na Coastal zikitambiana hivyo kabla ya kuvaana kesho Dar, michezo mingine itakayochezwa kesho ni pamoja na lile la Mtibwa Sugar dhidi ya 'vibonde' Agfrican Lyon ambayo imeshashuka daraja, japo bado hawajatangazwa rasmi na TFF kama desturi.
Timu hizo zitaumana kwenye uwanja wa Manungu Complex, Turiani, ambapo Mtibwa itakuwa ikisaka pointi za kuwafukuzia ndugu zao, Kagera Sugar waliopo nafasi ya tatu katika msimamo.
Kagera wenyewe watakuwa ugenini mjini Morogoro kuvaana na Polisi Moro ambayo kama ilivyo kwa Lyona na Toto ni kama zimeshajikatia tiketi ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza ilikoicheza msimu uliopita kabla ya kupanda Ligi Kuu msimu huu.
Polisi na Lyon zote zina pointi 19 kila moja na hata zikishinda mechi zao za mwisho zitafikisha pointi 25 ambazo zimerukwa na asilimia kubwa ya timu zinazoshiriki ligi hiyo itakayofikia tamati yake Mei 18.
Pambano jingine la kesho litazikutanisha timu za maafande za Ruvu Shooting itakayokuwa nyumbani kuwakabili wageni wao JKT Oljoro kwenye uwanja wa Mabatini-Mlandizi Pwani.
Tayari Afisa Habari wa Ruvu, Masau Bwire alemchimba mkwara kwamba vijana wao wapo tayari kutoa dozi kwa Oljoro kabla ya kuwakabilia Simba Jumapili kwenye uwanja wa Taifa, baada ya mechi yao ya awali kusogezwa mbele kitatanishi dakika za lala salama kabla ya kuanza kwake.
Bwire alisema lengo lao ni kuhakikisha mechi zao nne zilizosalia wanazishinda zote na kuwa fanya wamalize msimu wakiwa na pointi 42 zinazoweza kuwaweka katyika nafasi ya Tatu Bora au Nne msimu huu.
Mchezo wa mwisho kwa kesho utachezwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam kwa maafande wa JKT Ruvu watakapowakaribisha askari wenzao wa Magereza, Prisons-Mbeya ambazo hazina cha kupoteza kwenye msimamo wa ligi hiyo kutokana na kwamba zote hazina nafasi ya ubingwa wala kushuka daraja.
Msimamo wa Ligi hiyo kwa sasa ni kama ifuatayvyo:


                             P      W     D     L     F      A     D     Pts
Young Africans      24    17     5     2     44     13    31    56
Azam                    24    14     6     4     42     20    22    48    
Kagera Sugar        23    11     7     5     26     18     8     40     
Simba                   23    10     9     4     34     22    12     39
Mtibwa Sugar       24     9      9     6     27     24     3      36   
Coastal Union       24     8    10     6     24     21     3      34    
Ruvu Shooting      23     8     6      9     21     22     -1     30     
JKT Oljoro FC    24     7     7     10    22     28     -6     28     
Tanzania Prisons   24     6     8     10    14     21     -7     26    
Ruvu Stars           24      7     5     12    20     37     -17   26
JKT Mgambo       23     7     4     12    15     23     -8     25
Toto Africans       25      4     10   11    22     33     -11    22
African Lyon        24      5     4     15     16    36     -20     19
Polisi Morogoro   24      3    10    11     12    23     -11     19    
             

Mourinho na vijana wake kuvuna nini leo Ulaya?

http://www.footballtarget.com/wp-content/uploads/2012/11/real-madrid-vs-borussia-dortmund-match-preview-champions-league.jpg
KOCHA Jose Mourinho na vijana wake wa Real Madrid leo wana kibarua kizito cha kuudhibitishia dunia kwamba soka lina maajabu yake watakapowakaribisha Borussia Dortmund nyumbani kwao, Santiago Bernabeu katika nusu fainali ya marudiano wakiwa na deni la kipigo cha mabao 4-1 walichopewa ugenini.
Mourinho na vijana wake walichezea kichapo cha mabao 4-1 ugenini nchini Ujerumani katika pambano la kwanza la Nusu Fainali ya michuano hiyo na hivyo leo watalazimika kulipa kisasi ili  kutinga fainali na kusaka taji la 10 na la kwanza tangu mwaka 2002.

Madrid watahitajika kushinda mabao 3-0 ili kutinga fainali za Ulaya baada ya misimu kadhaa ya ukame wa taji hilo tangu ilipotwa mara ya mwisho mwaka 2002.
Hata hivyo huenda isiwe kazi rahisi kwa vijana wa Santiago Bernabeu kutokana na ukweli wapinzani wao wapo vyema msimu huu licha ya kutemeshwa taji la ubingwa wa Bundesliga na Bayern Munich.
Dortmund wanasaka heshima baada ya kutwaa taji hilo mara ya mwisho mwaka 1997, hivyo huenda hawatakubali kuipoteza nafasi waliyopata safari hii kwa mabao manne ya Robert Lewandowski aliyefunga katika pambano la awali wiki iliyopita.
Wakati hatma ya Madrid na Dortmund ikitarajiwa kufahamika usiku wa leo, mabingwa wengine wa zamani wa Ulaya, Barcelona na Bayern Munich zenyewe zitakuwa na kibarua kingine kesho nchini Hispania.
Barcelona iliyocheze kichapo cha aibu wiki iliyopita ugenini kwa kulala kwa mabao 4-0 itakuwa nyumbani kujaribu kutupa karata yake kwa wageni wao ambao msimu huu wanatisha kisoka barani Ulaya.
Ikiwategemea nyota wake kama Xavi, Iniesta, Cesc Fabregas na Lionel Messi, Barca itakuwa na kazi pevu kulipiza kisasi na kutaka kupenya katika pambano hilo ili kucheza fainali Mei 25 itakayochezwa kwenye uwanja wa Wembley, Uingereza.
Je, ni Wahispania au Wajerumani watakaoenda London kwenye fainali hizo? Tusubiri tuone maana soka lina maajabu yake.

Bi Hindu ashirikishwa Fungate la Kifo



MTUNZI wa riwaya na simulizi za kusisimua anayezidi kuja juu nchini, Ramadhan Yahya, ameamua kugeukia fani ya filamu akifyatua kazi iitwayo 'Fungate la Kifo', iliyowashirikisha wasanii mbalimbali akiwemo nyota wa Kaole Sanaa, Chuma Suleiman 'Bi Hindu'.
Akizungumza na MICHARAZO jana, Yahya aliyewahi kutamba na vitabu kama 'Uchawi Uliosumbua Maisha Yangu, 'Bibi Yangu Mchawi', na 'Katikati ya penzi' alisema filamu hiyo mpya imekamilika na inafanyiwa mipango ya kuanza kuisambaza.
Yahya alisema hiyo ni filamu yake ya pili baada ya ile ya 'Uchawi Uliotesa Maisha Yangu' iliyotokana na kitabu chake cha awali na imewashirikisha wasanii mchanganyiko wazoefu na chipukizi.
Aliwataja baadhi ya wasanii hao ni Chuma Suleiman maarufu kama 'Bi Hindu', Maua Mbwana na wasanii wengine wanaoibukiwa kwenye fani hiyo.
"Baada ya filamu yangu ya kwanza kufanya vyema kwa sasa natarajia kuja na filamu ya 'Fungate la Kifo' ambayo imeshirikisha wasanii mchanganyiko," alisema Yahya.
Aliongeza kuwa, tofauti na filamu ya awali 'Fungate la Kifo' ataisambaza mwenyewe kwa kile alichodai filamu ya awali hakuambulia cha maana cha kujivunia.
"Nitaisambaza mwenyewe, maana watu tunaowaamini wanatuumiza mno, tunatumia gharama kubwa kuzalisha filamu, lakini malipo tunayoambulia ni mkia wa mbuzi, tunawanufaisha wao, najaribu mwenyewe nione inakuwaje," alisema.
Aidha mtunzi huyo wa hadhithi na mchora katuni, alisema kwa sasa anafanya mipango ya kusaka mfadhili wa kusimamia kazi zake ili fedha zitakazopatikana katika sanaa yake aziwekeze kwa kuanzisha asasi ya kuwasaidia yatima, wajane na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.

MAZOEZI YA MISS KIBAHA 2013 YAZIDI KUPAMBA MOTO

Mkufunzi wa Warembo wa Miss Kibaha Rehema Uzuwiya akizungumza na warembo hawo wakati wa mazoezi yao yanayo endelea katika ukumbi wa Vijana Kinondoni

Warembo wa miss kibaha wakiwa katika pozi wakati wa mazoezi yao

Warembo watakao wania taji la Miss Kibaha wakiwa katika pozi wakati wa mazoezi yao yanayoendelea katika ukumbi wa vijana Kinondoni Dar es salaam