|
Mlela akipeana mkono na Katibu Mtendani wa Bodi ya Filamu nchini, Joyce Fisoo |
Na Genofeva Matemu, MaelezoWASANII wa filamu nchini wameshauriwa kutumia taaluma waliyonayo kupanua wigo wa filamu nchini na kuitangaza Tanzania duniani kote kwa kuzingatia matumizi mazuri ya lugha ya Kiswahili katika filamu wanazozitengeneza.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, juzi alipokutana na wasanii waliotarajia kuondoka jana kwenda Uingereza kurekodi filamu ya 'Sabasi' na Kampuni ya Didas Entertainment iliyopo nchini humo.
Fisoo alisema kuwa baadhi ya wasanii nchini wamekuwa makontena yanayopitisha biashara haramu kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine hivyo kuwaomba wasanii wanaokwenda Uingereza kuachana na tabia hiyo bali watumie fursa waliyoipata kuiwakilisha Tanzania vizuri na kutengeneza filamu bora itakayowawezesha kujulikana na kufungua fursa za kushirikishwa katika filamu na nchi nyingine duniani.
Aidha, Fisoo aliwataka wasanii hao kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za Uingereza kwani kwa kufanya hivyo watakuwa mabalozi bora na kutoa nafasi kwa wasanii wengine kupata fursa hizo.
Naye Mama wa Didas Entertainment, Nuru Idrisa, aliwataka wasanii wa Bongo Movie waliopata nafasi ya kurekodi filamu na Didas Entertainment kujiheshimu na kuvaa mavazi ya staha yatakayostiri miili yao muda wote watakaokuwa nchini Uingereza kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wamelinda heshima ya nchi.
Akitoa neno la shukrani, msanii wa Bongo Movie, Yusuph Mlela, aliishukuru Bodi ya Filamu kwa kuwa bega kwa bega na wasanii na kuwaahidi wadau wa filamu nchini kazi bora na yenye tija katika jamii.
Filamu ya 'Sabasi' inatarajiwa kurekodiwa hivi karibuni nchini Uingereza na Kampuni ya Didas Entertainment na kuwashirikisha wasanii Mlela, Esha Buhet na Husna Athumani, na ni filamu ya pili kurekodiwa na kampuni hiyo na kuwashirikisha wasanii kutoka Tanzania. Filamu ya kwanza kurekodiwa na kampuni hiyo iliyowashirikisha wasanii kutoka Tanzania ni ile ijulikanayo kwa jina la 'Mateso Yangu Ughaibuni'.