Campbell (10) akishangilia moja ya mabao yake na wachezaji wenzake wa Cardiff |
WAKATI Roberto Saldado akiendelea kuibeba Tottenham Hotspur kwa kuipa ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu ya England vijana wa Manuel Pellergrini, Manchester City jioni hii wameonja kipigo toka kwa Cardiff.
Man City wamejikuta wakizodolewa kwa kulazwa mabao 3-2 na waliopanda daraja Cardiff katika pambano lililojaa upinzani mkubwa.
Mabao mawili ya lala salama yaliyofungwa kwa kichwa na Fraizer Campbell yalitosha kuwazima Man City waliokuwa ugenini na kuwapa wenyeji ushindi wa kwanza Cardiff.
City walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Edin Dzeko muda mchache baada ya kuanza kwa kipindi cha pili baada ya dakika 45 za awali timu hizo kushindwa kutambiana.
Hata hivyo bao hilo lilirudishwa na Cardiff dakika ya 60 na Aaron Gunnarsson kabla ya Campbell kufunga mabao yake dakika za 79 na 87 na City kuambulia bao jingine dakika ya 90 lililofungwa na Alvaro Negredo.
Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyotangulia kuchezwa, Tottenham ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wageni wao Swansea City kwa bao la penati iliyofungwa na Saldado ambaye ni bao lake la pili baada ya wiki iliyopita kuifungia pia Spurs bao la penati iliposhinda ugenini.