STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, May 3, 2013

Mfanyabiashara Kariakoo ajirusha toka ghorofa ya 9, kisa...

Mfanyabiashara huyo akiwa hoi kando ya gari alilolidondokea ambalo liliharibika vibaya kama inavyoonekana pichani
MCHANA wa leo mitaa ya Kariakoo, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja tu la Shirima,  ambaye anadaiwa ni mfanyabiashara katika moja ya maduka yaliyopo eneo hilo la  Kariakoo, Dar es Salaam, amejirusha toka ghorofa ya 9 ya Hoteli ya Concord.
habari ambazo zimepatikana na kusimuliwa na mashuhuda wa tukio hilo lililosikitisha wengi, linasema kuwa mfanyabiashara huyo alijirusha toka kwenye jengo hilo na kuangukia gari kabla ya kukimbizwa hospitali kwa uangalizi zaidi maana haijafahamika kama kapoteza Maisha au bado yu hai.

Mfanyabiashara huyo alijirusha toka ghorofani na kuangukia Gari aina ya Toyota Corolla ambayo ni taxi iliyokuwa imepaki nje ya hoteli hiyo....chanzo cha kujirusha kwa mfanyabiashara huyo bado hakijafahamika mpaka sasa.

Mashuhuda wa tukio hilo lililotokea muda si mrefu wanaeleza kuwa walipatwa na mshuko baada ya kusikika kishindo cha kitu kilichokuwa kimeangukia gari hilo na waliposogea kushuhudia ndipo walipobaini kuwa alikuwa ni mtu huyo alietambulika kwa jina moja la Shirima.

Azam yaendelea kuanika sababu za kuing'oa AS FAR Rabat kesho nchini Morocco

Mshambuliaji John Bocco 'Adebayor' akichuana na wachezaji wenzake mazoezini mjini Rabat, Morocco kujiandaa na pambano lao la kesho dhidi ya AS  FAR Rabat

Na Patrick Kahamela, Rabat
SIKU chache zilizopita tulijadili juu ya sababu mbili kati ya sita, kwa nini Azam FC ina nafasi kubwa ya kuibwaga AS FAR, katika, katika makala ya jana tuliangalia jinsi Azam FC ilivyofanya maandalizi kabambe kwa kuijengea timu kujiamini kwa kuipa mechi za majaribio na maandalizi mengine. Baada ya hapo tulijadili jinsi Azam FC ilivyo na wachezaji kabambe wenye uwezo wa kupambana na timu yoyote kwenye mashindano ya Afrika. Tulifanikiwa kuwaangalia wachezaji wa eneo la ulinzi pekee, leo tutawaangaliwa wachezaji wa kiungo na ushambuliaji na sababu nyingine nne zilizosalia zinazoifanya Azam FC iwe katika nafasi kubwa ya kuitoa AS FAR.

Azam FC wakati wa dirisha dogo ilimsajili mchezaji wa kiungo toka SOFAPAKA Ochieng Humphrey Mieno, tangia kuwasili mieno amekuwa habanduki kwenye kikosi cha kwanza na kazi yake nzuri imeiwezesha Azam FC kufikia mafanikio iliyonayo hadi sasa. Mieno ni mrefu kwa kimo, ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira, mzuri kwenye kusoma mbinu za adui na kupanga mipango ya kuizima na ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo wa ushambuliaji na ulinzi. Hakika usajili wa Mieno umekuwa wa maana kubwa kwa Azam FC.

Tanzania kwa sasa inajivunia kuwa na wachezaji wenye kiwango cha juu cha uchezaji na ndiyo maana timu ya taifa imekuwa ikifanya vizuri. lakini ukiwaomba mashabiki wakutajie wachezaji watatu bora zaidi nchini basi bila shaka watakuambia ni Mbwana Samata wa TP Mazembe, Shomary Kapombe wa Simba na Salum Abubakar Sure Boy wa Azam FC. Sure boy amekuwa mchezaji wa kipekee kabisa kwa sasa… uwezo wake wa kupokonya mipira, kumiliki mipira na kuipa timu umiliki wa mpira ni wa hali ya juu sana. Sure Boy anazurura sana uwanjani na hachoki kirahisi. Azam FC inajivunia kumtengeneza mchezaji huyu ambaye alitua Azam FC akiwa na miaka 16 tuu na kwa sasa amekuwa lulu inayong’aa.

Utawaambia nini mashabiki juu ya Sure? Utawaambia nini wachezaji wenzake? Muulize kocha wake juu ya Sure, wote watakuambia ni mchezaji wa dunia yake na wa kipekee. Hakika silaha kubwa ya Azam FC kesho ni Salum Abubakar.

Azam FC imejaaliwa kuwa na wachezaji wengi wa kiungo lakini Jabir Aziz Stima ana sifa ya kipekee inayomfanya kuwa mchezaji muhimu kikosini. Stima ambaye alikuwa hakosekani kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Marcio Maximo ni mchezaji pili wa Afrika baada ya Dedier Drogba kuweza kuifunga Brazil goli, je ulikuwa unalijua hilo? Stima alifuga wakati Stars ilipocheza na Brazil na kufungwa 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki mwaka 2010. Stima ni bingwa wa kukaba. Kocha wake Stewart Hall anamuita mbwa wa polisi, muingize Stima uwanjani kisha mwambie akakabe kisha uone kama wapinzani wataweza kupiga zaidi ya pasi tano. Katika mchezo wa kesho ambao ni wa ugenini… Stima anatarajia kuwa na sehemu muhimu.

Sifa za kukaba za Stima pia anazo muaiverikosti Kipre Michael Bolou na hii inaifanya Azam FC iwe na uwigo mpana wa kupanga kikosi. Kocha akitaka wakabaji basi atawapanga Jabir Aziz na Kipre Bolou, lakini akitaka kucheza mpira basi atawatumia Abdi Kassim, Humphrey Mieno, Sure Boy na Mwaipopo. Wachezaji wote hawa wamesafiri na wapo katika hali nzuri. Ni suala la kusubiri tuu kuona nini kitatokea hiyo kesho.


Kipre Bolou alisajiliwa wakati wa dirisha dogo la msimu uliopita baada ya pacha wake kipre tchetche kuonesha mafanikio makubwa. Tangia awasili kipre Bolou amekuwa mhimili mkuu wa eneo la ulinzi. Amecheza karibu mechi zote na ilipobidi alifunga magoli mazuri sana. Azam FC inajivunia kuwa na mchezaji wa kimataifa wa aina ya Kipre Bolou.


Baadhi ya wachezaji wa Azam wakipasha nchini Morocco
Baadhi ya msafara wa Azam ukiwasilia Rabat, mbele ni Patrick Kahemela na kocha Stewart Hall
Ibrahim Joel Mwaipopo ni mmoja kati ya wachezaji waliosajiliwa na Azam FC mara baada ya kupanda ligi kuu misimu minne iliyopita. Mwaipopo mchezaji anayetumia zaidi mguu wa kushoto amekuwa akicheza kwenye eneo la kiungo cha ulizi na kazi yake imekuwa ya uhakika kiasi cha kumfanya kuwa na mkataba wa muda mrefu na Azam FC. Mwaipopo ana jicho la kuona nafasi, ana pasi za uhakika fupi na ndefu lakini pia anajua kupiga mashuti yenye macho. Ukiomuona mazoezini utaamini kuwa anakwenda kuanza kesho lakini ukimkuta anaanzia bechi huta shangaa kutokana na aina ya wachezaji ambao Azam FC inao kwa sasa.

Abdi Kassim Babi ni mchezaji mzoefu zaidi kwenye kikosi cha Azam FC na siku hizi amekuwa na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa kati au kurudi kwenye eneo lake la kiungo na kucheza kama namba kumi. Babi ana uzoefu wa mashindano ya ngazi hii na uzoefu wake unatarajia kuisaidia sana Azam FC hapo kesho. Ukitafuta wachezaji wa kiungo wa Tanzania watano wenye uwezo mkubwa wa kufunga na kupiga mipira ya adhabu basi hutaacha kumtaja Abdi kassim.

UONGOZI BORA WENYE BENCHI BORA LA UFUNDI NA MIPANGO NA DHAMIRA YA USHINDI


Azam FC ina uongozi bora na makini chini ya bodi ya wakurugenzi inayoongozwa na management ya Bakhresa Group, uongozi wa Azam FC chini ya mwenyekiti Said Muhammad ulichukua kila tahadhari kwa ajili ya mchezo huu ikiwemo kutanguliza timu ya watu saba kufanya ushushushu wa mazingira yalivyo na maandaliza kabla timu haijawasili. Mashushushu hao waliuarifu uongozi umuhimu wa kuwahi na Azam FC iliandika barua TFF kuomba mechi yale na Coastal Union irudishwe nyuma ili kuweza kuwahi Rabat. Azam FC iliwasili Rabat siku sita kabla ya mchezo kuweza kufanya mazoezi kwa zaidi ya mara nane ili kuzoea hali ya hewa ya baridi kali iliyopo hapa.
 
Pia klabu ilinunua nguo za michezo za kuvaa kwenye baridi kwa ajili ya wachezaji, soksi nzito za miguuni na mikononi, fulana za kukaba za kuvaa ndani pamoja pamoja na raba za kushindia ili kuondoa sababu za hali ya hewa kuweza kuathiri maandalizi ya timu na uwezo wa timu uwanjani.


Azam FC inakaa kwenye hotel ya nyota tano ya Golden Tulip Farah hapa Rabat hii inawafanya wachezaji wasiwe na manung’uniko na wasiathirike kiasaikolojia kutokana na matatizo ya huduma. Viongozi wamekuwa wakihakikisha timu inapata kila inachohitaji na hadi sasa hakuna tatizo lolote lililojitokeza.


BENCHI LA UFUNDI
Azam FC ipo chini ya kocha Stewat Hall, huyu ni mwalimu wa kiwango cha juu sana akiwa anamiliki cheti cha ukocha cha UEFA PRO LICENCE inayomfanya kuwa mkufunzi wa makocha kule uingereza.



Makocha wa Azam, Waingereza John Stewart Hall na Kally Ongalla
  
Stewart Hall kwa kushirikiana na wasaidizi wake wamepata nafasi si tuu ya kuangalia mikanda ya video ya AS FAR waliyotafutiwa, lakini pia wamepata nafasi ya kuwaangalia AS FAR ‘live’ wakiwa uwanjani na hii inawapa uelewa zaidi na kubuni mbinu za kuwakabili.


Azam FC imekamilika na imekuja na timu kamili akiwemo kocha mkuu Stewart Hall, wasaidizi wake Kalimangonga Ongala na Iddi Abubakar, Mtunza vifaa Joseph Nzawila, Meneja Jemedary Said na Daktari Juma Mwanandi Mwankemwa. Hakika timu imejipanga na ina hamu ya kushinda na kuiweka Tanzania kwenye ramani ya soka.

Golden Bush Veterani wapeleka 'maafa' Staki Shari Ukonga


 
Wazee wa Kazi, Golden Bush Veterani
 
Wazee wa Staki Shari Veterani walioumizwa na Golden Bush juzi
WAKALI wa Soka la wazee jijini Dar es Salaam, Golden Bush majuzi waliendeleza libeneke lao baada ya kuwanyuka Staki Shari Veterani kwa mabao 4-0 katika pambano maalum la kusherehekea sikukuu ya Wafanyakazi 'May Day'.
Kwa mujibu wa msemaji na mlezi wa klabu ya Golden walipata ushindi huo katika pambano hilo lililochezwa Ukonga na kuwashtukiza wenyeji wao kwa mabao mawili ya haraka kabla ya Staki Shari kukomaa.
Hata hivyo pamoja na kutuliza akili na kushambulia lango la wageni wao, haikuwasaidia kuwazuia wazee wa Golden Bush waliokuwa wakiongozwa na nyota wa zamani wa timu za Simba na Yanga pamoja na msemaji huyo, Onesmo Waziri 'Ticotico' kwa kuruhusu mabao mengine mawili.
Ticotico alisema kwa namna walivyokuzishughulikia timu zao pinzani ndani ya wiki mbili wameamua safari hii kupumzika kabla ya kuangalia waelekeze mashambulizi yao mitaa ipi ya jijini au nje ya Dar es Salaam.

Kiporo cha Simba, Ruvu Shooting kupigwa J'pili Taifa


Na Boniface Wambura
LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja tu ya kiporo kati ya  Ruvu Shooting dhidi ya Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.

Pambano hilo awali lilikuwa lichezwe Aprili 25, lakini likaahirishwa dakika za lala salama kutokana na uwanja huo wa Taifa kutumiwa na serikali kwa maandalizi ya sherehe za Muungano zilizofanyika siku iliyofuata kwenye uwanja wa Uhuru unaoendelea kutengenezwa.

Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.

African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.

TFF kukutana kujadili utekelezaji wa maagizo ya FIFA

Rais wa TFF, Leodger Tenga



Na Boniface Wambura
Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Mei 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuhusu uchaguzi wa shirikisho.

Kikao hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.

FIFA katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.

TFF yaitakia kila la heri Azam Morocco

Watanzania wanatarajia furaha kama hii kwa Azam iwepo pia katika pambano lao la kesho nchini Morocco

Na Boniface Wambura
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaitakia kila la kheri timu ya Azam katika mechi yake ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayochezwa Morocco kesho (Mei 4 mwaka huu).

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano hiyo itachezwa jijini Rabat kuanzia saa 11 jioni kwa saa za Morocco. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Azam iko nchini Morocco kwa karibu wiki nzima sasa ikijiandaa kwa mechi hiyo chini ya Kocha wake Stewart John Hall. Msafara wa Azam nchini humo unaongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella.

25 waripoti kambi ya Young Taifa Stars

Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen
Na Boniface Wambura
Wachezaji 25 kati ya 30 walioitwa na Kocha Kim Poulsen kwenye kikosi cha pili cha Taifa Stars (Young Taifa Stars) wameripoti kambini ambapo mazoezi yalianza tangu jana jioni (Mei 2 mwaka huu).

Kocha Kim amewaitaka wachezaji katika kambi hiyo ya siku tano ili kuangalia uwezo wao katika maeneo kadhaa kwa lengo la kupata baadhi ambao anaweza kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars siku za usoni.

Wachezaji watano walioshindwa kujiunga katika kambi ya timu hiyo iliyoko hoteli ya Sapphire jijini Dar es Salaam ni Aishi Manula, David Mwantika, Himid Mao, Samih Nuhu na Seif Abdallah ambao wako Morocco na timu yao ya Azam.

Kamati ya Mashindano TFF kupitia mchakato wa Ligi ya Mabingwa wa Mikoa


Na Boniface Wambura
Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.

Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).

Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.

Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.

Yanga, Coastal wavuna Mil.66


Na Boniface Wambura
Mechi namba 172 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa juzi (Mei 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 imeingiza sh. 66,022,000.

Watazamaji 11,478 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,378,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,071,152.54.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 10,230 na kuingiza sh. 51,150,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 69 na kuingiza sh. 1,380,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,819,793.62, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 4,691,876.17, Kamati ya Ligi sh. 4,691,876.17, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,345,938.09 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,824,618.51.

EXCLUSIVE: HATIMAYE NSA JOB APELEKA JINA LA KIGOGO TFF

MSHAMBULIAJI wa Coast Union, Nsa Job amewasilisha barua kwenye Shirikisho la soka (TFF) ambayo inamtaja kigogo ambaye alimpa rushwa.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimtaka mchezaji huyo kujieleza kutokana na kukaririwa akiongeza katika kituo kimoja cha radio akikiri kupokea rushwa ya sh2mil kwa mmoja wa kiongozi wa timu kubwa ili acheze chini ya kiwango pindi walipokuwa wanacheza na timu hiyo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa tayari mchezaji huyo amekwisha tuma barua ya kujieleza nao wameamua kulipeleka suala hilo katika kamati ya nidhamu ambayo inatarajiwa kukutana wiki ijayo.

Alisema mbali na suala hilo pia kamati hiyo itapitia mambo mbali mbali ya ligi kuu ambayo yametokea ikiwemo suala la viongozi ambao walikuwa wanatoa maneno ya uchochozi.

Alisema viongozi wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni za soka sio kuongea ongea vitu visivyo na maana ambavyo vitaleta matatizo katika soka.

Moja ya Viongozi ambao watajadiliwa ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga baada ya kudaiwa kutoa maneno ya uchochezi pindi TFF, walipohairisha mechi yao dhidi ya Mgambo JKT ya Tanga.  


CHANZO:SHAFII DAUDA

LADY JAYDEE KUZINDUA ALBAMU MIAKA 13 ya KISANII


Binti Machozi a.k.a Comandoo, Lady JayDee
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Katika mwaka huu 2013, Inatimia miaka 13 tangu nianze kazi ya muziki.
Nashukuru MUNGU tuko pamoja na pia, nashukuru umma wa Tanzania kwa kuendelea ku support muziki wa Tanzania na kunipa nguvu mimi kama msanii.
Nashukuru vyombo vyote vya habari vinavyoshiriki kikamilifu kukuza na kulinda sanaa ya Tanzania bila kujali maslahi binafsi.
Tumeandaa sherehe kubwa na nzuri ya miaka 13 ya LADY JAYDEE, katika muziki.
Na mdhamini mkuu kwa upande wa media ni East Africa TV.
Sherehe ya miaka 13 ya Lady JayDee katika muziki itaambatana na uzinduzi wa album yangu ya sita inayokwenda kwa jina la NOTHING BUT THE TRUTH ambayo ina jumla ya nyimbo 10.
Katika sherehe hizo pia kutakuwa na show ya nyimbo zote bora za JayDee nikishirikiana na baadhi ya wasanii wenzangu hapa nchini.
Sherehe zitafanyika Ijumaa tarehe 31 May 2013.
Nawakaribisha wote tufurahi pamoja
Na Mungu awabariki

Chelsea, Benfica kucheza fainali ya UEFA League


Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao jana dhidi ya Basel
Oscar Cordozo akishangilia moja ya mabao yake mawili aliyoifungua Benfica jana na kuipeleka fainali ya Europas League


CHELSEA ya England usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kutinga fainali ya Europa League baada ya kuifunga Basle ya Uswisi mabao 3-1 katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya ligi hiyo lililochezwa uwanja wa Stamford Bridge.
Ushindi huo mnono umeifanya Chelsea kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya wiki iliyopita kuinyuka Basle nyumbani kwao mabao 2-1 na sasa itavaana na Benfica ya Ureno ambayo jana ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Waturuki, Fenerbache.
Chelsea walitanguliwa kufungwa bao na wageni wao dakika chache kabla ya mapumziko kupitia Salah kabla ya kurejesha mabao hayo mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Fernando Torres aliisawazishia Chelsea bao dakika ya 50 kabla ya Victor Moses kuongeza la pili dakika mbili baadaye na David Luiz kupigilia msumari wa mwisho dakika saba baadaye kwa kufunga bao la tatu.
Nayo Benfica ikiwa nyumbani iliwatungua Fenerbache kwa mabao 3-1 na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa bao 1-0 ugenini.
Mabao ya wenyeji yaliwekwa kimiani na Gaitan dakika ya 9 kabla ya Dick Kuyt kusawazisha kwa njia ya penati dakika ya 23 na Cordozo kuongeza bao la pili kwa Benfica dakika ya 35 na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Cordozo aliiandikia tena Benfica bao la tatu na kuihakikishia nafasi ya kucheza fainali za michuano hiyo itakayopigwa Mei 15 kwenye mji wa Amsterdam, Uholanzi.