Chelsea wakishangilia moja ya mabao yao jana dhidi ya Basel |
Oscar Cordozo akishangilia moja ya mabao yake mawili aliyoifungua Benfica jana na kuipeleka fainali ya Europas League |
CHELSEA ya England usiku wa kuamkia leo imefanikiwa kutinga fainali ya
Europa League baada ya kuifunga Basle ya Uswisi mabao 3-1 katika pambano la marudiano la Nusu Fainali ya ligi hiyo lililochezwa uwanja wa Stamford Bridge.
Ushindi huo mnono umeifanya Chelsea kutinga hatua hiyo kwa jumla ya mabao 5-2 baada ya wiki iliyopita kuinyuka Basle nyumbani kwao mabao 2-1 na sasa itavaana na Benfica ya Ureno ambayo jana ikiwa nyumbani ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Waturuki, Fenerbache.
Chelsea walitanguliwa kufungwa bao na wageni wao dakika chache kabla ya mapumziko kupitia Salah kabla ya kurejesha mabao hayo mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Fernando Torres aliisawazishia Chelsea bao dakika ya 50 kabla ya Victor Moses kuongeza la pili dakika mbili baadaye na David Luiz kupigilia msumari wa mwisho dakika saba baadaye kwa kufunga bao la tatu.
Nayo Benfica ikiwa nyumbani iliwatungua Fenerbache kwa mabao 3-1 na kushinda kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya wiki iliyopita kufungwa bao 1-0 ugenini.
Mabao ya wenyeji yaliwekwa kimiani na Gaitan dakika ya 9 kabla ya Dick Kuyt kusawazisha kwa njia ya penati dakika ya 23 na Cordozo kuongeza bao la pili kwa Benfica dakika ya 35 na kufanya hadi mapumziko matokeo kuwa 2-1.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Cordozo aliiandikia tena Benfica bao la tatu na kuihakikishia nafasi ya kucheza fainali za michuano hiyo itakayopigwa Mei 15 kwenye mji wa Amsterdam, Uholanzi.
No comments:
Post a Comment