PAZIA la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 unatarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu ambapo timu zote 14 zitashuka dimbani kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu, imefahamika.
Akizungumza jijini jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia, alisema kuwa tarehe hiyo imeshapitishwa katika kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na tayari pia mechi za ligi hiyo zimeshapangwa lakini hazijathibitishwa na kamati yake kama taratibu zinavyoeleza.
Karia alisema kuwa tayari 'wataalamu' ambao huhusika na zoezi la kupanga ratiba za mechi wameshakamilisha zoezi hilo lakini kamati yake ndiyo inasubiriwa kupanga siku ya kukutana ili kuithibitisha.
"Ligi itaanza tarehe 24 Agosti ila nani ataanza na nani ndiyo bado hatujapitisha, tukishakutana na kupitia hilo kwa kuzingatia mazingira yetu ya timu kusafiri ndiyo itatolewa hadharani. Tutakuwa makini sana kwa sababu hatutaki makelele yaliyojitokeza mwaka jana na miaka ya nyuma yaendelee," alisema Karia ambaye ameshasema kuwa atawania cheo cha Makamu wa Rais katika uchaguzi ujao wa shirikisho hilo utakaofanyika Septemba.
Hata hivyo, Karia alisema kuwa suala la wadhamini wa ligi hiyo bado halijakamilika lakini kubwa wanachotaka ni kuona ni klabu zinafaidika na udhamini utakaopatikana.
Alisema kuwa kamati yake inatarajia kukutana Julai 3 asubuhi ili kupitia taarifa za msimu uliopita na kupata washindi wa tuzo mbalimbali na jioni yake washindi hao watatangazwa na kutunukiwa.
"Tumepanga tukutane siku hiyo hiyo ya tuzo ili habari zisivuje, kwa sababu kila mtu na kifua chake cha kuweka mambo… hadi sasa ni bingwa, mshindi wa pili na wa tatu ndiyo wanajulikana. Lakini kocha bora na tuzo nyingine tutajua siku hiyo baada ya kuangalia na kuthibitisha rekodi tulizonazo," aliongeza Karia.
Kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, bingwa mtetezi Yanga na mshindi wa pili, Azam watakutana katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii kama kanuni za ligi zinavyosema.
Timu 14 za msimu ujao wa ligi ni pamoja na Yanga, Azam, Simba, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Coastal Union, JKT Oljoro, JKT Ruvu, Ruvu Shooting, Mgambo Shooting, Prisons na zilizopanda daraja ambazo ni Mbeya City, Ashanti na Rhino Rangers ya Tabora.
NIPASHE