STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, September 5, 2012

Eddo Boy: Kinda la Simba achekeleaye kuitungua Mtibwa Sugar

LICHA ya kuibuka mfungaji bora wa michuano ya Super8, mshambuliaji kinda wa Simba, Edward Christopher Shija 'Eddo Boy' a.k.a Teko Modise, amedai hajafurahishwa kama alivyoibebesha timu yake ubingwa wa michuano hiyo. Eddo, alisema tuzo ya ufungaji bora kwake isingekuwa na maana kama Simba isingekuwa mabingwa kwa jinsi walivyojituma na kuipigania timu yao. "Ingawa mechi ya fainali dhidi ya Mtibwa Sugar kwangu ni mechi ngumu kuwahi kuicheza kwa jinsi ilivyokuwa na funga nikufunge, ila sijivunii tuzo ya ufungaji bora wala kung'ara kwangu zaidi ya kuipa Simba ubingwa," alisema. Alisema, mara pambano lilipoisha akiifungia bao la ushindi katika matokeo ya mabao 4-3, alijisikia faraja kwa kutwaa taji jingine akiwa na Simba. "Mechi na Mtibwa sintoisahau kwa walivyocheza na kurejesha mabao yetu kila tulipofunga kabla ya kuwazidi ujanja kwa bao la nne lililotupa ubingwa, hakika najisikia fahari kwa kuilaza Mtibwa na kuipa Simba taji jingine," alisema. Kabla ya taji hilo, Eddo alishatwaa na Simba mataji ya Rolling Stone 2011, Kinesi 2011, Uhai 2011 na Ujirani Mwema lililochezwa mwaka huu. Pamoja na mafanikio yote, Eddo anayeichezea pia timu ya taifa, akipandishwa mwaka huu na kocha Kim Poulsen toka timu ya U20, alisema habweteki wala kulewa sifa. "Siwezi kulewa sifa kwa mafanikio niliyonayo kwa kipindi kifupi, ndoto zangu nije kucheza soka la kulipwa Ulaya na kutamba kimataifa," alisema. LUNYAMILA Eddo, alizaliwa Septemba 10, 1992 mjini Tabora akiwa mtoto wa pili kati ya watatu kwa familia iliyolelewa na mama pekee. Elimu ya Msingi aliisoma Shule za Choma Chankola,Tabora na Mwele ya Morogoro, kabla ya kujiunga na Sekondari za St Francis na baadae Makongo. Kisoka alianza kutamba tangu akiwa darasa la tatu akiwa Morogoro, timu yake ya chandimu ikiwa ni Jamhuri Ball Boys na baadae Moro Kids iliyowakusanya baadhi ya nyota wanaotamba kwa sasa nchini. Alisema wakati akichipukia alivutiwa na baadhi ya nyota wa zamani wa Simba na Yanga kama Edibily Lunyamila, Salvatory Edward, Mark Sirengo na Nteze John wa Simba, huku akimtaja kocha Yahya Belini kama mtu aliyekigundua na kukiendeleza kipaji chake. Eddo alisema safari yake kisoka ilipata vikwazo vingi toka kwa mama yake aliyekuwa hapendi kabisa acheze, kiasi cha kumchapa, kumnyima chakula na hata kumfungia na kulala nje pale alipomkaidi na kujihusisha na soka. "Mama yangu aliyekwishafariki hakupenda nicheze soka, ila nilikuwa nunda na kuishia kulambwa bakora, kunyimwa chakula na hata kufungiwa mlango na kulala nje, ingawa sikukata tamaa," alisema. Alisema jambo zuri ni kwamba kabla mama yake hajafariki mwaka 2005 alishaanza kusikia sifa zake kisoka toka kwa shoga zake na kumuacha acheze hasa alipohamia Makongo jijini Dar es Salaam. Eddo, aliyedai hajaonana na baba yake mzazi tangu mwaka 1998 baada ya kutengana na marehemu mama yao, alisema roho inamuuma kuona mamaye akifa bila kula jasho lake kisoka. YANGA B Eddo, anayependa kula vyakula vyote na kunywa vinywaji laini, alisema safari yake kisoka alipohamia Dar aliwahi kuichezea Yanga B aliyokuja kuachana nayo baada ya kuona hawana muelekeo wowote wa kimaendeleo.maendeleo. Alisema alienda Yanga baada ya kuisaidia Kinondoni kutwaa ubingwa wa Copa Coca Cola mwaka 2007 na kisha kuifikisha timu ya Kinondoni katika fainali za Taifa na kulazwa na Ilala mabao 5-0. Alisema alipoachana na Yanga alirejea darasani katika Shule ya Lord Baden Powell kabla ya kutimkia Moro United B aliyoichezea kabla ya kutua Miundo Mbinu ya Lindi aliyoipandisha daraja la kwanza na kuichezea timu ya mkoa wa Lindi katika michuano ya Kombe la Taifa 2009. Alisema mara baada ya fainali hizo na Lindi kufungwa na Singida, ndipo aliponyakuliwa na Simba kung'ara nao akinyakua mataji na tuzo mbalimbali hadi kupandishwa katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo msimu uliopita. Eddo anayezishabikia Arsenal, Barcelona, Orlando Pirates na Brazil akiwazimia Neymar, Samuel Etoo na Ronaldo de Lima, alisema soka limempa mafanikio mengi kisoka na maisha ingawa hakupenda mambo yake yaanikwe. "Soka limenisaidia mengi, ila sipendi kila mtu ajue, najivunia na kiu yangu ni kung'ara zaidi nicheze soka la kulipwa Ulaya, safari yangu bado kabisa Simba sio mwisho wangu," alisema. Eddo ambaye hajaoa wala kuwa na mtoto, ingawa angependa kuwa na watoto watatu atakapooa, alitoa wito kwa wachezaji wenzake kujituma, kujiamini na kuwa na nidhamu waweze kufika mbali. Pia aliwakumbusha viongozi wa soka nchini kubadilika na kuachana na tabia ya kutumia nguvu na fedha nyingi kuwapapatikia 'mapro' wa kigeni na badala yake kuwekeza katika soka la vijana ili kulisaidia taifa hapo baadae. "Mafanikio ya kikosi cha Simba B ni funzo kwa viongozi na wadau wa soka nchini wawekeze katika soka la vijana badala ya kupigana kumbo kugombea mapro wa nje, fedha wazitumiapo kwao zisaidie soka la vijana," alisema. Eddo anayetamani kuwa mfanyabiashara mkubwa atakapostaafu soka na anayependa muziki wa reggae akimzimia J Booge, Biggy Signal na P Square, aliwashukuru mama yake, makocha wote waliomnoa na rafiki na wachezaji wenzake kwa kufika hapo alipo. Nyota huyo asiyeamini mambo ya uchawi katika soka akiamini mazoezi ndio kila kitu, alisema angekutana na Rais au waziri wa michezo angewaomba zijengwe na kuanzishwa shule maalum za michezo. pia kutaka soka la vijana lipewe kipaumbele zaidi. Mwisho

KIMOBITEL ALIVYOREJEA 'NYUMBANI' EXTRA BONGO

PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UTAMBULISHO WA KHADIJA MNOGA KIMOBITEL ALIPOREA BENDI YA EXTRA BONGO JANA JIJINI DAR ES SALAAM.

Mzee Yusuf aanzisha kampuni kusambaza kazi ili kudhibiti wezi

NYOTA wa muziki wa taarab nchini, Mzee Yusuf 'Mfalme' amefungua kampuni yake binafsi ya usambazaji wa kazi zake na wasanii wengine iitwayo MY Collection. Akizungumza na MICHARAZO, mkurugenzi huyo wa kundi la Jahazi Modern Taaran alisema ameamua kufungua kampuni hiyo ili kusaidia kuthibiti uchakachuaji na wizi wa kazi zake ambao umekuwa ukimkomesha mapato mengi. Alisema kampuni hiyo ambayo imeshafungua duka la kuuzia cd na dvd katika mitaa ya Likoma na Mhonda itakuwa ikihusika na usambazaji na uuzaji wa kazi za Jahazi Modern na zile za wasanii wengine iwapo watapenda kufanya hivyo kwake. "Katika kukabiliana na vitendo vya wizi wa kazi zangu, nimeamua kufungua kampuni ya usambazaji na uuzaji wa cd na dvd ambayo itahusika na kazi zote za Jahazi Modern, ila kama kutakuwa na watakaotaka kuwasaidia kusambaza kazi zao sitakuwa na noma," alisema. Naye Meneja Masoko wa kampuni hiyo, Mussa Msuba duka walillofungua litakuwa likihusika na kuuza kazi za taarab kwa jumla na rejereja ili kuwarahisishia mashabiki wa muziki huo eneo la kupata burudani hiyo. "Hili ni duka la awali tu, pnago ni kufungua karibu kila kona ya nchi kuwarahisishia mashabiki mahali pa kupata burudani za taarab kwa matumizi yao ya majumbani na ya kibiashara kwa ujumla na hasa kazi za Jahazi ambao wanatarajia kutoa albamu mpya ya tisa," alisema Msuba. Uamuzi wa Mzee Yusuf kufungua kampuni na duka hilo, imekuja mwezi mmoja baada ya kunasa baadhi ya albamu zake zilizochakachuliwa walipoendesha msako wakishirikiana na wadau wengine wa sanaa wakiwemo Shirikisho la Filamu Tanzania, TAFF na Bongo Movie.

Erick Mawalla: Kinda anayeililia ligi ya vijana, kombe la Taifa

KUTOKUWEPO kwa ligi ya muda mrefu na ya kudumu kwa timu za vijana na kutopewa kipaumbele kwa michuano ya Kombe la Taifa, kunamfanya beki kinda anayepanda chati nchini, Erick Mawalla 'Sekana' aamini ni sababu ya kudidimia kwa soka la Tanzania. Beki huyo aliyetua African Lyon akitokea timu iliyoshuka daraja ya Moro United anasema michuano ya timu za vijana na Kombe la Taifa kwa mtazamo wake ndio ukombozi wa soka la Tanzania na kurejesha makali yake katika anga la kimataifa. "Hatuwezi kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa iwapo hatuna ligi ya vijana, lazima iwepo mipango ya kuanzisha ligi hiyo na kuipa kipaumbele michuano ya Kombe la Taifa, ambayo siku za nyuma ilitumika kuibua nyota waliotamba nchini," anasema. Anasema hata klabu na mataifa yanayofanya vema katika soka la kimataifa, zilipoteza fedha zao kuwekeza kwa vijana na mavuno yao yanavutia kila mtu, kitu ambacho ametaka Tanzania nayo kufuata nyayo hizo ili ifanikiwe. "Bila kuwepo kwa ligi ya kudumu ya vijana, au shule maalum za kukuzia vipaji tangu utotoni na kutopewa kipaumbele kwa michuano muhimu kama Kombe la Taifa ni vigumu kuwa na timu imara kuanzia ngazi za klabu mpaka timu za taifa," anasema. Erick aliyeanza kucheza soka tangu shuleni kama winga kabla ya kubadilishwa na kuwa beki, anasema kuanzia serikali, wafadhili, viongozi na mashabiki watambue hakuna njia ya mkato ya mafanikio katika michezo bila watu kuwekeza fedha zao katika sekta hiyo. NYOTA NJEMA Kinda hilo, linalopenda kula chakula cha aina yoyote mradi akimdhuru na kunywa Juisi, anasema anashukuru soka kumsaidia kwa mengi ikiwamo kutwaa mataji na tuzo kadhaa tangu akiwa kinda ukiacha mafanikio binafsi ya kimaisha. "Siwezi kusema nimefanikiwa sana, ila nashukuru kwa muda mfupi niliopo katika soka nafarajika nimeweza kupata mafanikio ya kujivunia ikiwamo kutwaa vikombe, tuzo na kupata fedha zinazosaidia kuendesha maisha yangu," anasema. Erick, 'swahiba' mkubwa wa Mfungaji Bora wa michuano ya Super 8 anayeichezea Simba, Edward Christopher 'Eddo Boy', anasema moja ya mataji ambayo hawezi kusahau maishani mwake ni Kombe la Copa Coca Cola 2007 akiwa na timu ya vijana ya Kinondoni. "Hili ndilo lilikuwa taji langu la kwanza kubwa katika maisha ya soka, kwa hakika nilifurahi mno kuipa Kinondoni taji hilo, ingawa nimeshatwaa pia ubingwa wa Kombe la Taifa nikiwa na Ilala na mwaka jana tulishika nafasi ya tatu katika michuano kama hiyo," anasema. Erick, aliyeingia kwenye soka kwa kuvutiwa na 'mapacha' wa zamani wa klabu anayoishabikia ya Manchester United, Dwight Yorke na Andy Cole, anasema kabla ya kuibukia kwenye Coca Cola, kipaji chake kilianza kuonekana Kijitonyama Stars aliyoichezea tangu akiwa darasa la sita. "Baadae nilitua Yanga B nikiwa na swahiba wangu Eddo Boy na wengine, lakini kutokana na klabu hiyo kuonekana haikuwa na mipango endelevu ya soka la vijana, nilihamia Moro Utd B na kuichezea kwa misimu kadhaa akishuka na kupanda nayo Ligi Kuu," anasema. Chipukizi huyo anasema alikuwa katika kikosi cha Moro kilichoshuka daraja msimu wa 2009-2010 na kuirejesha tena Ligi Kuu msimu uliopita kabla ya kuzama tena na yeye kukimbilia African Lyon. Matarajio ya Erick anayeishabikia pia Real Madrid na aliyewataja makocha Juma Matokeo na Seleman Kiiza kama watu waliosaidia kukuza kipaji chake, ni kucheza soka la kulipwa nje ya nchi akidai tayari ameanza kipango ya jambo hilo. "Kiu yangu kubwa ni kucheza soka la kulipwa hasa Ulaya, naamini ni kipaji na uwezo wa kufanya hivyo, ingawa napenda kabla ya hapo nipate fursa ya kulitumikia taifa langu," anasema. Mchezaji huyo anasema licha ya kuitwa mara kadhaa katika vikosi vya timu za vijana U17 na U20, kiu yake kubwa ni kuichezea Taifa Stars. NSAJIGWA Erick anayehuzunishwa na kifo cha baba yake kilichotokea mwaka 2006, anasema licha ya kucheza mechi nyingi, pambano gumu kwake ni lile la Moro United dhidi ya Yanga lililochezwa msimu uliopita na lililoisha kwa sare ya mabao 2-2. Anasema anaikumbuka mechi hiyo hasa kwa tukio lililofanywa na aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa cha kumpiga 'kiwiko' winga wao Benedict Ngassa na kutolewa nje kwa kadi nyekundu na jinsi Yanga iliyosawazisha bao la pili. "Ni mechi hiyo na ile ya nusu fainali dhidi ya Mwanza katika michuano ya Kombe la Taifa 2011 tuliyopoteza ndizo ninazozikumbuka kwa ugumu na namna zilivyojaa upinzani," anasema. Erick Lawrance Mawalla alizaliwa Julai 5, 1993 jijini Dar es Salaam akiwa mtoto wa kwanza kati ya wanne wa familia yao, alisoma Shule ya Msingi Bunge kabla ya kutua Makongo Sekondari kutokana na kipaji chake cha soka. Akiwa Makongo ndiko alikoitwa timu ya vijana ya Kinondoni na baadae timu ya taifa ya U17 kabla ya kupandishwa ile ya U20 chini ya kocha Kim Poulsen. Anasema kama kuna watu anaowashukuru kumsaidia kufanikiwa kisoka na maisha basi si wengine zaidi ya wazazi, makocha wake na wachezaji wenzake bila kuusahau uongozi wa Moro United. Erick anayependa kusikiliza muziki na kuangalia filamu, anasema kama angekutana na Rais wau Waziri wa Michezo kilio chake kingekuwa juu ya kujengwa shule maalum za michezo.

Kimobiteli arejea Extra Bongo, atua na moja mpya

BENDI ya muziki wa dansi ya Extra Bongo imemrejesha kundini aliyekuwa muimbaji wao Khadija Mnoga 'Kimobitel' aliyekuwa ametimkia African Stars 'Twanga Pepeta'. Uongozi wa Extra Bongo ulisema umemrejesha kundini mwanamuziki huyo baada ya mwenyewe kuridhia kurudi huku bendi yao ikiwa ina upungufu mkubwa katika safu ya uimbaji kwa sauti ya kike. Mkurugenzi wa Extra, Ally Choki, alisema wakati wa kumtambulisha muimbaji huyo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa kurejea kwa Kimobitel kutasaidia kuimarisha safu yao ya uimbaji. Choki alisema Kimobitel aliyeikacha Extra Bongo miezi kadhaa iliyopita amerejea kundini akiwa na 'zawadi' kwa mashabiki kwa kuja na wimbo mpya uitwao 'Mgeni'. Mkurugenzi huyo alisema Extra Bongo inatarajiwa kumtambulisha rasmi Kimobiteli kwa mashabiki wiki ijayo baada ya kufanya mazoezi ya kutosha na wenzake. Kimobitel alisema amerejea Extra Bongo bila kulazimishwa na mtu huku akidai bendi aliyotoka hakuwa na mkataba wowote na hivyo anawaomba mashabiki wa bendi hiyo wampokee na watarajie mambo mazuri kutoka kwao. "Nimeamua mwenyewe kurejea Extra Bongo, na yale yaliyopita yamepita tuangalie mapya ninachoomba mashabiki wetu wasubiri vitu adimu toka kwangu," alisema. Mwanadada huyo aliyewahi kutamba na bendi mbalimbali ikiwemo African Revolution na Double M Sound, alisema anaamini aliwakwaza watu alipoondoka Extra Bongo, lakini ni suala la kusameheana kwani ametambua alipotoka na amerejea nyumbani akihitaji kupokelewa vema. Naye kiongozi wa bendi hiyo, Rogart Hegga 'Katapila' alisema wana Extra Bongo wamefurahishwa na ujio wa Kimobitel akidai bendi yao sasa imekamilika vya kutosha hasa baada ya kushindwa kuziba pengo la mwanamuziki huyo tangu alipoondoka. Alisema licha ya kwamba mwanamuziki huyo atatambulishwa rasmi wiki ijayo, lakini bendi yao itaendelea na maonyesho yao kama kawaida wiki hii kwa siku za Ijumaa na Jumapili kufanya vitu vyao White House-Kimara na Jumamosi Meeda Club, Sinza. Mara baada ya utambulisho wa mwanamuziki huyo kwa waandishi, alitambulishwa pia kwa wanamuziki wote wa Extra Bongo ambapo kwa kauli moja wanamuziki hao walimpokea na kumkaribisha nyumbani wakimuahidi ushirikiano ili bendi yao izidi kupaa.