|
Mwenyekiti wa Mtaa wa Kimara King'ongo, Bw Mapesi (kushoto) anayedaiwa kumuokoa mtoto na kijana aliyetaka kumchoma moto mtoto huyo kwa tuhuma za kuiba viatu. |
VITENDO vya watoto wadogo kufanyiwa vitendo vya kikatili vinazidi kushamiri katika jamii ambapo hivi karibuni mtoto mmoja wa miaka saba anayesoma Shule ya Msingi iliyopo Kimara King'ongo kata ya Saranga alinusurika kuuwawa kwa kuchomwa moto na kijana mmoja mshona viatu akimtuhumu mwizi.
Tukio hilo ambalo MICHARAZO imedokezwa lilitokea wiki mbili zilizopita majira ya mchana katika eneo la Kwa Komba, Kimara King'ongo baada ya mshona viatu huyo anayefahamika kwa jina na Ngosha kumpiga na kisha kumwagia dumu zima la mafuta ya taaa mtoto huyo kisha kumburuta hadi dukani ili anunue kiberiti cha kumwashia moto kabla ya wasamaria wema kuingilia kati na kumgeuzia kibao kijana huyo.
Inaelezwa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) siku moja kabla alienda kwa fundi huyo na kuviona viatu ambavyo alimuomba ampe akamuonyeshe baba yake ili aweze kumununu kutokana na kuvipenda na Ngosha alimpa bila hiyana akimtaka arejeshe mara baada ya kumaliza haja zake kwa baba yake.
Hata hivyo mmoja wa mashahuda wa tukio hilo alidai mara baada ya mtoto huyo kwenda na viatu hivyo kwa wazazi wake na kueleza shida na mahali alipovipata, baba yake alimchapa fimboa kimtaja kuvirejesha mahali alipovipata akiamini huenda kijana wake aliviiba.
Kwa kuwa ilishafika usiku, mtoto alilala na viatu na kesho aliamua kuvirejesha kwa Ngosha na kumueleza baba yake alimchapa akidhani ameviiba na ghafla kijana huyo (pengine kwa bhangi, anazoelezwa anavuta katika eneo lake la kazi) alimbadilikia kijana huyo na kuanza kumchapa makofi akidaia anawatafuta watoto wengi kama mtoto huyo.
Mtoto huyo aliamua kupiga kelele akijitetea yeye siyo mwizi, lakini Ngosha kama asiyemjua alimpiga tani yake kisha kuchukua dumu la mafuta ya taa alililokuwa nalo katika eneo lake la kazi na kumwagia kijana huyo mdogo bila huruma kisha kujisachi na kukuta hana kiberiti na kumburuta hadi kwenye duka lililokuwa jirani na eneo hilo la kituo cha mabasi cha Kwa Komba.
Hata hivyo baadhi ya waendesha pikipiki waliokuwa katika eneo hilo walioshuhudia tukio hilo na wasamaria wema wengine waliamua kuingilia kati na kumhoji Ngosha kwa nini anampiga mtoto na kutaka kumtenda alichokuwa amekusudia na bila aibu alisema anataka kumwasha mtoto mtoto huyo kwani mwizi.
Ndipo wasamaria wema na waendesha pikipiki hao waliamua kumgeuzia kibao kwa kumpiga kijana huyo kabla ya kuja kuokolewa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huyo aliyekuwa amembatana na Polisi na kuondoka na kijana huyo na mtoto aliyekuwa anachuruzika mafuta hadi kituo cha Kidogo cha Polisi cha Kimara.
"Huyo jamaa ni kama aliyechanganyikiwa, alimpa mwenyewe mtoto viatu kisha akamgeuzia kibao baada ya kusikia simulizi lake toka kwa wazazi wake, na kumwagia mafuta yaani kama tusingekuwepo mtoto wa watu angeteketea kibaya wazazi wake wote hakuwepo nyumbani," alisema dereva mmoja wa pikipiki Ally aliyeshuhudia tukio hilo mwanzo mwisho.
Ally alimwagia sifa Mwenyekiti huyo wa serikali ya Mitaa aliyemtaja kwa jina la Demetrius Mapesi, ambaye mbali na kumnusuru mtoto, lakini pia alisaidia Ngosha kufikishwa Polisi kwa usalama bila kudhurika kwani wananchi walutaka wamuunguze yeye wakidai wamemchoka kwa mambo yake yasiyoendana na ustaarabu.
"Kama siyo Mapesi, Ngosha angeiva yeye," alisema Ally.
MICHARAZO ilimpigia simu mwenyekiti huyo baada ya kupewa namba na dereva huyo, ambapo Mwenyekiti huyo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza liliishia Polisi Kimara ambapo mtuhumiwa huyo alifikishwa kwa ajili ya taratibu za kushtakiwa kwa kosa alilotaka kulifanya kwa mtoto huyo mdogo.
"Ni kweli tukio hilo lilitokea wiki mbili zilizopita na tulishamfikisha Ngosha mikononi mwa Polisi kwa taratibu za kufikishwa mahakamani, Ila ilitushtusha mno kijana mzima kaka yeye kumwagia mtoto mafuta ya taa na kutaka kumwasha moto kwa sababu ya viatu ambavyo inadaiwa alimpa mwenyewe," alisema Mapesi.
sikijana mmoja ambaye ni mshona viatu, maarufu kwa jina la Ngosha alikaribia kumlipua kwa moto mwanafunzi wa darasa la kwanza (jina kapuni) akimtuhumu alimuibia viatu.