|
Mabingwa watetezi wa Kagame, Yanga wakishangilia taji lao la mwaka jana |
MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Kagame, ambao pia ni mabingwa wapya wa soka nchini Tanzania, Yanga wametahadharishwa kufanya maandalizi ya kutosha iwapo wanataka kutetea taji la michuano hiyo ambaya kwa mwaka huu itafanyika nchini Sudan.
Yanga imepangwa kundi C pamoja na timu za Express ya Uganda, Vital'O ya Burundi na Port Djibout na itaanza kibarua chake siku mbili baada ya kuanza kwa michuano hiyo kwa kuumana na Express.
Kutokana na ugumu wa michuano hiyo itakayoanza Juni 18 hadi Julai 2, wanachama wa Yanga wameanza kutahadharisha mapema viongozi na wachezajiu wao kwamba wajiandae vyema kwa ajili ya kuzidi kuwapa raha katika ushiriki wao nchini Sudan.
Ramadhani Kampira, aliyewahi kuichezea timu hiyo na kuongoza Chama cha Soka wilaya ya Kinondoni (KIFA) alisema kwa kuiangalia michuano hiyo ya Sudan ni wazi itakuwa migumu, hivyo Yanga wanapaswa kujiandaa vyema na wachezaji kwenda 'kukaza' ili warejee Tanzania na taji.
Kampira alisema, yeye binafsi anaamini Yanga ina kikosi kuzuri kinachoweza kuwapoa raha, lakini bila kujipanga ni wazi inaweza kuwasononesha wanayanga ambao wanachekelea taji la 24 la Ligi Kuu Tanzania.
"Yanga wanapaswa kufanya maandalizi mazuri, tuna hamu ya kuona klabu yetu inatwaa taji kwa mara ya tatu mfululizo na kwa mara nyingine tena nje ya ardhi ya Tanzania baada ya mara mbili kunyakua Uganda," alisema.
Kampira, alisema tahadhari hiyo haipo kwa Yanga tu, bali hata kwa watani zao Simba ambao wana rekodi ya kunyakua taji hilo mara 6 pamoja na AFC Leopards ya Kenya kwa sababu nao ni wawakilishi wa Tanzania.
"Wawakilishi wetu wote wanapaswa kujipanga, wasitarajie mteremko Sudan, klabu zilizopo kwenye michuano hiyo siyo za kubeza nazo zinahitaji taji kama ambavyo Yanga na Simba zitakuwa zikilitamani,' alisema.
Jumla ya timu 13 zinatarajiwa kuchuana katika michuano hiyo ya kusaka Klabu Bingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo Simba wenyewe wamepangwa kundi A na timu za APR Rwanda, Elman ya Somalia na El Merreikh.
Kundi jingine la michuano hiyo ni lile la B lenye timu za Super Falcon ya Zanzibar, El Hilal na El Ahly Shandi za Sudan na Al Nasir Juba ya Sudan Kusini.