STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, September 16, 2013

Kivumbi cha Ligi ya Mabingwa Ulaya kuanza kesho, Moyes kuanza vipi?

Eti babu we ulikuwa unafanyaje mpaka ukatisha? Kama Moyes akimuuliza Sir Alex Ferguson

KIVUMBI cha Ligi ya Mabingwa wa Ulaya hatua ya makundi kinatarajiwa kuanza kesho, ambapo 'Mashetani Wekundu', Manchester United itaanza nyumbani dhidi ya Bayer Liverkusen ambapo mashabiki watataka kuona kocha David Moyes atavuna nini katika mechi yake ya kwanza katika michauno hiyo akiwa na Man Utd
Moyes aliyemrithi kocha mwenye mafanikio wa klabu hiyo aliyestaafu Mei mwaka huu, Sir Alex Ferguson atakuwa uwanja wa nyumbani wa Old Trafford, akiwa na kumbukumbu ya kukwama na Everton aliyokuwa akiinoakutinga hatua ya makundi msimu wa 2005-2006 baada ya kutolewa hatua ya mwisho wa mchujo kwa kung'olewa na Villarreal ya Hispania kwa jumla ya mabao 4-2.
Je, mbinu alizorithi toka kwa SAF zitamsaidia kuweza kufanya kweli kwenye kundi lake la A ambalo linaoonekana kuwa jepesi kulinganisha na mengine? Bila shaka ni suala la kusubiri kuona baada ya mechi hiyo ya kesho na nyingine za kundi lake lenye timu nyingine za Real Sociedad ya Hispania ambayo kesho pia itakuwa nyumbani kuialika Shakhtar Donetsk ya Ukraine.
Katika kivumbi hicho kesho pia itashuhudiwa mechi za makundi mengine matatu ya BC na Dna ratiba yake inaonyesha kuwa Galatasaray ya Uturuki itaumana na Real Madrid ambayo juzi ilimuongezea mkataba mpya nyota wake Cristiano Ronaldo na kumfanya awe mchezaji anayelipwa zaidi duniani, huku ikiwa na mchezaji ghali zaidi duniani kwa usajili Gareth Bale.
Pambano jingine la kundi B kwa kesho ni København  itakayoumana na Juventus, wakati mechi za kundi C itazikutanisha timu za Benfica ya Ureno dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji, huku Olympiakos Piraeus ya Ugiriki ikitarajiwa kuvaana na PSG ya Ufaransa.
Mabingwa watetezi, Bayern Munich ya Ujerumani yenyewe itaanza kibarua cha kutetea taji hilo iliyotwaa Mei mwaka huu kwa kuilaza Borussia Dotmund, nyumbani kuvaana na CSKA Moskva na Viktoria Plzeň itaialika Manchester City.
Keshokutwa Jumatano, kutakuwa na mechi nyingine za makundi manne yaliyosalia ambapo ratiba kamili ni kama ifuatavyo:
Schalke 04 vs Steaua BucharestChelsea   vs Basel
Olympique Marseille vs Arsenal
Napoli   vs Borussia Dortmund 
Austria Wien vs Porto
Atlético Madrid  vs Zenit
AC Milan vs Celtic
Barcelona  vs Ajax

Jeshi la Polisi Mbeya laonya mashabiki wa soka wenye vurugu


  RPC Mbeya, Diwani Athuman
 
JESHI la Polisi Mkoani Mbeya limewaonya mashabiki wa soka mkoani humo ambao Jumamosi walifanya vurugu kubwa na kusababisha kuutia doa mkoa huo katika medani ya soka.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo mkoani humo limewaonya mashabiki hao kuwa kama watgaendelea kufanya 'upuuzi' wao kama walivyofanya katika pambano kati ya Mbeya City na Yanga basi watakiona cha moto.
 Jeshi hilo limelaani vurugu hizo ikidai linauchafua mkoa wao na pia ni tishio kwa Mbeya kuweza kufungiwa na hivyo kuwanyima mashabiki wa kweli wa soka kushuhudia mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Taarifa rasmi ya jeshi hilo la Polisi iliyotiwa saini na ASP P Mhako kwa niaba ya RPC Diwani Athuman isome mwenyewe hapo chini;
--
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA  KAMISHINA MSAIDIZI WA POLISI DIWANI ATHUMANI ANAWATAKA MASHABIKI NA WAPENZI WA MPIRA WA MIGUU WAACHE VITENDO VYA KUFANYA VURUGU KATIKA MICHEZO ITAKAYOKUWA IKIFANYIKA KATIKA UWANJA WA KUMBUKUMBU YA SOKOINE NA MKOA KWA UJUMLA, KWANI VURUGU HIZO ZITASABABISHA MICHEZO HIYO KUHAMISHIWA SEHEMU NYINGINE NA WAPENZI KUKOSA BURUDANI  PIA WANANCHI KUKOSA KIPATO, HIVYO KUUTANGAZA MKOA WETU VIBAYA. 
 
VURUGU ZILIZOTOKEA JUMAMOSI TAREHE 14/09/2013 KWA MASHABIKI KULISHAMBULIA GARI LA VIONGOZI WA TIMU YA YANGA LILILOKUWA LIMEPAKI NJE YA UWANJA PIA KULISHAMBULIA KWA MAWE GARI LILILOKUWA LIMEBEBA WACHEZAJI WA TIMU YA YANGA NA KUHARIBU KIOO CHA MLANGO WA DEREVA NA KUFANYA MAANDAMANO AMBAYO YAMESABABISHA USUMBUFU KWA WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA SI CHA KIUNGWANA NA KISIJIRUDIE TENA KATIKA MICHEZO MINGINE.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA HAKURIDHISHWA NA VITENDO HIVYO NA KUWATAKA MASHABIKI NA WAPENZI WA MPIRA WA MIGUU KUWABAINI NA KUWATAMBUA  WALE WOTE WATAKAOFANYA VURUGU NA KULIJULISHA JESHI LA POLISI.

AIDHA JESHI LA POLISI HALITAVUMILIA VITENDO HIVYO NA KWA YEYOTE ATAKAYE/WATAKAO BAINIKA HATUA KALI ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA ZIDI YAKE/YAO.

Signed by:
[P.A MHAKO – ASP]
Kny: KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Vijana wa Airtel Rising Stars wakabidhiwa bendera

 Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akimkabizi bendera ya Taifa,kapteni wa timu ya vijana ya wasichana wa Artel Rising Stars,Stumai Abdallah timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.
 Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akimkabizi bendera ya Taifa,kapteni wa timu ya vijana ya wanaume wa Artel Rising Stars,Athanas Shindeka timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania,Angetile Osia (kushoto) akikabizi bendera ya Taifa,kwa timu za vijana za wasichana na wanaume wa Artel Rising Stars ,timu hiyo inaondoka leo kuelekea Nigeria kushiriki mashindano ya Afrika ya Airtel Rising Stars.

Wamalawi wamiminika uhamiaji kujiandikisha zoezi la utambuzi wa wahamiaji haramu

Raia wa Malawi wakijiandikisha katika Idara ya Uhamiaji, Mkoa wa Dar es Salaam leo kuhusu zoezi linaloendelea la kuwatambua wahamiaji haramu jijini Dar es Salaam. (Picha zote na Felix Mwagara, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi).


Baadhi ya raia wa Malawi wakiwa katika foleni ya kujiandisha leo kwenye ofisi za uhamiaji jijini Dar es salaam 
Zoezi la utambuaji ya wahamiaji  haramu likiendelea wahamiaji wakiwa katika ofisi ya uhamiaji leo jijini Dar es salaam

Ivory Coast vs Senegal, Ghana dhidi ya Misri Top 10 WC Afrika


SHIRIKISHO la Soka Afrika, CAF limetangaza ratiba ya mchujo wa mwisho kwa timu za nchi za Afrika kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia za mwakani ambapo vinara wa kandanda Afrika na wababe wa Tanzania, Ivory Coast imepangwa kuanzia nyumbani dhidi ya majirani zao Senegal.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo ya CAF ni kwamba mechi za kwanza zitachezwa Oktoba 10 na zile za mwisho zitakazoa wawakilishi watano wa Afrika watakaoenda Brazil zitachezwa Novemba 14 mwaka huu.
Wakati Ivory Coast walionyakua nafasi ya kwanza katika kundi C lililokuwa na timu za Morocco, Tanzania na Gambia ikipangwa na Senegal iliyoiengua Uganda wiki iliyopita, wawakilishi wa ukanda wa CECAFA, Ethiopia yenyewe imepangwa na Nigeria na itaanza kibarua chake nyumbani mjini Addis Ababa.
Mechi nyingine itakzikutanisha Tunisia dhidi ya Cameroon, huku Burkina Faso kuumana na Algeria na Ghana watavaana na Misri.

Hawa ndiyo warembo walioingia Top 5 ya Redd's Miss Tanzania 2013

Warembo watano waliofanikiwa kuingia hatua ya nusu fainali ya Redd’s Miss Tanzania 2013 wakiwa katika picha ya pamoja jana. Kutoka kushoto  ni Miss Tanzania Photogenic 2013, Happiness Watimanywa, Miss Tanzania Talent 2013, Prisca Clement, Miss Tanzania Personality, Severina Lwinga, Miss Tanzania Top Model 2013, Narietha Boniface na Miss Tanzania Sports Woman, Clara Bayo. (Na Mpigapicha Wetu). 

Hafsa Kizinja amuenzi Mzee Gurumo kiaina

 Malkia wa Zouk nchini Hafsa Kazinja akiwa na Omari Mkali (kushoto) na Abdul Salvador baada ya kukamilisha kurekodi wimbo wa 'NIMUOKEOE NANI' katika Studio za OM Productions jijini Dar es salaam wikiendi hii.
Omary Mkali akiwa katika pozi la picha na Hafsa.
Hafsa Kazinje akiwa Studio.

DAR ES SALAAM, Tanzania
Baada ya ukimya wa muda mrefu,   Malkia wa Zouk Tanzania,  Hafsa Kazinja,  anaibuka upya katika fani akiwa na ingizo lake la kwanza kati  ya kumi aliyoandaa kwa kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI”  anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.

Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi ulingoni kwa kutoa wimbo huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi mbalimbali tokea mwaka wa 1960.

“Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE NANI” ili  kumuenzi gwiji huyu wa muziki kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha Banana Zorro.

Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE NANI” katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.
“Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE NANI nimeuimba baada ya kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee Gurumo mwenyewe.

“Haikuwa rahisi kama inavyoweza kudhaniwa kwani baada ya kwenda kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa kuuimba wote kabla ya kuridhika maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake unaimbwa hovyo hovyo na kuharibiwa radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga kwa mara ingine.

Hafsa anasema katika ukimya wake amekuwa akifanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata mawaidha maridhawa toka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.

Msanii huyu wa kizazi kipya anasema ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

“Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa wingi kwenye tamasha hilo name naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI” hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya.

Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa mmoja wa waanzilishi wa  bendi ya TANCUT ALMASI YA Iringa iliyotamba na mtindo wake wa “FIMBO LUGODA”, anamtaja Hafsa kazinja mmoja wa wanamuziki wa kike waliojaaliwa sauti nzuri na kipaji cha hali ya juu hapa nchini.

“Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo na kupatia kisawasawa inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa maana si mchezo kuimba nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama alivyofanya Hafsa.
“Na hii inadhihirisha kwamba uwezekano wa kizazi kipya na cha zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na sioni kwa nini isiwe hivyo”, anasema Salvador.

Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya CHUCHU SOUNDS, chini ya marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja kama moja ya majembe ya muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba anaweza kufika mbali endapo kama moto aliokuja nao upya atauendeleza.

IMETOLEWA NA
OM PRODUCTIONS NA HISIA SOUNDS