Waimbaji Shaaban Dede na Juma Kitundu |
Wapuliza tarumbeta |
Kizazi kipya! Hassani Moshi Tx Junior', Eddo Sanga na Katundu wakifanya mambo |
Msondo, ambayo ipo studio tangu katikati ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani, imesharekodi nyimbo zote isipokuwa kwa sasa zinasubiri nyimbo hizo kufanyiwa 'mixing' na kuahiriwa ili kuikamilisha albamu hiyo itakayokuwa na nyimbo sita.
Msemaji wa Msondo Ngoma, Rajabu Mhamila 'Super D' alisema mashabiki wao waanze kujiandaa kusuuza roho zao baada ya kipindi kirefu cha ukimya wa kutolewa albamu mpya kwa sababu wamesalia hatua chache kukamilisha albamu yao ya 'Suluhu'.
Super D, alisema nyimbo zote tano za kukamilisha albamu hizo zimesharekodiwa katika studio zilizopo Mbagala nje kidogo ya jijini Dar es Salaam na wanasubiri kuchanganywa vionjo vyake kabla ya kukabidhiwa rasmi ili mashabiki wao waanze kupata burudani.
"Albamu yetu kwa 'Suluhu' bado kidogo kutoka hadharani, kwani tumesharekodi nyimbo zote isipokuwa zinasubiriwa kufanyiwa 'mixing' kabla ya kuhaririwa na kukabidhiwa rasmi," alisema.
Baadhi ya nyimbo zilizorekodiwa na zitakazokuwa katika albamu hiyo mpya ni 'Nadhiri ya Mapenzi' wa Juma Katundu, 'Lipi Jema' na 'Baba Kibebe' za Eddo Sanga, 'Kwa Mjomba Hakuna Mirathi' wa Huruka Uvuruge, 'Machimbo' na 'Suluhu' wa nyota Shaaban Dede 'Super Motisha'.
Bendi hiyo yenye umri wa zaidi ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake kwa zaidi ya miaka miwili sasa haijatoa albamu mpya tangu ilipotoa albamu ya mwisho mwaka 2010 iliyofahamika kwa jina la 'Huna Shukrani'.