STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 22, 2013

Niyonzima 'atikisa' kiberiti Jangwani


Haruna Niyonzima
KIUNGO wa kimataifa wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kuwa atakuwa tayari kusaini mkataba mpya wa kuichezea Yanga katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara endapo watampa dola za Marekani 150,000 (Sh. milioni 240).
Mkataba wa Niyonzima aliyejiunga na Yanga mwaka juzi akitokea APR ya Rwanda unamalizika mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka kwao Kigali, Rwanda ambako amekwenda kuitumikia nchi yake inayokabiliwa na mechi dhidi ya Mali Jumapili, Niyonzima, alisema hataki kurudia makosa aliyofanya mwaka jana.
Niyonzima alisema anaamini kuwa hicho kiwango cha fedha ndiyo dau lake kwa sasa au zaidi na ameamua kuwaambia Yanga kutokana na hatua yao ya kukataa kumruhusu mwaka jana kujiunga na El Mereikh ya Sudan iliyokuwa imekubali kumlipa kiasi hicho.
Kiungo huyo ambaye ni nahodha wa timu ya taifa lake (Amavubi), aliongeza kuwa hivi sasa kazi ya kuzungumzia mkataba wake itafanywa na wakala wake.
"Mambo nahitaji yafanyiwe kazi kabla sijaamua kuendelea kubaki Yanga, ikiwamo kuongezewa mshahara,'' alisema Niyonzima.
Kiungo huyo kipenzi cha mashabiki wa Yanga aliongeza kuwa hataki kupoteza nafasi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma wakati alipokuwa akiichezea APR ambao hawakuwa tayari kumruhusu kirahisi kuondoka ndani ya timu hiyo inayotetea ubingwa wake wa ligi Kuu ya Rwanda.
Akizungumzia matakwa hayo ya Niyonzima, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed, alisema jana kuwa wako katika mipango ya kuwapa mikataba mipya wachezaji wao wote wanaowahitaji kuendelea kuwa nao kabla ya kumalizika kwa ligi.
Hata hivyo, Ahmed alisema hawawezi kusema ni lini watakamilisha kazi hiyo kwani hiyo ni mipango ya viongozi wa klabu kwa kushirikiana na benchi kao la ufundi.
Niyonzima na Mrisho Ngassa wa Simba waliivutia El Mereikh baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyofanyika mwaka jana nchini Uganda lakini Ngassa aliamua kuikacha timu hiyo kwa madai kwamba anazingatia maslahi yake na siyo kukimbilia kucheza nje. Nafasi ya nyota hao ilichukuliwa na Selemani Ndikumana kutoka Interclub ya Burundi.


CHANZO:NIPASHE.

Rais Kikwete azindua Complex ya Azam na kuzipiga 'dongo' Simba, Yanga


 Rais Jakaya Kikwete akizindua rasmi Jiwe la Msingi wa Uwanja wa Azam Complex. (Picha na Habari Mseto Blog)
Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye Uwanja mwingine wa Azam ambao bado upo kwenye matengenezo
 Rais Jakaya Kikwete akikata utepe,wakati wa uzinduzi rasmi wa uwanja wa Azam Complex.
 Rais Jakaya Kikwete akiwapungia mkono  mashabiki wa Azam waliokuja kushuhudia uzinduzi rasmi wa uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi uwanja huo.
 Rais Jakaya Kikwete,akiwa kwenye chumba cha kufanyia mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi.
 Rais Jakaya Kikwete,akiwa kwenye chumba cha kufanyia mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex,baada ya kuuzindua rasmi.
Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye Uwanja mwingine wa Azam ambao bado upo kwenye matengenezo.
 
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipigwa na butwaa baada ya kufika katika makao makuu ya klabu ya Azam yaliyopo Mbande jijini Dar es Salaam jana na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kujenga miundombinu ya kisasa ya timu hiyo.
Rais Kikwete ambaye alikuwa amefuatana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, mkewe Mama Salma Kikwete na viongozi mbalimbali wa serikali, aliweka jiwe la msingi kuashiria kuzinduliwa rasmi kwa uwanja wa klabu hiyo wa uitwao Azam Complex, kisha akatembezwa kuiona miradi mbalimbali ya wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobaki mwaka huu katika michuano ya klabu ya Afrika.
Akizungumza baada ya kuzindua uwanja huo na kuona utekelezaji wa mipango ya Azam ikiwamo ya kulea vijana wenye vipaji vya soka, rais Kikwete aliupongeza uongozi wa klabu hiyo na kuzipa changamoto klabu kongwe za Simba na Yanga kujifunza kutoka kwao.
Kikwete pia aliipongeza Azam kwa kuwa timu pekee ya Tanzania iliyobakik katika michuano ya kimataifa baada ya Simba na Jamhuri kutolewa katika hatua ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika huku timu hiyo iliyokamata mnafasi ya pili msimu uliopita ikifuzu kwa raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
"Azam wamekuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza soka nchini na timu yao sasa ni timu kigogo. Simba na Yanga sasa wanalazimika kujipanga zaidi wanapocheza na timu hii," alisema Kikwete.Akieleza zaidi kuhusu Simba Yanga, rais Kikwete alisema kuwa licha ya kuwa 'mnazi' wa mojawapo miaka iliyopita, klabu hizo zinakabiliwa na matatizo mengi yakiwamo ya tuhuma za ushindi wa kununua, imani za kishirikiana na kukosa viongozi makini.
"Klabu hii (Azam) haina wanachama wengi kama baadhi ya klabu nyingine ambazo wanachama wake wanagombana kila kukicha. Viongozi wa Azam msibweteke kama hawa jamaa kwa kutegemea kamati za ufundi (ushirikina)… hakuna uchawi katika mpira. Kama uchawi ungelikuwa unacheza mpira, Afrika tungelikuwa tumeshatwaa Kombe la Dunia. Ni upuuzi kuwekeza kwenye kamati za ufundi," alisema Kikwete.
"Wapo watu wanawekeza kwenye kusajili wachezaji kila mwaka. Ukifuatilia vizuri, wachezaji wanasajiliwa si kwa sababu wanahitajika, bali wasichukuliwe na timu nyingine, mpira hauko hivyo. Wekeza kwa vijana kwa kuhakikisha wanakula na kulala vizuri. Unakuta kiongozi hajui mchezaji anakula nini na analala wapi.
"Timu hii (Azam) inaendeshwa bila kutegemea wanachama wanaokimbilia kupiga kura kwa kuhongwa. Itakuwa timu kubwa sana, labda mshindwe wenyewe kwa kuamua kutumiwa. Mkikubali kuwa kivuli cha timu yoyote ili kuisaidia, mtashindwa."
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni za Bakhresa (SBB) wanaomiliki Azam, Aboubakar Bakhresa, alimshukuru rais kwa kukubali kushiriki uzinduzi wa uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 7,000.
Alisema imewagharimu Sh. milioni 800 kulinunua eneo walilojenga uwanja huo, ofisi na hosteli za wachezaji na kwamba awamu ya kwanza ya ujenzi wa miundombinu hiyo tayari imeshawagharimu takriban Sh. bilioni tatu.
Azam ilianzishwa mwaka 2004 ikiwa na muungano wa timu za viwanda vitatu vya SSB. 2005 ilipanda dara la tatu, daraja la pili (2006), la kwanza (2007) na ilitinga Ligi Kuu ya Tanzania Bara 2008.
Hivi sasa, Azam ambayo haijawahi kushuka daraja tangu ipande ligi kuu, inakamata nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ikiwa na pointi 37 baada ya kucheza mechi 19, pointi 11 nyuma ya vinara Yanga walioshuka dimbani mara 20.
Novemba mwaka jana, mshindi mara tatu wa zamani wa tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika, Abedi Pele alipigwa butwaa pia alipofika Mbande na kukiri kuwa amevutiwa mno na jitihada za klabu hiyo katika kukuza soka la vijana.