Jaji Mark Boman akizungumza mchana wa leo jijini Dar es Salaam |
Na Suleima Msuya.
WAKATI Taifa likiwa katika
mjadala juu ya rasimu ya katiba ijayo Mwanasheria Mkuu Mstaafu wa Serikali,
Jaji Mark Boman ameipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Mstaafu
Joseph Warioba kwa kuja na rasimu nzuri na kuitaka kutoharakisha uwepo wa
katiba husika ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi.
Jaji Boman amesema
hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya
habari maelezo Jijini hapa.
Alisema mchakato
mzima wa kuandaa rasimu unahitaji umakini, uadilifu na kuhakikisha kuwa hakuna
misukumo yoyote ya kufanikisha suala hilo hivyo ni vyema wakahakikisha kuwa
mambo ya msingi yanayohusu jamii yanahusika.
Mwanasheria Mkuu
huyo Mstaafu alisema jambo ambalo linaonekana kugusa jamii kwa asilimia kubwa
ni kuhusu muungano, hivyo ni vyema tume ikafanya tathmini sahihi juu ya
utekelezaji wake ili kuhakikisha kuwa inakidhi kiu ya Watanzania.
Alisema kutokana na
rasimu hiyo ilivyochambuliwa na tume imejikita hasa kuhusu jinsi ya kuwa na
muungano wa nchi lakini ikajisahau kuwa ilikuwa ni fursa muhimu kwa wananchi
kuhusika moja kwa moja juu ya aina ya muungano wanaotaka na isiwe na maoni ya
wajumbe wa tume.
"Mimi kama
Mtanzania na pia mwanasheria mkongwe ambaye najua masuala ya nchi hii kwa upana
naamini tume imejitahidi kwa kiwango chake ila naona haipo sababu ya kukimbilia
kuwepo kwa katiba bila kuhakikisha kuwa mahitaji ya msingi hajatekelezwa hasa
ambayo yanagusa jamii," alisema.
Jaji Boman alisema
suala la muungano linahitaji mchango wa wadau hasa wananchi kwani ni jambo
ambalo linaweza kuweka muafaka wa hatma ya nchi kwa miaka ijayo.
Alisema ni vema
Tume ikatambua kuwa suala la muungano halihitaji maoni ya watu wachache kwani
ni wazi kuwa suala hilo limekuwa likiibua migogoro mingi kwa muda mrefu hasa
katika upande wa Zanzibar.
Alisisitiza kuwa
katika harakati za kutafua ufumbuzi juu ya sauala hilo la muungano ni vema tume
ikachukua maoni ya waliowengi ili kuhakikisha kuwa haja yao inatimia hata kama
wachache wenye uelewa watakuwa wanapinga.
Boman alisema dhana
kuhusu serikali tatu kuwa zitaongeza gharama za undeshaji wa Serikali ni
mtazamo finyu kwani kuna mifano ya nchi nyingi ambazo zimeungana na kuendeshwa
kwa mfumo huo na hakuna athari ya moja kwa moja ambayo imeonekana.
Alisema ni vyema
tume ikajikita kwa wananchi na kuachana na mitazamo ya baadhi ya viongozi wa
kisiasa ambao wengine wanaonekana kuwa yapo mambo ambayo wanataka yawepo kwa
maslahi yao na sio ya Taifa
Kwa upande mwingine
Jaji Boman ameiomba tume kuhakikisha kuwa rasimu hiyo ya katiba ya nchi inakuwa
na muongozo juu ya dira ya nchi, maslahi ya kijamii kwa jamii na mahitaji
muhimu yatajwe ili iwe ni muongozo sahihi kwa kiongozi yoyote ambaye atapata
kuongoza nchi.
Pia alisema ni
vyema rasimu hiyo ya katiba ianishe uwepo na uatambuzi wa rasilimali za nchi
ambazo kwa kiasi fulani zimeonekana kutumiwa kinyume na taratibu hivyo
kutowafaidisha wananchi kwa ujumla.
Alitolea mfano
suala la mikataba mibovu ambayo imekuwa ikiingiwa na Serikali iwapo kutakuwepo
na muungozo wa kikatiba juu ya suala la mikataba inaweza kuwa njia sahihi ya
kuwabana wahusika.
Alisema iwapo mambo
hayo ya msingi yakikosekana ni dhahiri kuwa kila kiongozi anaweza kufanya
anachotaka kutokana na mahitaji yake jambo ambalo ni kinyume na utawala
unavyotaka hasa katika ngazi ya nchi.