STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 1, 2013

AZAM INA KILA SABABU ZA KUSHINDA MOROCCO

Khamis Mcha 'Vialli' nyota wa Azam katika pambano lao dhidi ya As Far Rabat jijini Dar na kuisha kwa 0-0

Kikosi Tegemeo cha Azam

Azam wakijifua mjini Rabat

Wachezaji wa Azam, walipokuwa wakijiandaa na pambano lao dhidi ya BYCII

Na Patrick Kahemela, Rabat
KIKOSI cha timu ya Azam Fc ipo mjini Rabat ikijiandaa kukabiliana na AS FAR kwenye mechi ya raundi ya mwisho ya 16 bora za kombe la shirikisho. Azam FC imetua hapa na wachezaji 23, benchi lote la ufundi isipokuwa Ibrahim shikanda pekee aliye masomoni Nairobi na uongozi karibu wote na kwa pamoja kama timu Azam FC ina dhamira ya kuifunga na kuisukuma nje ya mashindano timu ya AS FAR.
Kuna sababu sita zinazoifanya Azam FC iamini na ijiamini kuwa inaweza kushinda kwenye mtanange wa jumamosi hii. Sababu hizo ni maandalizi bora, wachezaji wazuri, Uongozi Mzuri, benchi bora la ufundi chini ya Stewart Hall, Mipango mizuri na dhamira ya kupata mafanikio. Makala hii itakayowajia katika sehemu tatu itachambua vipengele vilivyoaninishwa hapa chini.
MAANDALIZI MAZURI
Timu za Tanzania kwa miaka mingi zimekuwa zikishiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF, kwa Azam FC hii ni mara yake ya kwanza kupata nafasi hii. Lakini unaweza kuona utofauti mkubwa wa maandalizi kati ya Azam FC na timu nyingi za Tanzania na utofauti huo ndiyo unaoifanya Azam FC hadi sasa kuweza kucheza mechi tano pasi na kupoteza mchezo hata mmoja.
Azam FC baada ya kujua kuwa itawakilisha nchi kwenye mashindano ya kimataifa iliamua kufanya juhudi za makusudi za kujiandaa kwa kiwango cha mashindano hayo yanayoandaliwa na CAF.
Azam FC ilifanya ziara na kucheza mechi nane za kimataifa za kirafiki nje ya ardhi ya Tanzania, ilikwenda Kinshasa Congo DRC na kushiriki Congo Charity Cup ambako ilitwaa kikombe kabla ya kusafiri tena hadi Nairobi ambako ilipata nafasi ya kucheza mechi nyingine tatu.
Lengo la ziara hizi ilikuwa ni kuwapa ukomavu na uzoefu vijana wake ili wanapokuwa kwenye mashindano ya CAF hasa wanapocheza mechi za ugenini wasiwe na hofu. Hakika matunda ya ziara hizi tunayaona kwani Azam FC imeshinda ugenini mechi zake zote mbili za awali hadi sasa.
Maadalizi ya Azam FC kwenye mashindano haya pia yalihusisha utafutwaji na usajili wa wachezaji wenye viwango vya kuweza kucheza na kuisaidia timu, uboreshwaji wa kambi ya mazoezi ya Chamazi mapema kwa ajili ya kambi ya nyumbani, ununuzi wa vifaa bora vya mazoezi na kadhalika.
UWEZO WA WACHEZAJI
Timu ni wachezaji, bila ya wachezaji bora wenye nidhamu, viwango bora na malengo ni sawa na bure. Azam FC ililitambua hilo mapema… Azam FC haikukurupuka kusaka wachezaji kwa mkupuo, usajili wa wachezaji kwa ajili ya mashindano ya CAF ulifanyika kwa umakini kwa muda mrefu huku klabu ikijiwekea malengo ya kuwa na kikosi bora kitakochoweza kupambana na kuvifunga vigogo vya soka la Afrika.
Leo ukiwaangalia wachezaji 25 wa Azam FC waliosajiliwa kwenye mashindano ya CAF utaungana nami kuwa ni wachezaji sahihi kwa mashindano haya.
Wachezaji wa Azam FC wana nidhamu na vipaji vya hali ya juu. Wote wana viwango vya kuweza kuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania na kuanza kwenye kikosi cha kwanza. Hapa nitazungumzia sifa za wachezaji wa eneo la ulinzi tuu kwa ufupi… halafu muendelezo wa makala hii utawaletea wachezaji wa kiungo na baadaye washambuliaji.
MWADINI ALLY; Golikipa chaguo la kwanza la kikosi cha timu ya Taifa ya Zanzibar na sehemu ya kudumu ya kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania. Ana uzoefu mkubwa wa michezo ya kimataifa akiiongoza Zanzibar kushika nafasi ya tatu mara mbili kwenye mashindano ya CECAFA. Ni golikipa hodari ambaye Azam FC tunajivunia kuwa naye
AISHI MANULA, utasemaje juu ya kipaji cha kijana huyu toka Morogoro? Wengi wanamfananisha na golikipa wa zamani wa Tanzania na Simba Mohammed Mwameja. Aishi anajiamini, ana umbo zuri na kipaji kikubwa sana. Ndiyo maana haishangazi kwa nini yeye ni golikipa namba moja wa timu za vijana za taifa na chaguo namba tatu la Taifa Stars ya kocha Kim Poulsen
HIMID MAO; Ana miaka 20 tuu lakini ni mkongwe ndani ya kikosi cha Azam FC, Himid ni kiungo mwenye sifa za kukaba ambaye sasa anacheza kama beki wa kulia wa Azam FC. Hakuna aliyeshangaa jina lake lilipoitwa na Kim Poulsen kuwa sehemu ya wachezaji 30 bora nchini wanaonyemelea nafasi za walio timu ya Taifa. Himid Mao aliibukia kwenye mashindano ya Copa Cocacola na baadaye kuwa nahonda wa timu za taifa za Tanzania chini ya miaka 20. Kabla ya mwalimu wa wakati huo wa Azam FC Itamar Amorim kumpa nafasi kwenye kikosi cha kwanza akitokea Azam Academy. Himid anafanya vizuri sana kwenye kikosi cha Azam FC hadi sasa.
WAZIRI SALUM; huenda ndiye mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha kumiliki mpira kuliko wachezaji wote nchini Tanzania kwa sasa. Waziri Salum, naye yumo kwenye daftari la kocha Kim Poulsen na ni mwanachama wa kudumu wa kikosi cha Zanzibar heroes. Mguu wake wa kushoto ni kama mkono wa paka kwani anaweza kufanya lolote na mpita kwa kutumia mguu huu. Ana mbinu za kukaba, ana krosi za hatari na chenga za maudhi. Ni hadhina kubwa kwa Azam FC na taifa la Tanzania
JOCKINS ATUDO; beki bora wa ligi kuu ya Kenya KPL msimu uliopita Jockins Atudo alitua Azam FC wakati wa dirisha dogo la Disemba mwaka jana ili kuimarisha ukuta wa Azam FC kwa ajili ya mashindano haya. Tangia atue Azam FC Atudo amethibitisha kuwa waliomchagua kuwa beki bora hawakukosea. Kocha wa zamani wa Harambee Stars James Nandwa alisema wakati tunataka maoni yake juu ya atudo kabla ya kumsajili kuwa ukiwa na beki kama Atudo unapata vitu viwili, kwanza uongozi ndani ya uwanja pili beki mwenye kipaji, nguvu, kimo na kujitolea… hakika kila kocha angependa kuwa na Atudo kwenye kikosi chake
LUCKSON KAKOLAKI; labda ndiye mchezaji mwenye busara zaidi kwenye kikosi cha Azam FC kiasi kwamba wachezaji wenzake wanamuheshimu na kumkubali kama kaka. Busara hizi za nje ya uwanja pia unaweza kuziona ndani ya uwanja mbapo Luckson amekuwa mhimili mkuu kwa Azam FC hasa pale eneo la ulinzi linapokabiliwa na majeruhi. Kiwango chake cha uchezaji kimekuwa cha uhakika wakati wote na hili alilithibitisha kwenye mechi ya awali dhidi ya AS FAR ambapo aliingia katika dakika ya sita baada ya Atudo kuumia na kucheza kwa ustadi mkubwa sana Luckson ni mchezaji mmoja wapo ambaye tunaweza kusema ana damu ya bluu (yaani ana damu yenye rangi ya Azam FC)
DAVID MWANTIKA; Tanzania tumejaaliwa kuwa na mabeki wazuri lakini hatujawahi kuwana beki wa kiwango cha David Mwantika tangia kuondoka kwenye ramani ya soka kwa Boniface Pawasa. Mwantika hapitiki kwa namna yoyote ile… Mwantika ana nguvu za asili na mwili uliojengeka. Wenyewe wanyakyusa wanamuita Bedui… Mwantika ana spidi ya upepo na amekuwa maarufu ndani ya wachezaji wa Tanzania lakini alikuwa na umaarufu mdogo nje kutokana na timu yake ya Prisons kutopewa nafasi sana na vyombo vya habari. Lakini ukikutana na washambuliaji wa ligi kuu watakuambia kuwa beki wanayemuogopa zaidi nchini ni David. Juzi kim Poulsen amemjumuisha kwenye kikosi chake na bila shaka wala wasiwasi Mwantika atavuka kwenye kikosi cha Young taifa Stars na kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars muda si mrefu
Katika makala zijazo, tutawaletea maelezo ya wachezaji waliosalia wa kiungo na ushambuliaji pamoja na sababu nyingine nne zilizosalia za kwa nini Azam FC itaifunga AS FAR ambazo ni UONGOZI BORA, BENCHI BORA LA UFUNDI, MIPANGO MIZURI, na DHAMIRA

Coastal yaibana Yanga, Lyon byebye VPL

Yanga iliyobanwa uwanja wa Taifa

maafande wa JKT Oljoro waliolazikisha suluhu kwa Ruvu Shooting

Coastal waliochelewesha sherehe za ubingwa za Yanga

Afican Lyon iliyoshuka rasmi Ligi Kuu baada ya kunyukwa na Mtibwa Sugar Manungu
WAKATI Mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga wakishikwa kwenye uwanja wa Taifa na Coastal Union ya Tanga kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1, African Lyon imezama rasmi Ligi Daraja la Kwanza baada ya kulazwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.
Yanga ambayo inakamilisha tu ratiba ya ligi hiyo baada ya Ijumaa iliyopita kutawazwa mabingwa baadaya Azam kung'ang'aniwa na Coastal na kyutoka sare ya 1-1, ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia Jerry Tegete kabla ya Coastal kusawazisha dakika chache baadaye kupitia kwa Abdi Banda na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa nguvu sawa hali iliyoendelea hadi dakika 90 zilipoisha na hivyo kugawana pointi moja moja na Yanga kufikisha pointi 57 na Coastal 35.
Katika mechi nyingine iliyochezwa uwanja wa Chamazi, JKT Ruvu walijikuta wakizama kwa kulazwa mabao 2-1 na Prisons ya Mbeya, huku uiwanja wa Mabatini Mlandizi wenyeji Ruvu Shooting walibanwa na JKT Oljoro kwa kutofungana.
African Lyon inayoburuza mkia ilijihakikishia kucheza Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao kwa kutunguliwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar katika pambano jingine lililochezwa uwanja wa Manungu, mjini Turiani. Mabao yoye ya washindi yakiwekwa kimiani na mshambuliaji nyota Hussein Javu katika dakika ya 30 na 59.
Mechi nyingine ya ligi hiyo ilichezwa mjini Morogoro kati ya Polisi Moro dhidi ya wageni wao Kagera Sugar iliyoisha kwa wenyeji kushinda bao 1-0 na kuifanya timu hiyo kuendelea kuvuta pumzi kusubiri kuona hatma yao katika ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22 sawa na Toto African..

Mikoa 18 yapata mabingwa wake


Na Boniface Wambura
Mikoa 18 kati ya 27 ya kimpira tayari imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa itakayoanza Mei 12 mwaka huu chini ya usimamizi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Timu tatu za juu katika Ligi hiyo ya Mabingwa zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014). Ligi ya FDL ina jumla ya timu 24 ambapo tatu katika ligi hiyo zilizoshuka daraja msimu huu ni Moro United ya Dar es Salaam, Small Kids ya Rukwa na Morani FC ya Manyara.

Mabingwa waliopatikana hadi sasa na mikoa yao kwenye mabano ni Abajalo SC (Dar es Salaam 2), Biharamulo FC (Kagera), Flamingo SC (Arusha), Friends Rangers (Dar es Salaam 3), Katavi Warriors (Katavi), Kiluvya United (Pwani), Kimondo FC (Mbeya) na Machava FC (Kilimanjaro).

Wengine ni Magic Pressure FC (Singida), Mbinga United (Ruvuma), Mji Njombe (Njombe), Polisi Jamii Bunda FC (Mara), Red Coast FC (Dar es Salaam 1), Rukwa United (Rukwa), Saigon FC (Kigoma), TECKFOLT FC ya Kilombero ambayo ni Shule ya Sekondari (Morogoro) na UDC FC ya Ukerewe (Mwanza).

Kila klabu inatakiwa kulipa ada ya ushiriki ambayo ni sh. 100,000 wakati usajili wa wachezaji wa timu hizo ni uleule uliofanyika katika Ligi ya Mkoa na unatakiwa kuwasilishwa TFF kwa ajili ya uthibitisho. TFF inapenda kusisitiza kuwa hakuna usajili mpya wa wachezaji kwa ajili ya ligi hiyo.

Mtanzania mwingine aula Norway


Na Boniface Wambura
Shirikisho la Mpira wa Miguu Norway (NFF) limetuma maombi ya kupatiwa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Godfrey Mlowoka ili aweze kucheza mpira nchini humo.

NFF inamuombea hati hiyo Mlowoka ili aweze kujiunga na klabu ya Ekne IL kama mchezaji wa ridhaa ambapo klabu yake ya zamani aliyokuwa akiichezea nchini imetajwa kuwa Sadani.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linafanyia kazi maombi hayo na mara taratibu zote zitakapokamilika hati hiyo ya uhamisho itatumwa nchini Norway.

Azam waendelea kujiwinda Morocco

Kocha Stewart Hall akiwanoa wachezaji wake Morocco


WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, Azam ambayo iko jijini Rabat kwa ajili ya mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho dhidi ya AS FAR Rabati ya huko inaendelea vizuri na mazoezi.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari Msaidizi wa Azam FC, Jaffer Idd maandalizi yanakwenda vizuri kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa Jumamosi (Mei 4 mwaka huu).

Msemaji huyo alisema wachezaji wana ari kubwa ya kuwapa raha watanzania na kuomba wazidi kuimbea kila la heri ili kupata ushindi Jumamosi na kutinga hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika.

Yanga, Coastal Union hapatoshi leo Taifa


Mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga

WAKIWA tayari na uhakika, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2012/13 Yanga, wanashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam leo kuvaana na Coastal Union ya Tanga, kila mmoja akitamba kutaka kulinda heshima yake mbele ya mwenzake.
Yanga licha ya kuwa bingwa tayari, imedai itateremka katika dimba hilo kuibuka na pointi tatu muhimu ili kulinda heshima na hadhi yao kama vigogo vya soka hapa nchini na Afrika Mashariki na Kati.
Kiburi hicho cha Yanga kinatokana na maandalizi ya mwisho waliyoyafanya wiki hii katika gym ya Quality Center pamoja na mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kiziguto, kikosi kizima kipo fiti kwa ajili ya mechi mbili zilizosalia na kudai kuwa, Salum Telela aliyekuwa anasumbuliwa na nyama za paja naye kajumuika na wenzake.
Coastal kwa upande wao wametamba kuwa lengo lao kubwa katika pambano dhidi ya Yanga ni kunyakua pointi tatu sambamba na kutibua sherehe za ubingwa wao waliotwaa Ijumaa iliyopita baada ya kuwabana Azam na kutoshana nao nguvu ya kufungana bao 1-1 mjini Tanga.
Coastal wapo nafasi ya sita katika msimamo ikitanguliwa na timu za Simba na Mtibwa Sugar, ikiwa na pointi 34 iwapo itaisimamisha Yanga itaweza kufikisha pointi 37 na kushika nafasi ya tano ila itategemea na matokeo ya pambano la Mtiwa sugar dhidi ya African Lyon linaloichezwa pia jioni ya leo.
Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku Azam Complex Chamazi, maafande wa JKT Ruvu na Tanzania Prisons watapigishana kwata, wakati Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini Mlandizi, Pwani kuwakabili ndugu zao Oljoro JKT ya Arusha.

Cheka, Mashali kumaliza ubishi leo PTA

Mabondia Francis Cheka (kulia) na Thomas Mashali wakiwa na Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi na Promota wa pambano lao, Tanaka Juma kabla ya kupima uzito jana
 
MABONDIA Francis Cheka 'SMG' na Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' leo wanatarajiwa kumaliza ubishi baina yao wakati watakapopanda ulingoni kuzipiga katika pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika.
Cheka na Mashali walioipimwa afya na uzito wao jana asubuhi na kukutwa wote wana kilo 74 watapigana katika pambano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam ambalo litasindikizwa na mapambano mengine 10 ya utangulizi.
Mabondia hao walitambiana jana wakati wa zoezi hilo la upimaji afya na uzito kila mmoja akitamba kuwa ni lazima leo ataibuka na ushindi kutwaa taji hilo pamoja na gari aina ya Noah watakayoigombania.
Cheka ndiye bingwa mtetezi wa taji hilo alililolitwaa mwaka jana kwa kumpiga Mada Maugo na ametamba kwamba hana hofu na Mashali ambaye ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati.
Mratibu wa pambano hilo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema kila kitu kimekaa sawa kwa ajili ya pambano hilo na kwamba  litachezeshwa na mwamuzi Jon Shipanuka kutoka Zambia na kusawidiwa na majaji Daud Chikwanje wa Malawi, Steve Okumu wa Kenya na Ismail Sekisambu wa Uganda.
Msimamizi mkuu atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBC, Boniface Wambura anayemwakilisha Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi ambaye ndiye aliyekuwa asimamie pambano hilo anatarajiwa kwenda Ghana kusimamia pambano jingine la kimataifa.

Real Madrid watupwa nje Ligi ya Ulaya licha ya ushindi wa nyumbani

Kipa Ike Casillas, akimliwaza Sergio Ramos aliyekuwa akilia baada ya Madrid kung'olewa kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku

LICHA ya kupigana kiume na kujipatia mabao 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund, kocha Jose Mourinho na vijana wake wa Real Madrid wamejikuta wakishindwa kutimiza ndoto za kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kusaka taji la 10 kwa kutupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-3.
Madrid ikiwa dimba la nyumbani la Santiago Bernabeu, nchini Hispania ilikuwa ikihitajika kupata ushindi wa mabao 3-0 ili kuing'oa Dortmund, lakini uwezo wao uliishia kwa kuambulia mabao hayo mawili ambayo hata hivyo hayawajasaidia kutokana na mechi ya awali wiki iliyopita kunyukwa mabao 4-1.
Mabao ya ushindi kwa Madrid jana yaliwekwa kimiani dakika za lala salama baada ya wageni wao kuwabana kipindi kizima cha kwanza na nusu ya kile cha pili kwa kutofungana.
Karim Benzema aliiandikia Madrid bao dakika ya 83 akimalizia kazi ya Mesut Ozil kabla ya dakika tano baadaye Sergio Ramos kuongeza la pili na kuwapoa wenyeji imani ya kupata bao jingine la kuwavusha hatua hiyo ya nusu fainali.
Hata hivyo hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Howard Webb kutoka England ikilia kuashiria kumalizika kwa pambano hilo wenyeji Madrid walikuwa washindi wa 2-0, lakini ushindi ambao haukuwasaidia kutinga fainali ya michuano hiyo na kuiacha Dortmund wakitangulia kumsubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya leo.
Nusu fainali hiyo inazikutanisha timu za Barcelona ya Hispania itakayoikaribisha Bayern Munich ya Ujerumani, ikiwa na deni la kipigo cha mabao 4-0 ilichopewa wiki iliyopita ilipocheza ugenini.
Kama ilivyokuwa kwa Madrid, Barcelona inayokaribia kutwaa ubingwa wa La Liga, itakuwa na kazi pevu ya kuwaondosha Wajerumani hao ambao msimu huu wameonekana kuwa moto wakiwa tayari wameshanyakua taji la Bundesliga hata kabla ligi haijamalizika.