STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 1, 2013

Cheka, Mashali kumaliza ubishi leo PTA

Mabondia Francis Cheka (kulia) na Thomas Mashali wakiwa na Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi na Promota wa pambano lao, Tanaka Juma kabla ya kupima uzito jana
 
MABONDIA Francis Cheka 'SMG' na Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' leo wanatarajiwa kumaliza ubishi baina yao wakati watakapopanda ulingoni kuzipiga katika pambano la kimataifa la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika.
Cheka na Mashali walioipimwa afya na uzito wao jana asubuhi na kukutwa wote wana kilo 74 watapigana katika pambano hilo litakalofanyika kwenye ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam ambalo litasindikizwa na mapambano mengine 10 ya utangulizi.
Mabondia hao walitambiana jana wakati wa zoezi hilo la upimaji afya na uzito kila mmoja akitamba kuwa ni lazima leo ataibuka na ushindi kutwaa taji hilo pamoja na gari aina ya Noah watakayoigombania.
Cheka ndiye bingwa mtetezi wa taji hilo alililolitwaa mwaka jana kwa kumpiga Mada Maugo na ametamba kwamba hana hofu na Mashali ambaye ni bingwa wa Afrika Mashariki na Kati.
Mratibu wa pambano hilo, Yasin Abdallah 'Ustaadh' alisema kila kitu kimekaa sawa kwa ajili ya pambano hilo na kwamba  litachezeshwa na mwamuzi Jon Shipanuka kutoka Zambia na kusawidiwa na majaji Daud Chikwanje wa Malawi, Steve Okumu wa Kenya na Ismail Sekisambu wa Uganda.
Msimamizi mkuu atakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Viwango na Ushindi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania, TPBC, Boniface Wambura anayemwakilisha Rais wa IBF/USBA, Onesmo Ngowi ambaye ndiye aliyekuwa asimamie pambano hilo anatarajiwa kwenda Ghana kusimamia pambano jingine la kimataifa.

No comments:

Post a Comment