Mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga |
WAKIWA tayari na uhakika, mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu 2012/13 Yanga, wanashuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam leo kuvaana na Coastal Union ya Tanga, kila mmoja akitamba kutaka kulinda heshima yake mbele ya mwenzake.
Yanga licha ya kuwa bingwa tayari, imedai itateremka katika dimba hilo kuibuka na pointi tatu muhimu ili kulinda heshima na hadhi yao kama vigogo vya soka hapa nchini na Afrika Mashariki na Kati.
Kiburi hicho cha Yanga kinatokana na maandalizi ya mwisho waliyoyafanya wiki hii katika gym ya Quality Center pamoja na mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kiziguto, kikosi kizima kipo fiti kwa ajili ya mechi mbili zilizosalia na kudai kuwa, Salum Telela aliyekuwa anasumbuliwa na nyama za paja naye kajumuika na wenzake.
Coastal kwa upande wao wametamba kuwa lengo lao kubwa katika pambano dhidi ya Yanga ni kunyakua pointi tatu sambamba na kutibua sherehe za ubingwa wao waliotwaa Ijumaa iliyopita baada ya kuwabana Azam na kutoshana nao nguvu ya kufungana bao 1-1 mjini Tanga.
Coastal wapo nafasi ya sita katika msimamo ikitanguliwa na timu za Simba na Mtibwa Sugar, ikiwa na pointi 34 iwapo itaisimamisha Yanga itaweza kufikisha pointi 37 na kushika nafasi ya tano ila itategemea na matokeo ya pambano la Mtiwa sugar dhidi ya African Lyon linaloichezwa pia jioni ya leo.
Nayo Kagera Sugar iliyo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo itakuwa mgeni wa Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku Azam Complex Chamazi, maafande wa JKT Ruvu na Tanzania Prisons watapigishana kwata, wakati Ruvu Shooting itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake Mabatini Mlandizi, Pwani kuwakabili ndugu zao Oljoro JKT ya Arusha.
No comments:
Post a Comment