STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, May 1, 2013

Real Madrid watupwa nje Ligi ya Ulaya licha ya ushindi wa nyumbani

Kipa Ike Casillas, akimliwaza Sergio Ramos aliyekuwa akilia baada ya Madrid kung'olewa kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku

LICHA ya kupigana kiume na kujipatia mabao 2-0 dhidi ya Borussia Dortmund, kocha Jose Mourinho na vijana wake wa Real Madrid wamejikuta wakishindwa kutimiza ndoto za kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kusaka taji la 10 kwa kutupwa nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-3.
Madrid ikiwa dimba la nyumbani la Santiago Bernabeu, nchini Hispania ilikuwa ikihitajika kupata ushindi wa mabao 3-0 ili kuing'oa Dortmund, lakini uwezo wao uliishia kwa kuambulia mabao hayo mawili ambayo hata hivyo hayawajasaidia kutokana na mechi ya awali wiki iliyopita kunyukwa mabao 4-1.
Mabao ya ushindi kwa Madrid jana yaliwekwa kimiani dakika za lala salama baada ya wageni wao kuwabana kipindi kizima cha kwanza na nusu ya kile cha pili kwa kutofungana.
Karim Benzema aliiandikia Madrid bao dakika ya 83 akimalizia kazi ya Mesut Ozil kabla ya dakika tano baadaye Sergio Ramos kuongeza la pili na kuwapoa wenyeji imani ya kupata bao jingine la kuwavusha hatua hiyo ya nusu fainali.
Hata hivyo hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi Howard Webb kutoka England ikilia kuashiria kumalizika kwa pambano hilo wenyeji Madrid walikuwa washindi wa 2-0, lakini ushindi ambao haukuwasaidia kutinga fainali ya michuano hiyo na kuiacha Dortmund wakitangulia kumsubiri mshindi wa nusu fainali nyingine ya leo.
Nusu fainali hiyo inazikutanisha timu za Barcelona ya Hispania itakayoikaribisha Bayern Munich ya Ujerumani, ikiwa na deni la kipigo cha mabao 4-0 ilichopewa wiki iliyopita ilipocheza ugenini.
Kama ilivyokuwa kwa Madrid, Barcelona inayokaribia kutwaa ubingwa wa La Liga, itakuwa na kazi pevu ya kuwaondosha Wajerumani hao ambao msimu huu wameonekana kuwa moto wakiwa tayari wameshanyakua taji la Bundesliga hata kabla ligi haijamalizika.

No comments:

Post a Comment