LICHA ya kutolewa, lakini Yanga inastahili pongezi kwa kupigana kiume mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Al Ahly baada ya kung'olewa kwa mikwaju ya penati katika pambano la marudiano lililochezwa usiku wa jana.
Yanga ilipambana kwa dakika 90 na kujikuta wakilala kwa bao 1-0 na kufanya matokeo ya jumla kuwa 1-1 na hivyo kuingia kwenye hatua ya upigaji wa penati ambapo ilionekana dhahiri walikuwa wakielekea kufuzu baada ya Deo Munishi Dida kudaka penati mbili za Wamisri.
Dida aliyeonyesha ushupavu mkubwa alidaka penati za Saed Mowaeb na Hossan Ashour huku zile za Abdalllah Said, Gedo, Mahmoud Trezeguet na Mohamed Nagieb zilimpita.
Hata hivyo Oscar Joshua alikosa penati naye na baadaye Bahanuzi aliyekuwa akimalizia mikwaju ya penati tano tano, alipaisha mkwaju wake wakati wachezaji wenzake wakijiandaa kushangilia kuwavua ubingwa Al Ahly na kuongezwa penati moja moja.
Katika hatua hiyo Mbuyi Twite alilizamisha jahazi la Yanga baada ya kukosa mkwaju wake na kuwafanya mabingwa watetezi hao kufuzu hatua ya pili na kutarajia kukutana na waarabu wenzao kutola Libya, Al Ahli Benghazi.
Kwa wastani Yanga ilikuwa imejiandaa kuweka rekodi kwa soka la uhakika na umakini mkubwa iliyooonyesdha katika mchezo huo kwa kuwabana wenyeji wao kwenye uwanja wa Border Guard mjini Alexandria.
Kipindi cha kwanza kiliisha kwa sare ya kutofungana kabla ya wenyeji kupata bao dakika za jioni baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya kuokoa mpira uliokwamishwa na Sayed Moawad. dakika ya 71.
Ndipo ikaja hatua ya kupigiana penati baada ya dakika 90 kumalizika kwa matokeo hayo yaliyofanya timu hizo kuwa nguvu sawa kwani Yanga ilishinda bao 1-0 nyumbani wiki iliyopita na zikaja penati na Yanga wakapata penati zao kupitia nahodha Nadir Cannavaro, Emmanuel Okwi na Didier Kavumbagu.
Kung'olewa kwa Yanga kumehitimisha safari ya timu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa baada ya awali Azam, KMKM na Chuoni kung'oka raundi ya awali katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.