* Kibao cha Soukous Machine kilimtambulisha dunia nzima
* Kwa sasa yupo Australia na bendi mpya ya Warako Musica
UNAPOLITAJA jina la Tchico Tchicaya kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa Soukous, akili zao zitaenda hadi miaka zaidi ya 20 iliyopita wakikumbukia kibao cha Soukous Machine kilichomtambulisha mno mwanamuziki huyo.
Kibao hicho kilichofyatuliwa mwaka 1987, kilimtambulisha vema Tchico kama mmoja wanamuziki wabunifu na aliyekuwa akipenda na kuuenzi utamaduni wa nchi yake ya Jamhuri ya Congo (Congo-Brazzaville).
Wakati kibao hicho kinatamba wanamuziki wakali wa Congo-Kishansa kama akina Pepe Kalle, Nyboma Mwandido, Kanda Bongoman na wengine ndio kwanza walikuwa wameanza kuiteka dunia kwa muziki wao na kumfanya Tchico kuenda nao sambamba na nguli hao ambao baadhi wameshafariki.
Nguli huyo ambaye kwa sasa ameweka maskani yake nchini Australia akiwa na bendi mpya iitwayo Warako Musica akishirikiana na Passi Jo, katika kibao hicho aliweka madoido ya ngoma asilia na milio ya ndege iliyovutia.
Katika kibao hicho mwanamuziki huyo, alikuwa akiisifia Afrika na kutaja majina ya baadhi ya miji ya nchi za bara hilo, huku akiufagilia muziki huo wa Soukous, ambao unaendelea kubamba mpaka leo katika medani ya muziki.
Tchico aliyeanza muziki zaidi ya miaka 30 iliyopita, majina yake kamili ni Pambou-Tchicaya Tchico, lakini majina yake ya mwisho ndiyo yakifahamika zaidi kwa wapenzi wa muziki wa Soukous aliokuwa akiupiga.
Ukali wa Tchico ulianza kuonekana mwaka 1970 alipoanza muziki kama muimbaji katika bendi iliyofahamika kwa jina la Monta Lokoka iliyokuwa na maskani yake katika mji mkuu wa Congo, Brazzaville.
Akiwa na bendi hiyo alifanikiwa kupakua na kutamba na albamu kali mbili zilizofahamika kwa majina ya Rina ya mwaka 1970 na Loemarthe iliyotoka mwaka 1971.
Miaka miwili baada ya kujiona kaiva vema, mkali huyo alijitosa katika bendi ya Les Bantous de la Capitale akiwa mmoja wa waimbaji nyota wa bendi hiyo iliyokuwa maarufu mwa makundi yaliyotamba enzi hizo jijini Brazzaville.
Ndani ya Les Bantous de la Capitale, Tchico alitoka na albamu za Isabelle ya 1972, Celia-Shantina (1973) na Santana ya mwaka 1974, ambapo baadaye alifyatua albamu nyingine za Shanta Maguy (1974), Sambela Sambela (1975) na Ah Ponton la Belle mwaka 1976 akiwa na kundi la African Kings.
Mwaka 1977 na 1979 Tchico alipeleka 'maujuzi' yake nchini Nigeria alipoishi na kufanikiwa kupakua albamu nne tofauti ambazo zilimpa mafanikio makubwa kiasi cha kubatizwa jina la utani la Voix d'or.
Katika kipindi hicho cha mafanikio ndipo alipokuwa akiimba na mkali Lolo Lolita ambapo walifyatua albamu iliyotamba ya Jeannot.
Mwaka 1983, Tchico aliamua kwenda Paris Ufaransa, kabla ya kufuatwa baadaye na utiriri mkubwa wa wanamuziki wa Kicongo kwenda nchini humo.
Akiwa katika jiji hilo la maraha, Tchico, aliweza kurekodi nyimbo mbalimbali katika studio tofauti tofauti, kulikoenda sambamba na kubadilika kwa jina la bendi yake toka Afro Festival hadi Les Evades de Ponton la Belle na kisha baadaye Les Officiers de la Musique Africaine.
Nyota yake ilizidi kung'ara zaidi katikati ya mwaka 1980 na mwanzoni mwa 1990 baada ya kubadili jina la kundi lake toka Orchestre Kilimandjaro hadi kuwa La Voix d' Or au Soukous Machine akitumia moja ya vibao vilivyompaisha kama jina la kundi, ambapo alifyatua vibao mbalimbali vikali vilivyotambulisha karibu bara zima la Afrika na dunia kwa ujumla.
Baadhi ya nyimbo alizotoa kipindi hicho ni pamoja na Lucie Matanga, Paris-Tropical, Les larmes de Les Iles, Kembo Na Nzambi, Guyguy wa Mapendo, Adios Luluna, Jambo Afrika, Deliverance na A'Argent Ange ou Demon.
Kutokana na kutambulika huko dunia nzima, mwanzoni mwa karne mpya yaani miaka ya 2000, aliamua kuhamia na kuweka makazi yake nchini Australia akiendelea na kazi yake ya muziki akiwa na Passi Joo katika bendi yake mpya iitwayo Warako Musica aliyotoa nao albamu ya 'Ya Banganga'.
Baadhi ya wanamuziki walioshiriki kutoa kibao cha Soukous Machine cha mwaka 1987 na ambacho pengine ndicho maarufu kwa Watanzania ni pamoja na yeye Tchico Tchicaya aliyeongoza katika uimbaji, Jacqueline Brouta na Samba Kadhy Bell waliokuwa waimbaji waitikiaji.
Katika gitaa la solo alikuwa Denis la Cloche, huku Casanova de Ketchel akicharaza gitaa la rhythms na katika gitaa zito la besi alisimama Remy Salomon, na 'mkaanga chips' (mpiga dramu) alikuwa ni Denis Hekimian.
Lolitta Babind alikuwa akipiga nyanga, wakati mpapasa kinanda alisimama mkali wa zamani aliyeitwa Tony na Jean Marie Kabongo na wajina wake, Jean Claude Leandre walikuwa wakipuliza ala za upepo Kabono akipuliza 'Domo la Bata' na mwenzie akipiga tarumbeta.
Mbali na kibao ca Soukous Machine, Tchico pia alitamba na vibao vingine kama Africa Dance Machine, Sonima, African Carnaval, Cocktail Tropical,
L'ambiance à Paris, Dynamic Afro-Soukous, L'argent domine le monde, Full Steam Ahead, Nostalgie d'Afrique, Amour maternel, Mon enfant na Giselle.
Nyingine ni pamoja na Amie Clara, Tania, Rosalie, Jeannot, Lucia, dans Tam Tam d'Afrique, Méditation, L'heure a sonné, Operation Soukous, Mamy Rosa, Josintha, From Congo to Nigeria, Ah Ponton la Belle na nyinginezo.
Ingawa ni miaka mingi imepita bila ya nyimbo za mkali huyo kusikika hapa nchini, lakini bila shaka Tchico hatasahulika kirahisi kwa vile namna ya uvaaji wake na hata upigaji wake wa muziki katika bendi alizozifanyia kazi, umemfanya kuwa vichwani kwa wapenzi wa muziki hususani wa Soukous.