STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Monday, November 19, 2012

Choki kuwaamua Coast, Dar Modern Jumamosi


MUIMBAJI nyota na Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki anatarajiwa kuwa jaji katika 'pambano' la makundi mawili ya muziki wa taarab nchini, Dar Modern 'Wana wa Jiji' na Coast Modern 'Watafiti wa Mipasho litakalofanyika siku ya Jumamosi.
Mchuano wa makundi hayo yanayotamba nchini kutokana na nyimbo zao, litafanyika kwenye eneo la Kimara jijini Dar es Salaam na Choki atawaongoza majaji siku ya onyesho hilo.
Tayari makundi hayo mawili yameanza kutambiana juu ya pambano hilo ambalo litafanyika wakati kila kundi likiwa limetoka kukamilisha albamu zao mpya.
Coast linaloongozwa na mkurugenzi wake Omar Tego, limekamilisha albamu ya 'Mwanamke Kujiamini' wakati Dar Modern lililopo chini ya Mridu Ally, limefyatua albamu tatu kwa mpigo za 'Nauvua Ushoga', 'Toto la Kiafrika' na 'Ndugu wa Mume'.


Watoto watatu wa Fella waachia mpya

Add caption



WASANII watatu chipukizi walioibuliwa na kituo cha Mkubwa na Wanae, Asnath Mathias 'Asnat', Yusuf Kondo 'K Young' na Getruda Ally 'Ge2' wameachia nyimbo zao mpya tatu tofauti, wakifuata nyayo za kaka zao kutoka kundi la TMK Wanaume Family.
Baadhi ya nyimbo za wasanii hao zimeshaanza kusambazwa katika vituo vya rdio kwa lengo la kurushwa hewani kusikika kwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya.
Meneja wa wasanii hao, Said Fella 'Mkubwa' aliiambia MICHARAZO kuwa, Asnat yeye amefyatua wimbo uitwao 'Tungi', wakati K Young ameachia 'Nitafika' na Ge2 akishirikiana na Abbas Maromboso amerekodi wimbo uitwao 'Nawashusha'.
Fella alisema wasanii hao ambao wanatarajiwa kutambulishwa rasmi kwa mashabiki katika onyesho litakalofanyika hivi karibuni katika klabu moja maarufu iliyopo jijini, baada ya mipango ya awali kuwatambulisha jana kushindikana.
Meneja huyo alisema chipukizi hao wameachia nyimbo hizo ikiwa ni siku chache baada ya kundi jingine analoliongoza la TMK Wanaume Family kukamilisha kibao chao kipya cha 'Mnatuonaje' alichodai ni cha kufungia mwaka 2012.
"Kituo chetu kimefanikiwa kuwafyatulia wimbo wasanii wake watatu tofauti, Asnat, K-Young na Ge2, ikiwa ni siku chache baada ya TMK Wanaume kuachia 'Mnatuonaje' wimbo unaokuja kuchukua nafasi ya ule wa 'Kichwa Kinauma'," alisema Fella.
Fella alisema kwa sasa kituo chao kinajipanga kwa ajili ya kurekodi video za nyimbo hizo ili wasanii hao chipukizi nao waanze kuuza sura wakifuata nyayo za chipukizi wenzao, Dogo Aslay, Dogo Mu, na H-Kumbi walioibuliwa na Mkubwa na Wanae.

Kanumba kuenziwa kiaina Dar






ALIYEKUWA muigizaji nyota wa filamu nchini, marehemu Steven Kanumba anatarajiwa kuenziwa kiaina kupitia tamasha litakalofanyika mapema mwakani sambamba na uzinduzi wa filamu maalum juu yake iitwayo 'After Death'.
Muongozaji maarufu wa filamu nchini, mwanadada Leah Richard 'Lamata' aliiambia MICHARAZO, kuwa tamasha hilo dogo litakalooenda sambamba na uzinduzi wa filamu hiyo litafanyika Februari mwakani jijini Dar es Salaam.
Lamata, alisema katika filamu hiyo ya After Death iliyotayarishwa na Jacklyne Wolper imewashirikisha waigizaji chipukizi ambao walioibuliwa na Kanumba kupitia filamu zake kama 'This is It' na 'Uncle JJ' pamoja na msanii aliyefanana kidogo na Kanumba.
"Filamu hiyo imekamilika kwa sasa ikiwa imeshirikisha wasanii kadhaa wenye majina na wasio na majina, akiwamo mmoja aliyefanana na Kanumba, na tumepanga kufanya katamasha ka kumuenzi wakati wa uzinduzi wake," alisema Lamata.
Lamata alisema wameamua kuitengeneza filamu hiyo ya 'After Death' kama njia ya kumuenzi Kanumba kutokana na mchango wake mkubwa katika kuendeleza tasnia ya filamu na wasanii wengi kwa ujumla enzi za uhai wake.
Alisema kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuweka  mambo sawa ili kufanikisha jambo walilokusudia, licha ya kusisitiza kua filamu hiyo mpya tayari imeshakamilika kila kitu na inasubiri kuzinduliwa na kuachiwa  mtaani.

Add caption

WALIOTIMULIWA YANGA KUKIMBILIA MAHAKAMANI


UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga, upo hatarini kuburuzwa mahakamani na waliokuwa watendaji wa sekretarieti yao waliyoivunja hivi karibuni kwa kile kinachoelezwa kushindwa kuwalipa 'mafao' yao baada ya kuwatimua.
Yanga ilivunja sekretarierti hiyo iliyowahusisha Katibu Mkuu wake, Celestine Mwesigwa na Afisa Habari, Louis Sendeu pamoja na kamati nzima ya utendaji iliyokuwepo kwa kilichoelezwa kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo tangu watimuliwe Yanga, watendaji hao imeelezwa wamekuwa wakizungushwa kulipwa malimbikizo ya madeni wanayoidai Yanga na fidia ya kuvunjiwa mikataba kwa baadhi yao.
Kutokana na kuzungushwa huko kunakoelezwa inatokana na msimamo wa uongozi kutoyatambua madeni ya nyuma, watendaji hao wameanza mchakato wa kulifikisha suala lao mahakamani ili kupatiwa haki zao kisheria.
Kwa mujibu wa habari za ndani toka Yanga na kuthibitishwa na mmoja wa watendaji hao, ni kwamba tayari suala lao lipo mikononi mwa wanasheria na wakati wowote litafikishwa mahakamani.
Chnzo hicho kilisema watendaji hao watalifikisha suala hilo katika mahakama ya kazi na usuluhishi wakiamini itawasaidia kupata jasho lao.
"Ni kweli tumepanga kwenda mahakamani kwa sababu tunaona kama haki yetu inataka kupotea bure, wao ndio waliovunja mkataba vipi wasitulipe, tayari jukumu la kufungua kesi lipo mikononi mwa mwanasheria wetu," mmoja wa walalamikaji hao aliyeomba kuhifadhiwa jina lake aliiambia MICHARAZO.
Mtandao huu lilimsaka Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrance Mwalusako, ili kupata ufafanuzi wa sakata hilo la kuzungushwa kwa malipo ya watendaji hao, ambapo alisema kwa kifupi kwamba hafahamu lolote.
"Mie sijui lolote kwa sababu wakiati wakitumuliwa sikuwepo madarakani na pia sifahamu kama wanajipanga kwenda mahakamani," alisema Mwalusako.
Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu chochote.
Mbali na Mwesigwa na Sendeu aliyekuwa amemaliza mkataba wake, wengine waliotimuliwa katika Sekretarieti hiyo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala na  Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu, huku aliyekuwa meneja wa timu, Hafidh Saleh aliyedaiwa kapangiwa majukumu mengine Yanga.

Mwisho

NTEBE AKIRI DURU LA KWANZA LILIKUWA GUMU


BEKI wa kutegemewa na timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Salvatory Ntebe, amesema licha ya kucheza misimu kadhaa ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hajaona ligi ngumu kama ilivyokuwa katika duru la kwanza ya msimu huu.
Aidha Ntebe aliyewahi kucheza soka la kulipwa katika klabu ya Atletico ya Burundi, alisema huenda duru la pili likawa gumu zaidi kwa vile muda wa mapumziko wa ligi hiyo timu zitakuwa zikijiimarisha maradufu.
Akizungumza na MICHARAZO juzi, beki huyo wa kati alisema duru la kwanza la ligi kuu msimu huu lilikuwa gumu na ndiop maana imekuwa na matokeo yenye kustaajabisha na timu kutoachana mbali kipointi kama msimu mingine.
"Tunashukuru kumaliza salama duru la kwanza, ila nikiri lilikuwa gumu sijawahi kuona, pale watu walipokuwa wakijua timu fulani inashinda matokeo yalikuwa kinyume na pale watu wasipotarajia kadhalika, inavutia," alisema.
Hata hivyo Ntebe alisema anadhani duru lijalo litakuwa gumu zaidi kwani timu zitatumia muda wa mapumziko kurekebisha makosa  na kuimarisha vikosi vyao, ili warejeapo duru la pili wakiwa wamejizatiti.
"Nadhani duru la pili litakuwa gumu zaidi, kila timu itatumia muda uliopo kuweka mambo sawa, hivyo kuongeza ushindani tofauti na duru lililopita lililokuwa na matokeo ya kustaajabisha karibu kila mechi," alisema.
Juu ya kikosi cha timu yake, Ntebe alisema kimepigana kadri ya uwezo wao na ndio maana kimekuwa katika nafasi iliyopo, ingawa anaamini duru lijalo timu hiyo itarejea na kasi na nguvu mpya na kufukuzana na klabu zilizopo juu.
Hadi ligi hiyo ikimaliza mzunguko wa kwanza jana kwa pambano la Ruvu Shooting na Prisons-Mbeya, Mtibwa ilikuwa nafasi ya nne na pointi 22 sawa na Coastal ila wakibebwa na uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mwisho

Ruvu Shooting yamaliza duru la kwanza kwa kishindo yapania duru lijalo

Kikosi cha timu ya Ruvu Shooting ambacho jana kilimaliza duru la kwanza kwa ushindi wa mabao 2-0




UONGOZI wa klabu ya Ruvu Shooting umesema utatumia mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara kukiimarisha kikosi ili waweze kufanya vema katika duru lijalo la ligi hiyo.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alisema yapo mapungufu waliyoyaona katika duru la kwanza lililohitimishwa jana kwa mchezo dhidi yao na Prisons-Mbeya na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 watayarekebisha ili wafanye vizuri duru lijalo.
Bwire, alisema wangependa kuona duru lijalo wakifanya vema zaidi na kujiweka katika nafasi nzuri, licha ya kukiri ndoto za ubingwa ni ngumu kwao kutokana na ushindani uliopo toka kwa klabu kubwa zilizopo nafasi za juu.
"Tutautumia muda wa mapumziko wa ligi kuimarisha kikosi chetu kwa kurekebisha dosari zilizoonekana duru la kwanza, hata hivyo bado ni mapema mno kuweka bayana panga pangua ya kikosi chetu kwa sasa," alisema.
Bwire, alikiri duru la kwanza lilikuwa gumu na lenye ushindani ila anashukuru timu yao ilifanya vema ambapo imemaliza duru hilo ikiwa na pointi 20 ikiwa nafasi ya nane.
"Duru la kwanza lilikuwa gumu na lenye ushindani, kila timu ilionekana kuwa makini kutopoteza pointi kirahisi na kuifanya ligi isitabirike kirahisi," alisema.
Ligi Kuu inayoshirikisha timu 14 kwa sasa ipo mapumzikoni kwa muda wa kama miezi miwili kabla ya kuanza tena duru la pili mapema mwakani.

Mwisho

GUINESS FOOTBALL CHALLENGE YAREJEA KWA KISHINDO



SHINDANO maarufu inalohusisha mashabiki wa soka nchini la 'Guiness Football Challenge', limerejea upya safari hii likifahamika zaidi kama 'Pan Africa Guinness Football Challenge' likishirikisha washiriki wa mataifa matano ya barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa mwa MICHARAZO na waratibu wa shindano hilo ambalo mshidni wake atajinyakulia dola za kimarekani 900,000 litahusisha washiriki wa mataifa ya Tanzania, Kenya, Uganda, Ghana na Cameroon.
Taarifa hiyo inasema washiriki wa mataifa hayo ya Afrika Mashariki na Magharibi watachuana kuwania ubingwa wa Afrika kupitia shindano hilo maarufu la kwenye runinga.
Msimu uliopita wawakilishi waliopatikana kuiwakilisha Tanzania nchini Afrika Kusini waliweza kufanya vema, kitu ambacho wanaamini hata msimu huu wawakilioshi watakaopatikana hawataangusha watanzania katika fainali hizo.
Taarifa hiyo imeeleza usaili wa shindano la hapa nchini unatarajiwa kufanyika siku ya Jumamosi kwenye viuwanja vya Leaders na litawahusisha watu wote wenye umri kuanzia miaka 18 na wenye uwezo na ufahamu mzuri juu ya mchezo wa soka.
"Wapenzi wa soka wanakaribishwa kushiriki kwani nafasi zipo wazi kinachohitajika ni upeo wa mambo ya soka na uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu kama vile kupiga danadana kwa manjonjo na ufundi zaidi wa kuuchezea mpira," taarifa hiyo inasema.
Katika mchakato wa kupata wawakilishi wa Tanzania katika shindano la msimu huu, kutakuwa na burudani ya kusikitiza usaili huo toka kwa wasanii mbalimbali.

Mwisho

SERENGETI BOYS ILIVYOINYOA KONGO JANA KATIKA PICHA

Kipa wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, ya Kongo Brazzaville, Ombandza Mpea Joe akilalama baada ya mpira wa adhabu uliopigwa na Mufathir Yahya Abbas kutinga nyavuni na kuwapa wenyeji ushindi wa 1-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.

Bao pekee leo

Kipa wa Kongo akining'inia kwenye milingoti ya lango baada ya kuukosa mpira uliopaa juu ya lango lake

Mchezaji wa Serengeti, Suleiman Hamisi Bofu akipiga mpira kichwa mbele ya beki wa Kongo, Ondongo Boungena

Beki Okombi Francis wa Kongo akiokoa mbele ya Joseph Kimwaga 

Wachezaji wa Kongo wakimdhibiti mchezaji wa Serengeti

Hussein Twaha 'Messi' akiwafunga tela wachezaji wa Kongo

Makocha wa Serengeti Jacob Michelsen na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo wakiwapa maelekezo vijana wao wakati mpira uliposimama kwa muda

Kipa wa Serengeti Boys, Peter Manyika akiruka hewani kupangua mchomo mkali ulioelekezwa langoni mwake 

Kipa wa Kongo, akimdondokea kiungo wa Serengeti, Farid Mussa Shah kudaka mpira, huku beki wake, Ondongo Boungena akiwa tayari kumsaidia 

Farid kulia na Ondongo kushoto

Kikosi cha vijeba wa Kongo Brazzaville

Beki Ismail Adam Gambo wa Serengeti akimdhibiti Ibara Vinny wa Kongo Brazzazille

Hussein Twaha akiwatoka wachezaji wa Kongo

Serengeti wakishangilia bao lao kwa staili ya aina yake

11 wa kwanza wa Serengeti leo

Wachezaji wa Serengeti Boys wakiimba wimbo wa taifa

Benchi la Ufundi la Serengeti Boys wakati wa wimbo wa taifa

Hussein Twaha akipasua katikati ya msitu wa wachezaji wa Kongo

Hussein Twaha akimiliki mpira mbele ya beki wa Kongo

Joseph Kimwaga akimtoka beki wa Kongo Brazzaville


Beki wa Kongo Okombi Francis baada ya kumpitia kwanja Tumaini Baraka Mosha wa Serengeti
Mudathir akiondoka na mpira

Tumaini Baraka Mosha akimtoka Okombi

Kushoto refa anasema twende, huku Tumaini Baraka Mosha akiwania mpira dhidi ya Ondongo

BENZEMA AIBEBA REAL MADRID, MESSI SASA ABAKISHA SABA TU










MADRID, Hispania
Barcelona walijichimbia kileleni mwa msimamo wa La Liga, Ligi Kuu ya Hispania kwa tofauti ya pointi sita dhidi ya Atletico Madrid wakati Lionel Messi alipofunga magoli mawili kwa mara ya saba msimu huu na kutengeneza jingine lililofungwa na Alex Song kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe na klabu hiyo katika ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Real Zaragoza jana (Novemba 17, 2012).

Mwanasoka Bora wa Dunia, Messi aliongeza idadi ya magoli yake msimu huu hadi kufikia 17 baada ya kufunga mabao safi wakati Barca ambayo haijafungwa katika La Liga msimu huu ikifikisha pointi 34 kutokana na mechi 12.

Atletico wana pointi 28 na leo Jumapili (Novemba 18, 2012) watacheza dhidi ya Granada, wakati Real Madrid inayokamata nafasi ya tatu ikipunguza tofauti ya pointi baina yao na Atletico kuwa pointi mbili baada ya kushinda nyumbani 5-1 dhidi ya Athletic Bilbao.

Baada ya goli la mapema la kujifunga la Jon Aurtenetxe, Karim Benzema, Sergio Ramos, Mesut Ozil na Sami Khedira wakaongeza mengine kwa kikosi cha kocha Jose Mourinho kikiendelea kuimarika baada ya kuanza msimu wka kusuasua ambapo sasa wameshinda mechi saba katika mechi nane zilizopita.

Real sasa wamefunga magoli 19 dhidi ya Bilbao katika mechi zao zilizopita za La Liga kwenye Uwanja wa Bernabeu na tukio la kushangaza lilikuwa ni kwa straika Cristiano Ronaldo kushindwa kuongeza idadi ya mabao 12 aliyo nayo katika La Liga msimu huu baada ya kutofunga jana.

Straika huyo wa zamani wa Manchester United alirejea uwanjani akiwa na jeraha la juu ya jicho aliloumia katika mechi iliyopita ya La Liga waliyoshinda 2-1 dhidi ya Levante.

Messi sasa amefikisha magoli 78 katika mwaka wa kalenda wa 2012 kwa klabu yake (magoli 66) na kwa nchi yake ya Argentina (magoli 12) na anaikaribia kwa kasi rekodi inayoshikiliwa na Mjerumani Gerd Muller aliyefunga magoli 85 mwaka 1972.

Ushindi wa jana wa Barca pia unamaanisha kuwa kocha Tito Vilanova, aliyerithi mikoba ya Pep Guardiola mwishoni mwa msimu uliopita, amekuwa kocha wa kwanza kuiongoza timu kupata ushindi wa mechi 11 katika mechi 12 za ufunguzi wa La Liga tangu kocha Radomir Antic afanye hivyo wakati akiwa na Real Madrid msimu wa 1991-92.

MATOKEO MECHI ZA LA LIGA JANA JUMAMOSI (NOV. 17, 2012)

Barcelona    3 Real Zaragoza   1 
Osasuna      0 Malaga              0 
Real Madrid 5 Athletic Bilbao    1 
Valencia       2 Espanyol           1 

MATOKEO MECHI ZA SERIE A ZILIZOCHEZWA JANA JUMAMOSI (NOV. 17, 2012)

Juventus 0 Lazio      0 
Napoli     2 AC Milan 2  


Chanzo:Straikamkali

SERENGETI BOYS WANUSA FAINALI ZA AFCON U17


BAO lililotokana na faulo iliyotolewa kwa Serengeti Boyz na refa Mganda Miiro Nsubuga baada ya Hussein Ibrahim wa Serengeti kuchezewa faulo na beki wa Congo, Mohendik Brel iliisaidia timu ya Tanzania U17 kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kongo jana.
 

Mfungaji wa bao hilo alikuwa kiungo Mudathir Abbas, aliyekwamiza faulo hiyo dakika ya 15 na kuiwezesha Serengeti Boys kushinda bao 1-0 na kujiweka katika nafasi nzuri  ya kufuzu fainali za Afrika mwakani zitakazofanyika nchini Morocco.

Pambano la timu hizo lilifanyika jana kwenye uwanja wa Taifa na kushuhudia vijana wa Serengeti Boys wakikaribia kurejea rekodi iliyowekwa na kaka zao wa timu hiyo mwaka 2004 walipotinga fainali kabla ya kung'olewa kwa kosa la kuchezesha 'kijeba' Nurdin Bakar.

Bao hilo pekee la Sengereti lilipatikana dakika mbili tu baada ya kipa Peter Manyika Peter kudaka vyema mpira wa kichwa uliopigwa na Ibara Vinny kutoka karibu na lango uliokuwa ukionekana kuelekea golini kuitanguliza Kongo mbele.

Wageni waliokuwa wamewazidi 'mno' vijana wa Serengeti kutokana na muonekano wao wa 'miili jumba',  walicharuka baada ya goli hilo na kufanya mashambulizi mfululizo huku wakitawala sehemu kubwa ya mchezo huo ambao ni wazi kuwa matokeo yangekuwa vinginevyo kama si uhodari wa Manyika aliyestahili tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Ushindi uliiweka Serengeti katika mazingira mazuri ya kuandika historia kwa kufuzu kihalali kwa fainali za Afrika kwa mara ya kwanza ikiwa watafanikiwa walau kuambulia sare katika mechi yao ya marudiano itakayochezwa Brazzavile wiki mbili zijazo.

Serengeti waliwahi kufuzu kwa fainali hizo lakini wakaondolewa baada ya kukutwa na hatia ya kuchezesha wachezaji wenye umri mkubwa, lakini safari hii wamepata mteremko na kunusa fainali zitakazofanyika mwakani nchini Morocco baada ya wapinzani wao wa awali kujitoa na sasa kubakiwa na kazi ya kuitoa Congo tu ili itinge kwa fainali hizo.

Basile Erikiki, kocha wa Congo aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu dakika mbili kabla ya kumalizika kwa kosa la kumbwatukia refa akiwa karibu na mstari wa uwanja, aliipongeza Serengeti kwa kuonyesha ushindani mkali na soka la kasi, lakini akijipa matumaini ya kusonga mbele kwa kudai kuwa vijana wake watajirekebisha kwa kutumia vyema nafasi watakazopata katika mechi ya marudiano tofauti na ilivyokuwa jana.

Ticha wa Serengeti, Jacob Michelsen, amewasifu vijana wake kwa kuibuka na ushindi katika mechi aliyokiri kwamba ilikuwa ngumu kwa kila upande.
"Ila bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kutimiza lengo la kuwatoa wapinzani wetu (Congo) na kusonga mbele," alisema Michelsen.

Vikosi: Peter Manyika, Miza Abdallah, Mohamed Mohamed, Ismail Gambo, Miraji Adam, Mudathir Abbas, Mohamed Haroub, Joseph Lubasha/Dickson Ambundo (dk.60), Hussein Ibrahim, Selemani Bofu/Tumaini Mosha (dk. 76) na Farid Shah.

Congo Brazzavile: Ombandza Mpea, Imouele Ngampio, Mabiala Charlevy, Okombo Francis, IOndongo Bowrgema, Ibara Vinny, Binguila Bardry, Obassi Ngatsongo, Mohendiki Brei, Atoni Mavoungou na Biassadila Arci.