Kikosi cha timu ya Ruvu Shooting ambacho jana kilimaliza duru la kwanza kwa ushindi wa mabao 2-0 |
UONGOZI wa klabu ya Ruvu Shooting umesema utatumia mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara kukiimarisha kikosi ili waweze kufanya vema katika duru lijalo la ligi hiyo.
Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alisema yapo mapungufu waliyoyaona katika duru la kwanza lililohitimishwa jana kwa mchezo dhidi yao na Prisons-Mbeya na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 watayarekebisha ili wafanye vizuri duru lijalo.
Bwire, alisema wangependa kuona duru lijalo wakifanya vema zaidi na kujiweka katika nafasi nzuri, licha ya kukiri ndoto za ubingwa ni ngumu kwao kutokana na ushindani uliopo toka kwa klabu kubwa zilizopo nafasi za juu.
"Tutautumia muda wa mapumziko wa ligi kuimarisha kikosi chetu kwa kurekebisha dosari zilizoonekana duru la kwanza, hata hivyo bado ni mapema mno kuweka bayana panga pangua ya kikosi chetu kwa sasa," alisema.
Bwire, alikiri duru la kwanza lilikuwa gumu na lenye ushindani ila anashukuru timu yao ilifanya vema ambapo imemaliza duru hilo ikiwa na pointi 20 ikiwa nafasi ya nane.
"Duru la kwanza lilikuwa gumu na lenye ushindani, kila timu ilionekana kuwa makini kutopoteza pointi kirahisi na kuifanya ligi isitabirike kirahisi," alisema.
Ligi Kuu inayoshirikisha timu 14 kwa sasa ipo mapumzikoni kwa muda wa kama miezi miwili kabla ya kuanza tena duru la pili mapema mwakani.
Mwisho
No comments:
Post a Comment