|
Nahodha wa Ghana, Asamoah Gyan |
MALABO, Guinea ya Ikweta
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Ghana, Christian Atsu anaweza kuwa nguzo muhimu katika mechi ya nusu-fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Guinea ya Ikweta leo kama Asamoah Gyan atashindwa kucheza kutokana na majeraha, mchezaji mwenzake Jonathan Mensah alisema juzi.
"Sote tunafahamu nini Atsu anaweza kukifanya, inasaidia sana kuwa na wachezaji ambao wanaweza kuleta tofauti mchezoni," beki Mensah aliwaambia waandishi wa habari.
"Ana nafasi muhimu katika timu, anafanya kile anachotaka kufanya na anaongezeka ubora siku hadi siku. Tuna furaha yuko katika makali yake hivi sasa na ataisaidia timu."
Atsu (23), alifunga goli kali wakati kikosi cha Avram Grant kilipotinga katika hatua ya nusu-fainali kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Guinea mjini Malabo Jumapili lakini ni lazima wajiandae kuwakabili wenyeji leo bila ya nahodha wao mwenye ushawishi kikosini Gyan.
Baada ya kupona malaria na kufunga goli la dakika za lalasalama la ushindi wa Ghana katika mechi yao ya pili ya hatua ya makundi dhidi ya Algeria, Gyan aliumizwa kwa teke la kurukiwa tumboni kutoka kwa kipa wa Guinea, Naby Yattara.
Wakati Gyan akiwa shakani katika mechi ya nusu-fainali leo, Mensah anaamini Atsu, ambaye yuko kwa mkopo Everton akitokea katika klabu yake ya Chelsea, anaweza kufunika kutong'aa kwake kwenye ngazi ya klabu na kutamba kwenye timu ya taifa.
"Hisia inakuwa ni tofauti anapoichezea Everton. Tunamuachia anafanye kile anachoweza vyema, ni timu tofauti kabisa," alisema Mensah.
"Timu hii ya Ghana haina mfungaji maalum wa magoli, sote tunafunga tunapopewa nafasi, hilo ni jambo ambalo linalotusaidia sana."
Huku akisifu kuongezeka ubora kwa Atsu, Mensah pia alielezea umuhimu wa Gyan kwenye kikosi cha Black Stars.
"Ndani na nje ya uwanja Gyan ni kiongozi, yeye ni nahodha wa timu na wakati wowote anaokuwapo uwanjani huthibitisha yeye ni kiongozi wa kweli," alisema.
"Yeye ni mshambuliaji bora barani Afrika hivyo wakati wowote anaokuwapo uwanjani ni kama jumlisha mbili kwenye timu.
"Anajisikia maumivu. Amefadhaika sana, kwa sababu ndiyo kwanza alikuwa ameanza kurejea katika makali na kisha majeraha haya yamekuja. Tumezungumza na morali yake iko juu, lakini wakati huohuo hayuko fiti kwa asilimia 100.
"Yeye ni bonge la kiongozi na hata pale asipofunga, au kupata fursa ya kufunga, wakati wote hufanya kazi kwa ajili ya timu. Yeye ndiye kinara wetu na tuna furaha kuwa naye," aliongeza.
Iwapo Ghana wanaing'oa Guinea ya Ikweta na kukutana na Ivory Coast watarejesha kumbukumbu ya Fainali za mwaka 1992 zilizozikutanisha timu hizi na Ivory Coast kushinda kwa mikwaju ya penati.