Jokha Kassim
Na Kambi Mbwana, Dar es Salaam
UKIPATA bahati ya kuusikia wimbo wa Riziki Mafungu
Saba, hakika utaanza kuupenda muziki wa taarabu, hata kama
awali hujaupenda.
Ni wimbo mzuri. Wenye mashairi mazito na yenye
ujumbe murua, unaoelezea jinsi riziki zinavyopangwa na Mungu na wala sio
binadamu, wakiwamo wenye roho mbaya.
Wimbo huo umeimbwa na mwanamama Jokha Kassim,
alipokuwa na kundi zima la Zanzibar Stars Modern Taarab.
Kwa sasa Jokha anafanya kazi katika kundi zima la
Tanzania Moto Modern Taarab, maarufu kama
T-Moto, lenye wakali wengine kibao.
Tayari Jokha amerekodi wimbo unaokwenda kwa jina
la ‘Domo la Udaku’, ukiwa ni ujio mpya wa kundi hilo la taarabu nchini.
Mwimbaji huyo juzi alifanya mazungumzo na Fiesta
Magazine na kusema kuwa muziki ni kipaji chake, alichobarikiwa na Mungu.
Cheche zake zilianza kuonekana tangu zamani,
alipokuwa hodari sana
wa kuimba nyimbo mbalimbali za taarabu.
“Muziki huu ni kipaji changu, tangu zamani
niliweza kuimba kwa ufanisi na kushangaza wengi waliokuwa wakiona mahala
popote.
“Nashukuru, leo hii nimeweza kufanya juhudi na
kufika T-Moto, ikiwa ni baada ya kujulikana nilipofanya kazi na Zanzibar Stars kwa
mafanikio makubwa,” alisema.
Licha ya kuanza zamani kuimba, lakini alianza
kuingia kwenye kundi la muziki mwaka 2002, alipohitajiwa na uongozi wa Zanzibar
Stars na kumtambulisha kimuziki.
Kilichomkwamisha kuingia mapema kwenye sanaa ni
kukatazwa na wazazi wake, hivyo kusubiri hadi mwaka huo alipoanza kushika
kipaza sauti na kurindimisha sauti yake.
Jokha alikuwa mke wa kwanza wa Mfalme, Mzee
Yusuph, ila kwa sasa wameachana na kila mmoja anaishi kivyake.
Siku chache baada ya kuachana na mzee Yusuph, hamu
ya kuimba ilimtesa, hivyo kuamua kufanya harakati za kuibua kipaji chake.
Jokha na Mzee Yusuph wamezaa mtoto mmoja, ambaye
pia ni mwimbaji na Mkurugenzi wa kundi la Jahazi Modern Taarab.
“Nilifanya kazi ya ziada kuingia kwenye muziki,
maana baba yangu hakupenda suala hilo,
hivyo kunipa wakati mgumu.
“Hata hivyo Mungu akipanga lake hakuna
wa kuweza kutengua, ndio maana nimeweza kufika hatua hii na kujulikana sehemu
kubwa kupitia soko la muziki wa taarabu,” alisema.
Mwimbaji huyo mwenye mvuto wa aina yake,
anashindwa kubainisha chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake na mume wake Mzee
Yusuph.
Anasema riziki imekwisha kwa ndoa yao, huku akisema bado
wanaheshimiana kwasababu wameachana bila kuwa na ugomvi, huku wakifanikiwa
kupata mtoto mmoja, aliyepewa jina la Yusuph Mzee Yusuph.
Muziki wa taarabu unazidi kufanya vizuri kutokana
na waimbaji wake wengi kuwa wabunifu.
Katika hilo
anaamini kuwa mambo yatazidi kuwa mazuri, huku mashabiki wakipata vitu adimu
kutoka kwao.
Mwimbaji huyo anavutiwa na mkali wa muziki huo
nchini, Zuhura Shaaban.
Katika kundi lake la T-Moto, Jokha ameimba nyimbo
zaidi ya tatu, ukiwamo wa ‘Unavyojidhani Haufanani’ ‘Mimi ni Star’ na
‘Aliyeniumba Hajanikosea’, ambao ulibeba jina la albamu ya kwanza.
Kwa albamu hii mpya inayoandaliwa, Jokha
amesharekodi wimbo mmoja unaokwenda kwa jina la Domo la Udaku.
Katika hilo,
ni wazi kuwa wao watakuwa juu zaidi, maana bendi nyingi zimekosa ubunifu na
mikakati ya kimuziki.
“Kwenye muziki kumekuwa na ushindani, hivyo
nadhani kinachotakiwa ni mipango, mikakati pamoja na nyimbo nzuri.
“Sisi tunavyo vitu hivyo, nadhani ni wakati wetu
kuwa kileleni maana mashabiki wana kiu ya kuona mambo yetu yanakuwa mazuri,”
alisema.
Jokha alizaliwa miaka kadhaa iliyopita, Zanzibar, katika Hospitali
ya Mnazi Mmoja.
Elimu ya Msingi aliipata katika shule ya Darajani
na kuhitimu mwaka 1995 ile ya Sekondari aliipata kwenye shule ya Haile Selasi.
Mbali na Jokha, wengine wanaopatikana kwenye kundi
hilo ni pamoja na Nyawana Fundikira, Aisha Masanja, Shimuna Kassim, Amina
Rashid, Hanifa Juma, Shaban Ramadhan, Mrisho Rajabu, Rahma Omari, Silver
Mwandilee, Kasikile Msukule na wengineo.
You might also like: