Mkurugenzi wa Michezo, Leonard Thadeo |
SERIKALI kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imemaliza kupitia Rasimu ya Katiba ya klabu ya Simba kwa ajili ya kuidhinisha katiba hiyo na kuifanya klabu hiyo kuendelea na taratibu za uchaguzi mkuu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Leonard Thadeo alipokutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali za waandishi leo jijini Dar es Salaam.
Akijibu moja ya hoja iliyomtaka kufafanua Wizara imefikia wapi katika upatikanaji wa Katiba ya Klabu ya Simba Bw. Thadeo amesema kuwa upitiaji wa Katiba umemelizika na kuonekana kuwa na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha katiba hiyo.
“Mchakato wa upitiaji wa Katiba ya klabu ya Simba umemalizika jana lakini kumekuwepo na mapungufu machache yanayohitaji kurekebishwa ili Wizara iweze kuidhinisha Katiba hiyo” amesema Bw. Thadeo.
Akifafanua zaidi Bw. Thadeo amesema kuwa mapungufu hayo yanalenga zaidi upande wa kisheria ambapo mtu anaweza kutafsiri neno vibaya hivyo kupata maana tofauti na Katiba ilivyokusudia hivyo kuitaka klabu hiyo kufanya marekebisho hayo mapema na kurejesha Katiba hiyo Wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa.
Aidha Bw. Thadeo amewataka waandishi wa habari pamoja na wanachama wa klabu ya Simba kuwa na subira ili waweze kupata Katiba itakayokidhi malengo ya klabu yao kwani mchakato wa upitiaji wa Katiba ulihitaji umakini.