STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, March 15, 2013

Falcon yakiona cha moto Ligi Kuu ya Zenji

 
TIMU ya soka ya Bandari ya Zanzibar jana iliifumua bila huruma Falcon pia ya visiwani humo katika pambano kali la Ligi Kuu ya Grand Malt ya Zanzibar iliyochezwa kwenye uwanjwa wa Amaan.
Chini ni baadhi ya matukio ya pambano hilo katika picha kama zilivyopigwa na Martin Kabemba.
 







 

ROBO FAINALI MABINGWA ULAYA WAHISPANIA WATENGANISHWA


  Ratiba ya mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopangwa leo mchana.

MONACO, Ufaransa
RATIBA ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imetangazwa mchana wa leo huku timu tatu za Hispania na mbili za Ujerumani zikitenganishwa bila kukutana wenyewe kwa wenyewe.
Hispania imeingiza timu tatu katika hatua hiyo ambapo ni mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo Real Madrid, Barcelona na Malaga wakati Ujerumani inafuatia ikiingiza klabu mbili za Bayern Munich na mabingwa watetezi wa nchini hiyo, Borrusia Dortmund.
Kwa mujibu wa atika ratiba hiyo, Malaga ya Hispania itaanzia nyumbani kuumana na Borussia Dortmund, kama itakavyokuwa kwa Real Madrid, iliyopangwa kukipiga na Galatasaray ya Uturuki iliyo na nyota wa zamani wa Galacticos, Wesley Sneijder na Muivoey Coast, Didier Drogba..
PSG ya Ufaransa itakuwa na kibarua kipevu kilichowashinda AC Milan, wakati watakapowaalika FC Barcelona ya Hispania, huku, Bayern Munich ikitarajiwa kukutana uso kwa uso na ‘Kibibi Kizee cah Turin’ Juventus yha Italia.
Mechi za hatua hiyo mkondo wa kwanza zitachezwa Aprili 2 na 3, ambapo mechi kati ya Malaga dhidi ya Dortmund na ile ya Madrid na Galatasaray zitapigwa Jumanne, huku PSG dhidi ya Barca na ile ya Bayern na Juve itapigwa Jumatano.
Michezo ya marudiano zitachezwa kati ya Aprili 9 na 10, kusaka miamba minne itakayocheza nusu fainali ya michuano hiyo, itakayopigwa mwishoni wa mwezi ujao na kurudiana Mei mwanzoni, kusaka tiketi ya fainali Mei 25 kwenye Uwanja wa Wembley. 
Aidha, ratiba ya michuano ya Europa League pia ilipangwa leo katika hafla hiyo, ambapo Chelsea ya England itatoana jasho na Rubin Kazan ya Russia, huku Tottenham Hotspur ya England ikipimana ubabu na FC Basel Uswisi.
Fenerbache ya Uturuki itakuwa na kibarua dhidi yaLazio ya Italia, huku Benfica ya Ureno ikikamuana na Newcastle ya England. Mechi za kwanza robo fainali hii zitapigwa Alhamisi ya Aprili 4 na marudiano yatakuwa Aprili 11.

Yanga, Ruvu Shooting hapatoshi kesho Taifa



Na Boniface Wambura

LIGI Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho (Machi 16 mwaka huu) kwa mechi tatu ambapo Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma mkoani Mara ndiye aliyepewa jukumu la kuchezesha mechi hiyo namba 146. Adongo atasaidiwa na Anold Bugado wa Singida na Milambo Tshikungu kutoka Mbeya wakati mwamuzi wa mezani ni Hashim Abdallah wa Dar es Salaam.

Mtathmini wa waamuzi ni Army Sentimea wakati Kamishna wa mechi hiyo inayokutanisha vinara Yanga na Ruvu Shooting inayoshika nafasi ya saba ikiwa na pointi 29 chini ya ukufunzi wa Charles Boniface Mkwasa na Msaidizi wake Selemani Mtungwe ni Emmanuel Kavenga kutoka Mbeya.

Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 8,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.

Pia TFF inawaasa washabiki wa mpira wa miguu kuacha kununua tiketi mikononi mwa watu kwa vile wanaweza kuuziwa tiketi bandia. Tiketi zote zitauzwa katika vituo vinavyotangazwa katika magari maalumu, na uwanjani pia katika magari hayo.

Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua washabiki 25,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na Mgambo Shooting kutoka Tanga. Ugumu wa mechi hiyo unatokana na ukweli kuwa timu zote mbili zinapigana kuepuka kurudi zilikotoka (daraja la kwanza).

Mgambo Shooting inayonolewa na Mohamed Kampira inashika nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24 katika ligi hiyo yenye timu 14. Toto Africans ambayo iko nyumbani itaingia uwanjani ikiwa na pointi 14 katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi.

Baada ya kulala 2-1 mbele ya Simba katika mechi iliyopita, Coastal Union itakuwa mgeni wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro.

Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) kwa mechi moja itakayozikutanisha JKT Ruvu na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Azam vitani tena Kombe la Shirikisho, TFF yaitakia heri


Na Boniface Wambura

WAWAKILISHI pekee wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa, Azam wanatarajiwa kushuka dimbani siku ya Jumapili ugenini kuwakabili wenyeji wao Barrack YC II katika pambano la raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeitakia kila la kheri timu hiyo iweze kufanya vema katika pambano hilo la kwanza litakalochezwa mjini Monravia, Liberia.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana wiki mbili zijazo na tayari Azam wameshatua nchini humo wakiwa na matumaini kibao ya kufanya vema katika mechi hiyo ya kwanza.
TFF imesema wanaungana na watanzania wote hususani mashabiki wa Azam kuiombea heri timu hiyo iweze kuipeperusha vema bendera ya Tanzania.
Azam ilipata nafasi hiyo ya kuendelea mbele kwenye michuano hiyo kwa kuinyuka jumla ya mabao 8-1 Al Nasir Juba ya Suadn Kusini walioumana nao katika mechi ya mzunguko wa awali.
Wawakilishi wengine wa Tanzania waliokuwa wakishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba na Jamhuri Pemba zenyewe ziliondolewa katika raundi ya awali na kuiacha Azam wakiendelea kupeta.

Pazia la FDL kufungwa rasmi wikiendi hii


Na Boniface Wambura

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2012/2013 unamalizika wikiendi hii huku timu za Mbeya City ya Mbeya, Ashanti United ya Dar es Salaam na Rhino Rangers ya Tabora zikiwa tayari zimepata tiketi ya kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao.

Kundi A mechi zote zitachezwa Jumapili (Machi 17 mwaka huu) ambapo Majimaji vs Mbeya City kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Kurugenzi vs Mkamba Rangers (Mafinga) na Burkina Faso vs JKT Mlale (Jamhuri, Morogoro).

Kesho (Machi 16 mwaka huu) katika kundi B itakuwa Green Warriors vs Polisi Dar (Karume, Dar es Salaam) na Ndanda vs Villa Squad (Nangwanda Sijaona, Mtwara). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Moro United vs Ashanti United (Karume, Dar es Salaam) na Tranist Camp vs Tessema (Mabatini, Mlandizi).

Kundi C ni kesho (Machi 16 mwaka huu) Polisi Tabora vs Pamba (Ali Hassan Mwinyi, Tabora). Keshokutwa (Machi 17 mwaka huu) ni Polisi Mara vs JKT Kanembwa (Karume, Musoma), Polisi Dodoma vs Mwadui (Jamhuri, Dodoma) na Rhino Rangers vs Morani (Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

TFF yatoa mkono wa rambirambi kifo cha Muyeshi



Na Boniface Wambura

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha aliyekuwa Ofisa Habari wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi kilichotokea juzi (Machi 13 mwaka huu) jijini Nairobi, Kenya baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Muyeshi aliitumikia CECAFA kwa muda mrefu, hasa katika kuhakikisha waandishi wa habari wanapata mazingira mazuri ya kufanyia kazi wakati wanaporipoti matukio mbalimbali ya Baraza hilo.

Alitoa mchango mkubwa katika eneo la habari za mpira wa miguu, tangu akiwa gazeti la East African Standard la Kenya akiwa mwandishi, na baadaye Mhariri wa Michezo kabla ya kujiunga na CECAFA, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu Muyeshi, CECAFA, Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) na tasnia ya habari kwa ujumla, na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Muyeshi mahali pema peponi. Amina


TFF yaondoa free pass viwanjani, kisa mapato kiduchu

Viongozi wakuu wa TFF, Rais Leodger Tenga na Katibu Mkuu, Anegtile Osiah

Na Boniface Wambura

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeondoa utaratibu wa wadau wake kuingia bure kwenye mechi kwa kutumia tiketi maalum (free pass).

Kutokana na uamuzi huo hakutakuwa tena na pasi za bure kwa ajili ya kushuhudia mechi zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa TFF katika viwanja mbalimbali nchini.

Uamuzi huo umetokana na ukweli kuwa free pass zimekuwa zikipunguza au kuchukua mgawo wote wa TFF kwenye mechi, na wakati mwingine Shirikisho hulazimika kutoa fedha za ziada kugharamia pasi hizo.

Pasi zote ambazo imekuwa ikitoa kwa wadau wake hukatwa katika mgawo wa TFF katika mechi husika. Shirikisho hivi sasa linapata asilimia nne tu ya mapato katika mechi za Ligi Kuu, ligi ambayo hivi sasa inaendeshwa na Kamati yake ya Ligi.


Kumekucha pambano la Cheka na Mashali


MAANDALIZI ya pambano la ndondi la kimataifa la kuwania ubingwa wa IBF-Afrika baina ya bingwa mtetezi, Francis Cheka 'SMG' na Thomas Mashali 'Simba Asiyefugika' yamepamba moto ikiwamo kutangazwa watakaowasindikiza.
Cheka na Mashali watavaana katika pambano hilo la uzani wa Super Middle la raundi 12 Mei Mosi kwenye ukumbi wa PTA jijini Dar es Salaam na litasindikizwa na mapambano manane ya utangulizi likiwamo la ndugu wa mabondia hao.
Kwa mujibu wa waratibu wa pambano hilo, mabondia ndugu wa Cheka na Mashali watakaopigana siku hiyo ni Cosmas Cheka dhidi ya Charles Mashali.
Mapambano mengine ya utangulizi siku hiyo ni pamoja na lile la mtoto wa nyota wa zamani wa masumbwi nchini na Afrika, Rashid Matumla, Mohammed Matumla atakayepigana na Bakari Dunda.
Michezo mingine itawakutanisha Jonas Segu dhidi ya Adam Ngange, Ibrahim Class atakayepigana na Amos Mwamakula na Khalid Shomari atakayepimana ubavu na Mahinya Ramadhani.
Pia bondia Mustafa Dotto atapigana na Abdallah Juma, kabla ya Yusuf Jibaba kuchapana na Shaaban Mhamila na Ramadhani Mkundi dhidi ya Kassim Mbundike.
Taarifa ya waratibu hao inasema kwa sasa wanaendelea kufanya mchakato wa kumpata mgeni rasmi katika pambano hilo kubwa ambalo litamaliza ubishi baina ya Cheka na Mashali ambao hawajawahi kukutana.

Afisa habari CECAFA afariki dunia

Finny Muyeshi (kushoto) enzi za uhai wake (Picha: NATION)

AFISA Habari wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Finny Muyeshi, amefariki dunia juzi Jumatano usiku.
Akizungumza kwa njia ya simu jana kutoka Nairobi, Kenya, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye, alisema kuwa marehemu Muyeshi alifariki akiwa kwenye hospitali ya Coptic iliyoko jijini humo.
Musonye alisema kuwa marehemu Muyeshi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa figo ambao ndiyo umesababisha kifo chake.
Alisema kuwa CECAFA imepata pigo la kuondokewa na afisa huyo ambaye alikuwa ni mmoja wa watendaji wa sekretarieti kwa muda wote.
"Tumeondokewa na kiongozi wetu, ni pigo kwa CECAFA na ni pigo kwa soka la ukanda huu, alikuwa ni zaidi ya afisa habari katika maendeleo ya kila siku," alisema Musonye.
Aliongeza kuwa jana jioni alitarajia kushiriki kikao cha familia kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi ya kiongozi huyo.
Marehemu Muyeshi ambaye ni Mkenya ameitumikia CECAFA kwa zaidi ya miaka 10 akiwa ni msaidizi wa Musonye katika kusimamia mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) pamoja na michuano ya Kombe la Chalenji ambayo hufanyika kila mwaka katika ukanda huu.
Kutokana na kusumbuliwa na maradhi hayo, hakuweza kuitumikia CECAFA tangu mwaka juzi.
Kufuatia hali hiyo, Afisa Habari wa Chama cha Soka cha Uganda (FUFA), Rogers Mulindwa, alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi. Ameen.


CHANZO:NIPASHE



Stars, Morocco kuvaana kwenye jua kali

Hekaheka wakati mechi ya Taifa Stars na Morocco mwaka juzi

MECHI ya Kundi C ya kuwania kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia kati ya timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi 24 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam itachezwa kuanzia saa 9:00 kamili mchana.
Akizungumza jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba, alisema kuwa lengo la kupanga muda huo ni kunufaika na hali ya hewa ya iliyopo (ya joto) kulinganisha na wageni (Morocco) ambao wachezaji wao wengi wanatoka barani Ulaya ambako baadhi ya maeneo yake hivi sasa yana baridi kali.
Kawemba alisema kuwa kwa sababu hiyo, watu wa benchi la ufundi wanaamini kwamba muda huo utawanufaisha zaidi Stars ambayo inaundwa na wachezaji wengi wanaoishi jijini Dar es Salaam na kuzoea hali ya joto la jua la mchana.
"Kule wanakotoka (wachezaji wa Morocco) hivi sasa kuna baridi kali na hivyo kwa muda huo kwetu tunaweza kunufaika," alisema kiongozi huyo ambaye aliongozana na kocha wa Stars, Kim Poulsen, kwenda mjini Marakech wiki iliyopita kuipeleleza Morocco iliyokuwa ikicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mali.
Aliongeza vilevile kuwa Morocco wanatarajiwa kutua nchini Alhamisi (Machi 21) kwa ndege ambayo itapitia Dubai kabla ya kutua jijini Dar es Salaam.
Kikosi kitakachoivaa Morocco kinatarajiwa kuingia kambini Jumamosi lakini kitakuwa kamili ifikapo Jumanne baada ya nyota wake wawili wanaocheza TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, watakapotua nchini siku hiyo pamoja na wachezaji wa Azam ambao watakuwa wamerejea nchini kutoka Liberia.
Katika kujiandaa na mechi hiyo Februari 6 mwaka huu, Stars ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon ambapo ilishinda bao 1-0.
Mbali na Stars kuivaa Morocco, mechi nyingine ya Kundi C itakuwa ni kati ya Ivory Coast watakaowakaribisha Gambia.
Stars yenye pointi tatu inahitaji ushindi ili kuendelea kuwa kwenye nafasi nzuri ya kufuzu katika kundi hilo linaloongozwa na Ivory Coast yenye pointi nne, Morocco (pointi mbili) na Gambia wanaoshika mkia wakiwa na pointi moja.
Tanzania haijawahi kufuzu fainali za Kombe la Dunia. Mara ya kwanza na ya mwisho Stars kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ilikuwa mwaka 1980 ambapo Rais wa TFF anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga ndiye aliyekuwa nahodha wake.

Adebayor aivusha Spurs robo fainali, Chelsea, Newcastle wawafuata



Adebayor akipongezwa na mchezaji mwenzake baada ya kufunga bao jana

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo, Emmanuel Adebayor jana aliiwezesha timu yake ya Tottenham Hotspurs kufuzu Robo Fainali ya michuano ya Ligi ndogo ya Ulaya (Europa League) baada ya kufunga bao dakika za nyongeza dhidi ya Inter Milan.
Adebayor ni kama aliwanyamazisha mashabiki wa wenyeji waliomdhihaki katika mechi hiyo kwa kumuiitia ndizi wakimfananisha na nyani kwa kufanya matokeo ya mwisho wa pambano hilio lililochezwa Italia kuisha kwa Inter kushinda 4-1.
Hata hivyo matokeo hayo hayakuiwezesha timu hiyo ya Italia kusonga mbele baada ya kuchezea kichapo cha mabao 3-0 katika mechi ya awali wiki iliyopita na matokeo ya jumla kuwa mabao 4-4.
Spurs ambayo ilimkosa winga wake nyota, Garreth Bale inasonga mbele kwa faida ya bao la ugenini lililofungwa na Adebayor.
Mabao yaliyotishia kuing'oa Spurs kabla ya kwenda muda wa ziada yalifungwa na Cassano dakika ya 20, Palacio dakika ya 52 kabla ya William Gallas kujifunga dakika ya 75 na kufanya dakika 90 mechi hiyo kuisha kwa Inter kushinda mabao 3-0.

Katika muda wa ziada Adebayor aliiandikia Spurs bao dakika ya 96 kabla ya Inter kuchomoa dakika nne baadaye na kufanya hadi dakika ya 120 matokeo kuwa mabao 4-1 Inter wakiibuka kidedea.
Katika mechi nyingine za michuano hiyo ya Ulaya, Newcastle United ilipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Anzhi Makachkala, Chelsea nayo ikipata ushindi wa mabao 3-1 na kuing'oa Steaua Bucharest.
Mabao ya Chelsea iliyochezea kichapo cha bao 1-0 ugenini yalifungwa na Mata dakika ya 33, John Terry mabao 58 na Fernando Torres dakika ya 71 wakati bao la kufutia machozi la wageni, liliwekwa kimiani na Chiriches aliyefunga dakika ya 45.
Matokeo mengine ya mechi za michuano hiyo iliyochezwa usiku wa jana ni kama ifuatavyo; Lazio iliifunga Stuttgart mabao 3-1 magoli yake yote yakifugwa na Libor Kozak na kufuzu robo fainali kwa jumla ya mabao 5-1, Fenerbahçe ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Victoria Plzen na Fenerbahce kusonga kwa ushindi wa mabao 2-1.
Benfica ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Bordeaux na kufuzu hatua hiyo kwa jumla ya mabao 4-2, huku Rubin Kazan ikisubiri muda wa nyongeza kuing'oa Lavente kwa mabao 2-0 na Zenit licha ya kushinda nyumbani bao 1-0 iling'oka kwa Basel baada ya awali kufungwa mabao 2-0 na hivyo kutoka kwa mabao 2-1.
Kwa matokeo hayo timu zilizotinga hatua hiyo ni hizi zifuatazo:
Newcastle United, Chelsea na Tottenham Hotspurs zote za Uingereza, Lazio ya Italia, Fenernahce ya Uturuki, Benfica ya Ureno, Robin Kazan ya Russia na Fc Basel ya Uswisi.