STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Wednesday, March 4, 2015

TFF yaijibu Yanga kuhusu kinda la Simba

http://i1.wp.com/millardayo.com/wp-content/uploads/2015/01/Jerry-Muro.jpg
Jerry Muro
BAADA ya uongozi wa Yanga kudai kuhujumiwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), bodi hiyo imewajibu wanajangwa kwamba 'Mkuki kwa Nguruwe, kwa binadamu mchungu'. Mapema leo, uongozi wa Yanga umetishia kutoingiza timu uwanjani katika mechi yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Ruvu Stars iliyopangwa kuchezwa Uwanja wa Taifa Machi 11, kutokana na kile ulichodai kutoshirikishwa katika uamuzi wa mabadiliko ya ratiba.
Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga, amesema jijini hapa leo kuwa uongozi wa Yanga ulikuwa unatambua kwamba kikosi chake kingecheza dhidi ya JKT Ruvu leo kabla ya kuivaa Simba SC Jumapili, lakini kimeshangaa baada ya kusoma kwenye mitandao kwamba mechi yao dhidi ya JKT Ruvu Stars haipo.
Hata hivyo, Fatma Shibo, Kaimu Ofisa Mtendaji wa TPLB, amesema mabadiliko ya ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara hayajafanywa kwa siri na yametokea kutokana na ushiriki wa timu nne za ligi hiyo, Azam FC, Mtibwa Sugar FC, Simba SC na Yanga katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mapema mwaka huu. Fatma amekanusha madai ya Yanga kwamba mechi yao dhidi ya JKT Ruvu Stars wanayodai ilipangwa kuchezwa leo kwamba yamefanywa kwa siri, kwa vile uongozi wa wanajangwani ulitaarifiwa tangu Febuari 16 juu ya mabadiliko ya ratiba ya ligi.
"Mabadiliko ya ratiba ya ligi kuu yametokea kutokana na ushiriki wa timu nne za Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar Januari mwaka huu," Fatma amesema.
"Hili la pili la Yanga kudai hatukuwashirikisha katika kupangua mechi yao dhidi ya JKT Ruvu si kweli kwa sababu tuliwasiliana na uongozi wa Yanga tangu Februari 16. Labda wawe na tatizo la kutofungua email, lakini Katibu Mkuu wao (Jonas Tiboroha) alisema aliona email yetu kuhusu suala hilo," amesema zaidi Fatma.
Ofisa huyo amesema bodi haina njama zozote za kuihujumu Yanga katika mechi zake kwani waliibeba pia katika kuilazimisha Tanzania Prisons irejeec Mbeya kutoka Dar es Salaam kucheza dhidi yao mechi waliyoshinda 3-0 jijini Mbeya juzi.
"Kama ni watu wa kulalamika, walipaswa kulalamika Prisons kwa sababu walikuwa hapa Dar es Salaam, lakini tukawaambia warejee kwao Mbeya kucheza dhidi ya Yanga baada ya uongozi wa Yanga kutuomba wacheze mechi zao zote zsa Mbeya kabla ya kwenda Botswana. "Mpaka sasa bodi inadaiwa pesa ya gharama za usaffiri na timu ya Prisons kwa sababu tuliwafanya wasafiri mara mbili kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kurudi tena hapa Dar es Salaam," amesema zaidi Fatma.
Katika hoja zake, Muro amedai TPLB ni janga la kitaifa na kwamba kusogezwa mbele kwa mechi hiyo dhidi ya kikosi cha Felix Minziro cha JKT Ruvu, ni hujuma dhidi ya Yanga  kwa kuwa timu hiyo ya Jangwani jijini hapa itakuwa na siku mbili tu za kupumzika baada ya kucheza dhidi ya maafande hao kabla ya kuivaa Platinum ya Zimbabwe katika mechi yao ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika Jumamosi.
Huku akihoji kiwango cha elimu cha Kaimu Ofisa Mtendaji wa TPLB, Fatma na watendaji wengine wa bodi hiyo, Muro amesema tayari uongozi wa Yanga umewasilisha barua TFF tangu jana kusaka ufafanuzi wa mabadiliko ya ratiba hiyo.
“Kwa sasa mpinzani wetu ni Azam FC na siyo Simba, mechi dhidi ya Simba kwetu ni kwa sasa kama bonanza, siyo kipaumbele chetu, sisi tunawasubiri siku hiyo ifike tucheze nao, lakini hawana jipya kwa tunawazidi pointi nyingi,”ametamba Muro.
"Azam kesho na keshokutwa tunamwacha mbali maana mpaka sasa tuko mbele yake kwa pointi nne katika msimamo wa ligi, sisi wapinzani wetu na klabu ambazo unaweza kuzilinganisha na sisi ni Kaizer Chief ya Afrika Kusini au TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambazo zinacheza michuano ya kimataifa," amesema zaidi Muro

Pep Guardiola hana mpango wa kuhama Bayern

http://www.predapublishing.com/the-sportist/wp-content/uploads/2014/10/pg-68-garside-pa.jpgKOCHA wa klabu ya Bayern Munich, Pep Guardiola amesema hana mpango wowote wa kuikacha timu hiyo mwishoni mwa msimu kufuatia kuzuka tetesi kuwa anataka kuhamia Manchester City.
Mkataba wa Guardiola na mabingwa hao wa Bundesliga unatarajiwa kumalizika majira ya kiangazi mwaka 2016 lakini mazungumzo ya mkataba mpya yamesimamishwa hatua iliyozua minong’ono ya kuondoka.
Hata hivyo, Guardiola ameweka wazi kuwa bado anataka kuendelea kuinoa Bayern na hajafanya mazungumzo na klabu nyingine yeyote.
Akihojiwa Guardiola amesema hajapokea ofa yeyote kutoka kwa City kwa klabu nyingine kwani matumaini yake ni kubakia Bayern kwa kipindi kirefu.
Guardiola aliendelea kudai kuwa kwa sasa bado ana mkataba na Bayern na anapenda kuheshimu hilo mpaka hapo watakapokaa tena na kuzungumza juu ya mkataba mpya.

Air Jordan nouma! awafuka wanamichezo wote duniani

https://usatftw.files.wordpress.com/2014/09/ap_britain_ryder_cup_golf_67543664.jpg?w=1000&h=736MCHEZAJI mkongwe wa mpira wa kikapu nchini Marekani, Michael Jordan 'Air Jordan' ameendelea kuweka rekodi katika vitabu hata baada ya kustaafu mchezo huo baada ya kutajwa kama mwanamichezo pekee aliyechomoza katika orodha ya mabilionea ulimwenguni.
Wakati akicheza kikapu katika ligi maarufu nchini Marekani NBA, Jordan aliweka rekodi mbalimbali kutokana na umahiri pindi anapokuwa uwanjani lakini hali hiyo imebadilika kwani hivi sasa ameonyesha kuwa mahiri kibiashara pia.
Jordan mwenye umri wa miaka 52 ametajwa kushika nafasi ya 1,741 katika orodha ya watu matajiri duniani ambayo hutolewa na jarida la Forbes kila mwaka akiwa mwanamichezo pekee kuchomoza katika orodha hiyo.
Nguli amepata utajiri mkubwa kutokana na kuingia mkataba na kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike ambao ulimuingizia zaidi ya dola bilioni 2.25 mwaka 2013 pamoja na kumiliki hisa asilimia 89 zenye thamani ya dola milioni 700 katika timu ya Charlotte Hornets.

Prisons yamfurusha Mwamaja, Makatta amrithi

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjaJrEavPqz6tdbaPJoZmvtYQffdUBf8ZB4pv78v6DDUEKBlffZJyhLOcc-KGwJFL0hn5CO0P6O5Fj_T_zQU8jrYulHMFe7oQSEzt6e49kVAVtP6uu4macHTa9l2xDasmWECDTPulRIcOs/s1600/mwamaja.JPG
Kocha David Mwamaja aliyesitishiwa mkataba wake na Prisons-Mbeya
KLABU ya Prisons Mbeya imemtimua aliyekuwa Kocha wao mkuu, David Mwamaja na nafasi yake imechukuliwa na Mbwana Makatta aliyewahi kuinoa timu hiyo siku za nyuma.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Prisons, Hassain Yusuph alithibitisha kusitishiwa mkataba kwa kocha Mwamaja na kunyakuliwa kwa Makatta aliyekuwa akiinoa timu ya Ligi Daraja la Kwanza, Oljoro JKT.
Timu hiyo ndiyo inayoburuza mkia katika msimamo wa ligi hiyo wakikusanya pointi 14 tu baada ya jioni ya leo kulazimisha sare ya 0-0 na JKT Ruvu kwenye mchezo uliochez a kwenye uwanja wa Chamazi.
Hassain alisema kuwa mabadiliko hayo yamefanywa kutokana na kocha Mwamaja kushindwa kuiweka pazuri timu hiyo na kocha mpya atainoa timu hiyo kwa kipindi chote kilichofuata cha kumalizia ligi.

Mtibwa Sugar yazinduka, Ndanda yaiua Ruvu

Mtibwa Sugar waliozinduka
Polisi Moro waliokubali kichapo mbele ya Mtibwa leo
TIMU ya Mtibwa Sugar wametakata kwenye uwanja wa nyumbani baada ya kuicharaza Polisi Moro kwa mabao 2-1 katika pambano lililochezwa uwanja wa Manungu Complex
Mtibwa ambao kwa muda mrefu walikuwa hawajashinda walipata mabao yake kupitia kwa Ally Shomari na Said Mkopi baada ya awali wageni wao kuitangulia kufunga bao kwa mkwaju wa penati kupitia Said Bahanuzi.
Kwa ushindi huo Mtibwa wamepanda hadi katika nafasi ya tano wakifikisha pointi 22.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo Ndanda Fc ya Mtwara iliitambia nyumbani Ruvu Shooting kwa kuilaza mabao 2-1 katika pambano kali lililochezwa uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani.
Ndanda walianza kuandika bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza jingine kupitia kwa Omega Seme na wenyeji Ruvu walijipatia bao la kufutia machozi dakika za lala salama.
Bao hilo lilifungwa na Yahya Tumbo na kuifanya Ndanda kufikisha pointi 19 wakati Ruvu wakiswaliwa na pointi 21.
Ligi hiyo itaendelea tena siku ya Jumamosi na Jumapili kutakapochezwa pambano la watani wa jadi Simba na Yanga.