STRIKA

STRIKA

USILIKOSE

USILIKOSE

Friday, February 22, 2013

ASLAY AKIACHIA VIDEO 2, MUGOGO, DULLA YEYO WANA KIMODO



Dogo Aslay

WAKATI msanii Dogo Aslay kuiachia video za nyimbo zake mbili za 'Utachezaje' na Wahenga aliyoimba na Ally Nipishe, wakali wengine wa Kituo cha Mkubwa na Wanae, Mugogo na Duila yeyo wameana kupika wimbo wao mpya uitwao 'Kimodo'.
Meneja wa wasanii hao, Said Fella aliiambia MICHARAZO kuwa, wimbo huo mpya umefanywa chini ya prodyuza Shirko na unakuja baada ya kazi yao ya 'Wameweka' kufanya vema kwenye vituo cha radio na runinga tangu wautoe hadharani.
Fella, alisema kwa sasa wimbo huo unamaliziwa kurekodiwa kabla ya kusambazwa ili kurushwa hewani kuwapa raha mashabiki wa muziki nchini.
Aidha Fella alisema msanii Dogo Aslay ameziachia hewani video zake mbili za 'Utachezaji' na 'Wahenga' baada ya kuzisambaza wakati mkongwe Hija Cheka 'Bibi Cheka' akiendelea na mchakato wake wa kurekodi video ya wimbo wake mpya na wa tatu wa 'Nalia'.
"Bibi Cheka yeye anarekodi video ya wimbo wake wa 'Nalia' alioufanya kwa Shirko, huku Dogo Aslay akiachia video za nyimbo zake mbili za 'Utachezaje' na 'Wahenga' aliomshirikisha Ally Nipishe chini ya ufadhili wa watu wa Italia," alisema Fella.
Fella alisema wakati wasanii hao wakiendelea na michakato ya kutoa kazi zao mpya, kituo chao bado kinaendelea na utaratibu wa kuwatoa wasanii mmoja mmoja.

Mkurugenzi wa Mkubwa na Wanae, Said Fella

GOLDEN BUSH USO KWA USO NA CLOUDS FC


Kikosi cha Golden Bush Veterani wakiwa na kocha wao, Madaraka Selemani.

WAKALI wa kutatandaza soka mkoa wa Dar es Salaam, Golden Bush Veterani jioni ya leio inatarajiwa kushuka dimbani kuvaana na kikosi cha kituo maarufu cha redio nchini Cloud's Fm, 'Clouds Fc.
Pambano hilo la kirafiki ambalo linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka wa jijini kutokana na tambo za pande zote mbili litachezwa kwenye uwanja wa Tanganyika Packers kuanzia saa 10:30 jioni.
Kwa mujibu wa Mlezi wa Golden Bush, Onesmo Waziri 'Ticotico' ni kwamba kikosi chao tangu Jumatatu walikuwa kambini katikati ya jiji wakijiandaa na pambano hilo baada ya kupoteza mechi yao mwishoni mwa wiki dhidi ya Survey ya Chuio Kikuu.
Ticotico alisema katika mechi ya leo wanatarajia kuwashusha dimbani wachezaji wake nyota ili kuhakikisha wanaitoa nishai Clouds, aliodai walikuwa wakiwakwepa mara kwa mara wakiomba nafasi ya kucheza nao.
"Tupo kamili kwa ajili ya kutoa kipigo kwa Clouds, hasa ikizingatiwa wamekuwa wakitukwepa mara nyingi, pia tumetoka kupoteza mechi mwishoni mwa wiki iliyopita, hivyo hatutaki tena tufanye makosa," alisema Ticotico ambaye ametamba atakuwepo dimbani kuwaongioza vijana wake kusaka ushindi.
Baadhi ya nyota wa timu hiyo wanaotarajiwa kushuka dimbani leo ni pamoja na Wisdom Ndhlovu, Herry Morris, Majaliwa, Said Swedi 'Panucci', Shija Katina, Waziri Mahadhi 'Mandieta' na wengineo, huku wapinzani wao wakitarajiwa kuwategemea zaidi akina Shafii Dauda, Mbwiga Mbwiguke, Lwambano, Ally Mayay 'Tembele', Gofrey Lea na wengineo