Kikosi cha Simba |
MECHI ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya mabingwa watetezi Simba dhidi ya wenyeji Prisons iliyofanyika juzi kwenye Uwanja wa Sokoine jijini hapa imeingiza Sh. milioni 40.8.
Akizungumza jana, mkuu wa kituo katika kanda hiyo, Blassy Kiondo, alisema jumla ya mashabiki 8,165 walilipa kiingilio cha Sh. 5,000 kila mmoja kushuhudia mchezo huo.
Kiondo alisema kuwa kila klabu imepata jumla ya Sh. milioni 8.7 na kiasi kingine kimekwenda katika taasisi nyingine kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania.
Alisema kuwa kiasi kilichopatikana juzi hakijavunja rekodi iliyowekwa katika mechi ya kwanza ya ligi kuu msimu huu uwanjani hapo iliyowakutanisha Prisons na Yanga ambapo Sh. milioni 50 zilipatikana.
Alisema pia hali ya hewa ya mvua jijini Mbeya nayo ilichangia kupunguza idadi ya mashabiki katika mechi ya juzi.
Hata hivyo, habari za mtaani zinadai kuwa wimbi kubwa la mashabiki lilioibuka kuishabikia timu iliyopanda daraja hadi Ligi Kuu ya Bara msimu ujao ya Mbeya City Council linaweza kuwa moja ya sababu za kupungua kwa mapato katika mechi hiyo.
Simba inayoshika nafasi ya tatu katika msimamo, ilishinda mechi hiyo kwa bao 1-0 na kuifanya ifikishe pointi 31, tano nyuma ya vinara Yanga ambao wana mechi moja mkononi. Azam ni ya pili ikiwa na pointi 36 sawa na vinara, lakini wanabaki katika nafasi ya pili kutokana na tofauti nzuri ya magoli. Azam kama Simba wamecheza mechi 17.
CHANZO:NIPASHE
No comments:
Post a Comment