Na BONIFACE WAMBURA
SIMANZI katika medai ya soka baada ya mwishoni mwa wiki wachezaji wawili mmoja wa zamani na mwingine anayekipiga Polisi Tabora kufariki dunia.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
mchezaji wa zamani wa timu za Coastal Union, TPC na Taifa Stars, Behewa
Ali Sembwana (72) kilichotokea jana usiku (Machi 31 mwaka huu) mkoani
Tanga.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti
Sembwana akiwa mchezaji, alitoa mchango mkubwa kwa timu mbalimbali
alizochezea, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
Sembwana
aliyekuwa akicheza wingi ya kulia alidumu katika Taifa Stars kwa miaka
kumi, kama ilivyokuwa kwa kombaini ya Mkoa wa Tanga (Tanga Stars)
aliyoiwakilisha katika michuano ya Kombe la Taifa (Taifa Cup).
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Sembwana, Chama cha Mpira wa Miguu
Mkoa wa Tanga (TRFA) na klabu ya Coastal Union na kuwataka kuwa na
subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko
yanatarajiwa kufanyika leo (Aprili 1 mwaka huu) kijijini kwake Lusanga,
Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Mungu aiweke roho ya marehemu Sembwana
mahali pema peponi. Amina
Aidha TFF limepokea kwa masikitiko taarifa za
kifo cha mshambuliaji wa timu ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ya Polisi
Tabora, Regan Mbuta kilichotokea jana (Machi 31 mwaka huu) usiku kwa
ajali ya pikipiki mjini Tabora.
Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora
(TAREFA), Yusuf Kitumbo, marehemu anatarajiwa kusafirishwa leo (Aprili 1
mwaka huu) kwenda kijijini kwao Kimamba, Wilaya ya Kilosa mkoani
Morogoro kwa ajili ya maziko.
Msiba
huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kwani Mbuta alikuwa mmoja wa
washambuliaji tegemeo wa Polisi Tabora, na bao lake la mwisho
aliyoifungia timu ilikuwa kwenye mechi ya mwisho ya FDL msimu huu dhidi
ya Pamba ya Mwanza iliyochezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
inatoa pole kwa familia ya marehemu Mbuta, TAREFA na klabu ya Polisi
Tabora na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito. Mungu aiweke roho ya marehemu Mbuta mahali
pema peponi. Amina