Hamad Juma akichuana na Messi siku ya pambano la Coastal na Simba Taifa |
Hata hivyo beki huyo wa pembeni, aliyepandishwa kikosi cha kwanza toka timu ya vijana msimu huu, amesema anajisikia fahari kubwa kuwalaza mapema mashabiki wa Simba walioamini wangeshinda.
Akizungumza na MICHARAZO, Hamad alisema kila akikaa na kufikiria alichokifanya kwenye uwanja wa Taifa, hushindwa kujiamini kama ni yeye kutokana na ukweli wapinzani wao walisheheni nyota watupu.
Hamad alisema maamuzi aliyoyafanya mara baada ya beki wa Simba, Omar Salum kuzembea kuokoa mpira hakutarajia, lakini yaliweza kuwapa bao pekee lililoipa Coastal pointi tatu muhimu.
"Huwa nashindwa kuamini kama ni mimi niliyefunga bao lile na kuizamisha Simba, hata hivyo nashukuru kwa kusaidia Coastal na kuweka rekodi ya kuifunga timu kubwa kama ya Simba," alisema.
Alisema ushindi huo ulikuwa muhimu kwao ikizingatiwa kocha wao Yusuph Chipo aliwaamini vijana na kuwapanga katika pambano hilo timu yao ikitoka kufungwa mabao 4-0 na Azam.
Beki huyo alifunga bao hilo dakika ya 44 na kudumu hadi mwisho na kuifanya Simba ipoteze mechi ya nne katika ligi ya msimu huu na kuiacha ikibakia kwenye nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo.
Simba pia ilishapoteza mechi nyingine tatu mbele ya Azam, Mgambo JKT na JKT Ruvu na kutishia kukosa uwakilishi wa nchi kwa mara ya pili mfululizo kutokana kutanguliwa na Azam, Yanga na Mbeya City.